Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Sayyid Riyadh Saeed al-Hakim, mwalimu wa Hawza, akiwa mzungumzaji mkuu wa hafla hiyo, alisisitiza kwamba; Qur’ani Tukufu ni muujiza wa milele wa Uislamu na ni miongoni mwa nguzo muhimu zaidi za kuhifadhi utambulisho na misingi ya Umma wa Kiislamu.
Alieleza kwamba; tofauti na miujiza ya muda iliyohusiana na Mitume waliotangulia, athari na uongofu wa Qur’ani unaendelea katika vizazi vijavyo, na jambo hili linaakisi tabia ya Qur’ani ambayo haifungamani na wakati wala zama fulani.
Bw. al-Hakim aliongeza kuwa; moja ya majukumu makuu ya Qur’ani ni kuhifadhi utambulisho wa jamii ya Waislamu na kuulinda dhidi ya upotovu na mgawanyiko kupitia kuhifadhi matini ya Mwenyezi Mungu ambayo ndiyo msingi wa kanuni na hakika ya Uislamu.
Alibainisha kwamba; licha ya kupita zaidi ya karne kumi na nne tangu kuanza kwa ujumbe wa Mtume Muhammad (saww), Qur’ani bado ni sababu kuu ya kuhifadhi utambulisho wa kidini na wa kiroho wa Waislamu duniani kote.
Mwalimu huyu wa Hawza pia alirejelea riwaya nyingi kutoka kwa Mtume Mtukufu wa Uislamu, Muhammad (saww), na Maimamu wa Ahlul-Bayt (a.s.), ambazo zinasisitiza umuhimu wa kuisoma Qur’ani kwa sauti nzuri na kwa usahihi.
Alisema kwamba; usomaji wa namna hiyo husaidia kuwasilisha maana ya Qur’ani kwa ufanisi zaidi na huimarisha uhusiano wa kihisia na wa kiroho wa Waumini na ujumbe wake wa mbinguni.
Chanzo: Karbala Now Agency.
Maoni yako