Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ahmad Al-Qattan, Mwenyekiti wa Jumuiya ya "Kauluna wal-'Amal" na mwanazuoni wa Kisunni wa Lebanon, katika msimamo wake wa kisiasa wa kila wiki alisisitiza kuwa: Madrasah ya Karbala imeufundisha Umma jinsi ya kusimama imara juu ya haki na kupambana na dhulma, bila kujali ukubwa wa kujitolea na mhanga unaohitajika katika njia hiyo.
Akirejelea kiwango kikubwa cha mateso, mitihani na mabalaa yaliyomkumba Imam Hussein (as) pamoja na Ahlul-Bayt wake, alibainisha kwamba; pamoja na magumu yote hayo, walibaki kuwa bendera iliyoinuliwa kwa fahari, hawakurudi nyuma hata kidogo, wala hawakuacha misingi na maadili yao.
Sheikh Al-Qattan aliunganisha mwenendo huu wa kihistoria na hali halisi ya zama hizi huku akisisitiza: Mwelekeo huu wa Hussein unaonekana wazi katika kusimama imara Mujahidina wa Lebanon na uthabiti wao katika kushikamana na haki bila kuchukua msimamo wa upande wowote, licha ya kuachwa peke yao na ulimwengu.
Aidha, alisema kuwa; mfano huu umejitokeza kwa sura yake nzuri zaidi katika Ukanda wa Ghaza, ambapo wananchi wake wameonesha ushujaa mkubwa kwa kusimama kidete mbele ya watu wa batili na dhulma, na kuendelea kushikamana na haki licha ya changamoto na mashinikizo makubwa wanayokabiliana nayo.
Maoni yako