Kwa mujibu wa kitengo cha kimataifa cha “Shirika la Habari la Hawza”, kufuatia kuongezeka kwa ukandamizaji dhidi ya wapinzani pamoja na vizuizi vinavyozidi kuongezeka dhidi ya uhuru wa kujieleza nchini Bahrain, kukamatwa kiholela kwa shakhsia za kidini kumeibua hisia kali za kulaaniwa. Sheikh Abdullah al-Daqqaq, mkurugenzi wa Hawza ya Wabahrain nchini Iran, kwa kulaani hatua hizi, amesisitiza kwamba; kuna ukiukwaji wa wazi wa haki za msingi za wanazuoni na wanafikra, matini ya taarifa yake ni kama ifuatavyo:
بسم الله الرحمن الرحیم
Tunalaani vikali hatua ya serikali ya Bahrain ya kuwakamata kiholela baadhi ya wanazuoni wa Kishia, hatua hii hatari ni ukiukwaji wa wazi wa uhuru wa kujieleza na wa itikadi, na ni uvamizi wa wazi dhidi ya haki za kidini na kiraia ambazo zimetambuliwa katika mafundisho ya mbinguni pamoja na sheria na mikataba ya kimataifa.
Kuwalenga wanazuoni, wanafikra na watu wenye uhuru wa kujieleza kwa tuhuma na visingizio visivyo na msingi, si tu kwamba hakutasaidia kuleta uthabiti na utulivu nchini, bali pia kutasababisha kuongezeka kwa mvutano na kuzidi mgogoro wa kisiasa na wa haki za binadamu nchini Bahrain; hasa kwa kuwa wanazuoni siku zote wamekuwa na nafasi muhimu katika kuhimiza mageuzi, pamoja na kuimarisha amani na utulivu wa kijamii.
Tunasisitiza kwamba; kuendelea kwa sera ya kuweka vikwazo dhidi ya uhuru wa kidini na kuzishughulikia shakhsia za kidini na za kielimu, kutapelekea kuongezeka kwa kutoridhika na mvutano katika jamii. Aidha, jukumu kamili la vitendo hivi pamoja na athari zake hasi dhidi ya usalama na utulivu wa kijamii liko juu ya serikali ya Bahrain.
Kwa msingi huo sisi:
Tunataka kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa wanazuoni wote na watu wote waliokamatwa kutokana na mitazamo yao ya kidini na kisiasa.
Tunataka kusimamishwa kwa sera ya kukamata kiholela na kuita watu katika vyombo vya usalama dhidi ya wananchi, wanazuoni na makhatibu wa dini.
Tunaziomba taasisi za haki za binadamu na mashirika ya kimataifa kutekeleza wajibu wao wa kisheria na wa kimaadili kuhusu ukiukwaji unaoendelea wa haki za binadamu nchini Bahrain.
Tunatangaza mshikamano wetu kamili na familia za waliokamatwa pamoja na wananchi wa Bahrain katika kudai haki, heshima ya kibinadamu na kulinda uhuru wa kijamii.
Maoni yako