Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Harakati ya Umma ya Lebanon katika taarifa yake, imelaani mashambulizi ya mara kwa mara ya Kizayuni yanayofanywa kusini mwa Lebanon na Biqaa pamoja na ukiukwaji wa kila siku wa mamlaka ya Lebanon katika mazingira ya kimya cha kutatanisha cha kimataifa na kushindwa kwa taasisi za kimataifa kukomesha sera za uchokozi na ugaidi ambazo adui wa Kizayuni anazitekeleza dhidi ya Lebanon na wananchi wake.
Katika taarifa hiyo imeelezwa:
“Mbele ya vitisho vya mara kwa mara vya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa uvamizi, kuhusu kulenga vitongoji vya kusini mwa Beirut na kupanua wigo wa mashambulizi, Harakati ya Umma inasisitiza kwamba; vitisho hivi si jambo jipya kwa utawala ambao kimsingi umejengwa juu ya uvamizi, mauaji na ugaidi, sera ya kutisha na kulazimisha haitafanikiwa kamwe kuvunja azma ya wananchi wetu wala kudhoofisha uthabiti na msimamo wao, kwani uzoefu wa zamani umethibitisha kwamba, nia ya mataifa yanayoamini haki na uhuru wao ina nguvu zaidi kuliko mashine zote za kivita na za uchokozi.”
Harakati hiyo, sambamba na kueleza imani yake kubwa kwa wananchi wanaopambana ambao wanaonesha mifano mizuri zaidi ya kusimama imara na kujitolea, ilitoa shukrani kwa watu wanaokabiliana kwa ujasiri na ushujaa, wanaosisitiza haki ya Lebanon ya kutetea ardhi yake, mamlaka yake na heshima ya wananchi wake.
Harakati ya Umma ilibainisha: “Kutegemea ahadi za Marekani au mashinikizo ya kimataifa kwa ajili ya kuilinda Lebanon, mara nyingi kumeonesha kushindwa kwake, kwa sababu ulinzi wa taifa na kuhifadhi mamlaka yake huwezekana tu kupitia kushikamana na haki za kitaifa na kukataa aina yoyote ya ushawishi wa kisiasa na maagizo kutoka nje.”
Kuilinda Lebanon kunahitaji kiwango cha juu kabisa cha mshikamano na umoja miongoni mwa wananchi wake
Harakati hiyo pia ilisisitiza tena msimamo wake wa kudumu wa kupinga aina yoyote ya kuhalalisha uhusiano na adui wa Kizayuni, na inaamini kwamba; mazungumzo yoyote ya moja kwa moja ya kisiasa na utawala huo nje ya mfumo mpana wa kitaifa na bila kupata haki kamili ni kutoka nje ya misingi ya Umma na ni kuharibu haki za kitaifa na za kijamii ambazo zimegharimiwa kwa kujitolea kwa kiwango kikubwa.
Mwisho, Harakati ya Umma iliwataka wananchi wa Lebanon kuimarisha zaidi umoja wa kitaifa na mshikamano wa ndani, na ikaonya dhidi ya juhudi za kuanzisha fitina na mifarakano kwa ajili ya kutumikia miradi na malengo ya adui, huku ikisisitiza kwamba; kuilinda Lebanon kunahitajia kiwango cha juu kabisa cha mshikamano na umoja miongoni mwa wananchi wake.
Maoni yako