Ijumaa 29 Mei 2026 - 20:00
Rais wa Cyprus Kaskazini: Sitafanya Mazungumzo na Serikali Inayoua Watoto

Hawza/ Rais wa Jamhuri ya Cyprus Kaskazini amekosoa vikali ushirikiano wa kijeshi na kisiasa wa Cyprus Kusini na Israel, na kusisitiza kuwa; serikali ya Benjamin Netanyahu kutokana na mauaji ya watoto huko Ghaza haina uhalali wa kimaadili wa kufanya mazungumzo wala kuaminiwa.

Kwa mujibu wa kitengo cha kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Rais wa Jamhuri ya Kituruki ya Cyprus Kaskazini amekosoa vikali kuongezeka kwa ushirikiano kati ya sehemu ya Kigiriki ya Cyprus na Israel pamoja na India, na kusisitiza kwamba; hatajihusisha na “serikali yoyote inayoua watoto.”

Tufan Erhürman, rais wa Jamhuri ya Kituruki ya Cyprus Kaskazini, katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Uturuki cha “A Haber”, alitathmini maendeleo ya hivi karibuni katika eneo la Mashariki ya Mediterania, mikakati ya kikanda ya serikali ya Cyprus Kusini na mwenendo wa ushirikiano na Uturuki, akirejelea hatua za serikali ya Cyprus ya Kigiriki, alisema kuwa; mwenendo huo umeongeza mvutano katika eneo hilo na kwamba miungano mipya imewaweka Waturuki wa Cyprus moja kwa moja katika mazingira ya tishio.

Erhürman huku akisisitiza kuwepo kwa uratibu kamili na Rajab Tayyib Erdogan, rais wa Uturuki, pamoja na serikali ya Uturuki katika masuala ya kidiplomasia na kiusalama, alisema: “Kuanzishwa kwa njia ya biashara katika eneo hili bila kuizingatia Uturuki na Waturuki wa Cyprus hakuwezekani wala hakutakuwa na manufaa.”

Pia alirejelea kuwepo kwa ndege za kivita aina ya F-16 za Ugiriki katika uwanja wa ndege wa “Andreas Papandreou” huko Cyprus Kusini na kupanuliwa kwa matumizi ya kijeshi ya kambi ya anga ya “Paphos” ndani ya mfumo wa makubaliano ya eneo hilo na Israel, Marekani na Ufaransa, na akaongeza: “Kwa vitendo, mnatoa kambi ya anga inayosimamiwa na Cyprus Kusini mikononi mwa nchi za kigeni.”

Erhürman pia alizungumzia taarifa na madai kuhusu ununuzi wa ardhi na vijiji hukk Cyprus Kusini na raia wa Israel, na akasema kwamba; ingawa bado hakuna taarifa za uhakika na zilizothibitishwa kuhusu suala hilo, lakini dalili za kutoridhika kwa kiwango kikubwa zinaonekana miongoni mwa jamii ya Kigiriki ya Cyprus. Akirejelea kufanyika kwa maandamano ya kupinga hali hiyo katika eneo hilo alisema: “Mnaona wazi kwamba wananchi wa Cyprus Kusini pia hawaridhiki na suala hili.”

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, huku akiikosoa vikali serikali ya Benjamin Netanyahu katika eneo hilo, alisisitiza: “Haiwezekani kwangu kuiamini au kuiheshimu serikali yoyote inayoua watoto na kuifanya kuwa mshirika wa mazungumzo.”

Mwishoni, rais wa Cyprus Kaskazini huku akisisitiza uratibu wa kisiasa na Ankara katika suala la Cyprus alisema: “Haiwezekani kuchukua msimamo kuhusu suala la Cyprus bila kushauriana na Jamhuri ya Uturuki, mahusiano kati ya Cyprus na Uturuki yanapaswa kujengwa juu ya mazungumzo, si maamuzi ya upande mmoja.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha