Kwa mujibu wa kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Wapalestina katika mji wa Ghaza wameusindikiza mwili wa Muhammad Odeh maarufu kwa jina la “Abu Amr”, mmoja wa makamanda waandamizi wa “vikosi vya Izzuddin Qassam”, pamoja na mke wake na watoto wake; waliouawa kishahidi kufuatia mashambulizi ya mabomu dhidi ya jengo la makazi katika mji huo.
Mazishi hayo yalifanyika saa chache baada ya vyanzo vya ndani kuripoti kuuawa kwa Odeh na familia yake kufuatia shambulio la anga la Israel.
Baada ya shambulio hilo, jeshi la Israel lilitangaza kwamba lilimlenga Odeh; mtu ambaye lilimtaja kuwa kamanda mpya wa “vikosi vya Izzuddin Qassam”, tawi la kijeshi la Harakati ya “Hamas”.
Tangazo hili lilitolewa siku 11 baada ya kuuawa kwa kamanda wa awali wa vikosi hivyo, Izzuddin Al-Haddad, katika shambulio la anga la Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza.
Muhammad Odeh ni nani?
Muhammad Odeh ni mmoja wa makamanda mashuhuri wa kijeshi katika Vikosi vya Qassam ambaye jina lake lilijitokeza kwa nguvu baada ya mfululizo wa mauaji yaliyowalenga makamanda waandamizi wa harakati hiyo wakati wa vita vya maangamizi dhidi ya Ukanda wa Ghaza.
Odeh alichukua uongozi wa “Vikosi vya Qassam” baada ya Izzuddin Al-Haddad; ambaye Israel ilitangaza tarehe 15 Mei mwaka huu kwamba imemuua.
Ripoti hizi zinaonesha kwamba; Odeh katika miezi ya hivi karibuni alikuwa mmoja wa watu wa karibu zaidi wa Al-Haddad, hususan katika suala la kujenga upya mfumo wa uongozi wa kijeshi baada ya kuuawa kwa baadhi ya makamanda mashuhuri.
Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za vyombo vya habari, Muhammad Odeh hapo awali alikuwa mkuu au msimamizi wa kitengo cha ujasusi wa kijeshi kinachohusishwa na “Vikosi vya Qassam”, na anatajwa kuwa mmoja wa akili muhimu zaidi za kiintelijensia ndani ya harakati hiyo.
Alikuwa na jukumu katika kukusanya na kuchambua taarifa za kijeshi zinazohusiana na jeshi la Israel, na pia alikuwa akisimamia uratibu kati ya vikosi vya uwanjani wakati wa operesheni ya “Mafuriko ya Al-Aqsa”.
Baadhi ya ripoti zimemtaja Muhammad Odeh kama “Mtu wa Kivulini” kutokana na kutokuwepo sana katika vyombo vya habari na uchache wa taarifa binafsi zinazojulikana kumhusu; pia hakuna picha nyingi mpya zinazopatikana kumhusu yeye, jambo linaloonyesha hali ya siri ya shughuli zake ndani ya mfumo wa kijeshi wa harakati hiyo.
Muhammad Odeh alikuwa sehemu ya juhudi za kimuundo zilizoongozwa na Izzuddin Al-Haddad kwa ajili ya kupanga upya mfumo wa uongozi wa Qassam baada ya kuuawa kwa Muhammad Deif, Muhammad Sinwar na baadhi ya makamanda wengine wa kijeshi.
Israel inasema kuwa; mara kadhaa imejaribu kumlenga na kumuua Odeh, iwe wakati wa vita au kabla yake, lakini hatua kali za kiusalama zilizokuwa zikizingatia harakati zake zilizuia mafanikio ya operesheni hizo.
Miongoni mwa majaribio hayo ni shambulio lililosababisha kubomolewa kwa nyumba ya baba yake katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza; nyumba ambayo baada ya usitishaji vita, mwezi Oktoba uliopita, ililengwa na katika shambulio hilo mwanawe mkubwa aliuawa kishahidi.
Maoni yako