Jumapili 21 Juni 2026 - 13:15
Baadhi ya Nchi za Ghuba Kuzuia Kufanyika Maombolezo ya Hussein ni Kurudia Sera za Utawala wa Baath

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji amesema: Leo ni wajibu kwa maadui wa Imam Hussein (as) kuwa na hofu kwamba mwisho wao utakuwa kama mwisho wa utawala wa zamani wa Saddam.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji, Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Najaf Ashraf, katika khutba za Swala ya Ijumaa alizozitoa katika Husainiya Kuu ya Fatimiya mjini Najaf Ashraf, akizungumzia hati ya maelewano ya hivi karibuni kati ya Iran na Marekani alisema: Kuna makubaliano ya kimataifa kwamba hati hii ya maelewano imethibitisha kuwa Iran imeshinda na ni yenye nguvu, na kwamba juhudi zote za kuiangusha Iran zimefeli.

Aliongeza: Rais wa Marekani amekiri kwamba walishindwa katika juhudi zao za kuiangusha serikali ya Ira, ukweli ni kwamba kulifanyika makumi ya majaribio ya kuiangusha serikali hii, lakini yote yalifeli, hali hii imetokana na mwamko wa wananchi, uongozi, na mafundisho ya Hussein ambayo yamejaza nyoyo na fikra zao, hata hivyo, jeraha bado linatokwa damu, na majeraha yetu hayatapona isipokuwa kwa kuondoka tawala dhalimu na waporaji, nasi tutaendelea kusubiri mpaka kudhihiri kwa Imam wetu wa Zama (a.f.), tukisema:

«أین الطالب بذحول الأنبیاء وأبناء الأنبیاء، أین الطالب بدم المقتول بکربلاء»

"Yuko wapi mwenye kudai kisasi cha damu za Manabii na wana wa Manabii? Yuko wapi mwenye kudai kisasi cha damu ya aliyeuawa Karbala?"

Mapokezi ya Familia za Mashahidi wa Minab katika Haram Takatifu ya Alawi

Imamu wa Sala ya Ijumaa wa Najaf Ashraf, akizungumzia masuala ya ndani, alisema: Mapokezi yaliyofanywa na Haram Takatifu ya Alawi kwa familia za wanafunzi mashahidi wa shule ya Minab nchini Iran yanaonesha uhusiano na mshikamano uliopo kati ya mataifa ya Iraq na Iran.

Alisema kuwa; Ataba Takatifu zimekuwa mstari wa mbele katika kuonyesha uhusiano huu, kwa sababu suala hili ni suala la dini, madhehebu na ubinadamu, si suala la mipaka ya kijiografia, ukabila au maslahi ya kiuchumi.

Kusisitiza Mshikamano na Taifa la Lebanon

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji, akizungumzia masuala ya kimataifa, alisema: Mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya watu wetu nchini Lebanon, ambayo bado yanaendelea hadi sasa, ni ukiukaji wa makubaliano yote na haki zote za binadamu.

Tunaiunganisha sauti yetu na Mashia wa Lebanon, Hizbullah nchini Lebanon na wananchi wote wa Lebanon, na tunautaka ulimwengu usimame dhidi ya mauaji haya.

Kwa Nini Wanaogopa Maombolezo ya Hussein?

Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Najaf Ashraf aliendelea kwa kusema: Hapa tunalijibu swali hili: Kwa nini wanapigana na Imam Hussein (as)? Na kwa nini wanaogopa maombolezo ya Hussein?

Leo baadhi ya nchi za Ghuba zinapiga marufuku shairi za Hussein na zinatumia sera zilezile zilizokuwa zikitumiwa na utawala wa zamani wa Baath.

Aliendelea: Sasa nitawasomeeni baadhi ya maamuzi ya utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya marasim za Hussein.

Katika barua ya tarehe 25/03/2001 iliyotumwa kwa makamanda wa vitengo mbalimbali chini ya kichwa cha "Maelekezo ya Mwezi wa Muharram", ilielezwa kwamba:

1. Matembezi ya mazuwaru (Mashaya) yamepigwa marufuku kabisa, na hatua kali zichukuliwe dhidi ya yeyote anayeyafanya.

2. Kupiga matam au kujipiga vifua mitaani au majumbani kumepigwa marufuku kabisa.

3. Wanaotambulika rasmi kama washairi hawaruhusiwi kusoma tenzi mitaani au kupitia vipaza sauti, bali ndani ya misikiti pekee.

4. Kanda za kaseti zikaguliwe na usambazaji wake katika maduka uzuiwe.

5. Upishi wa vyakula ufanyike ndani ya nyumba na si mitaani; na yeyote atakayekiuka maelekezo hayo afikishwe mahakamani.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji alisisitiza: Lakini Imam Hussein (as) alibaki hai katika nyoyo za watu, huku maadui wa Imam Hussein (as) wakitoweka.

Na leo ni wajibu kwa maadui wa Imam Hussein (as) kuwa na hofu kwamba; mwisho wao utakuwa kama mwisho wa utawala wa zamani wa Saddam.

Tunapaswa kuwashukuru wananchi wa Iraq na Mashia wote wa Ahlul-Bayt (as) kwa kuhuisha msiba huu mchungu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha