Alhamisi 18 Juni 2026 - 17:54
Australia Yachunguza Taarifa za Unyanyasaji wa Israel dhidi ya Wanaharakati wa “Msafara wa Sumud”

Hawza/ Kufuatia kuibuka kwa taarifa zinazodai kuwepo kwa kukamatwa, mateso na vitendo vya udhalilishaji dhidi ya baadhi ya wanaharakati wa “Msafara wa Kimataifa wa Sumud”, serikali ya Australia imetangaza kuanza uchunguzi rasmi kuhusu namna Israel ilivyoamiliana na raia wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Shirika la Habari la Anadolu, wanaharakati wa Australia waliokuwa sehemu ya “Msafara wa Kimataifa wa Sumud” jana walikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia, Penny Wong.

Wanaharakati hao walieleza kwamba; katika mkutano huo suala la namna walivyotendewa na Israel lilijadiliwa, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia aliahidi kwamba Polisi wa Shirikisho la Australia (AFP) watachunguza madai yaliyotolewa, yakiwemo madai yanayohusiana na vitendo vya udhalilishaji na ukiukaji wa haki zao.

Juliet Lamont, mmoja wa wanaharakati wa msafara huo, alisema: "Wong anaamini kwamba tulitekwa nyara, tuliteswa, tulikamatwa, na baadhi yetu pia walifanyiwa vitendo vya unyanyasaji."

Polisi wa Shirikisho la Australia pia walitoa taarifa wakitangaza kuwa uchunguzi rasmi kuhusu suala hilo umeanza. Aidha, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Australia ambaye jina lake halikuwekwa wazi alisema kuwa; Penny Wong anaunga mkono kufanyika kww uchunguzi huru na wa uwazi kuhusu jambo hilo.

Msemaji huyo aliongeza kwamba; Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia hapo awali pia alikuwa amelaani hatua za maafisa wa Israel pamoja na mwenendo wa Ben Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Israel, ambaye amewekwa chini ya vikwazo vya Australia.

Kwa upande mwingine, Ubalozi wa Israel mjini Canberra ulitoa taarifa kupitia mtandao wa kijamii wa X, ukikanusha madai yaliyotolewa na wanaharakati wa “Msafara wa Kimataifa wa Sumud” kuhusu kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji na matumizi ya nguvu dhidi yao.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha