Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Islamic Analysis, Umoja wa Vijana wa Uturuki (TGB) umetangaza uamuzi wake wa kuandaa maandamano makubwa ya kupinga mkutano wa NATO ambao umepangwa kufanyika mwezi ujao katika mji mkuu wa Uturuki.
Umoja huo ulieleza kwamba utaandaa maandamano ya kupinga mkutano wa NATO unaotarajiwa kufanyika tarehe 7 na 8 Julai 2026 mjini Ankara. TGB imewataka wazalendo wote kushiriki katika mkusanyiko mkubwa utakaofanyika siku ya Jumamosi tarehe 4 Julai katika eneo la Kızılay, Ankara, na imesisitiza kwamba mkutano huo unapaswa kufutwa.
Katika taarifa yake rasmi, umoja huo ulikosoa vikali kufanyika kwa mkutano huo na kusema: "NATO, ambayo ni shirika kubwa zaidi la kigaidi duniani kwa mtazamo wetu, itafanya mkutano wake tarehe 7 na 8 Julai 2026 katika mji mkuu wa nchi yetu, Ankara, wanataka kutandaza kivuli cha nyota nyeusi ya NATO juu ya Ankara, makao ya mapambano yetu ya kitaifa na mji mkuu wa jamhuri yetu, NATO ya uvamizi, ambayo inaunga mkono mauaji ya halaiki, imehusishwa na mapinduzi ya kijeshi, imekuwa msaidizi wa makundi ya FETO na PKK, na imeizingira Uturuki, haiwezi kuuchafua mji mkuu wetu."
Katika taarifa hiyo ilisisitizwa kuwa; mkutano wa NATO uliopangwa kufanyika tarehe 7 na 8 Julai 2026 unapaswa kufutwa mara moja, hakuna Nafasi ya Uturuki Katika Mipango ya Umwagaji Damu ya NATO
TGB pia ilitangaza kuwa itachukua msimamo thabiti dhidi ya mipango ya mataifa yenye nguvu duniani inayolenga Uturuki. Katika tamko lake ilisema: "Katika mipango ya umwagaji damu ya NATO, hakuna nafasi inayoweza kuamuliwa kwa Uturuki dhidi ya NATO, shirika la vita la Marekani na Israel, tutaungana chini ya bendera ya hilali na nyota. Sisi sote ni Ömer Halisdemir, na tutakuwa askari watakaoisimamisha NATO, kuanzia Trump hadi Mark Rutte, hatuwataki wahalifu wa ubeberu wa Kizayuni, wauaji wa halaiki na maadui wa Uturuki mjini Ankara."
Kwa upande mwengine Umoja wa Vijana wa Uturuki umewaalika wazalendo wote na raia wa rika zote pamoja na wenye mitazamo mbalimbali ya kisiasa kushiriki katika maandamano hayo.
Taarifa hiyo ilihitimishwa kwa wito ufuatao: "Tunawaalika wazalendo wote, bila kujali mtazamo wao wa kisiasa au umri wao, kushiriki katika maandamano yatakayoanza siku ya Jumamosi tarehe 4 Julai saa 10:00 jioni (16:00) kutoka Mtaa wa Mashrutiyet katika eneo la Kızılay, na kwa kupaza sauti kubwa: ‘NATO adui wa Uturuki, toka Ankara!’ Ili kuimarisha madai haya, jiungeni na maandamano yetu, na tukutane Ankara."
Waandaaji wa maandamano hayo walitangaza kwamba, sambamba na kampeni hiyo, ukusanyaji wa saini za kidijitali unaendelea kupitia tovuti ya imzaver.com.
Maelezo: Ömer Halisdemir alikuwa mwanajeshi wa Uturuki aliyekuwa na mchango mkubwa katika kuzuia na kubadilisha mwelekeo wa jaribio la mapinduzi la kundi la Fethullah Gülen dhidi ya serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan mwaka 2016.
Maoni yako