Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, sambamba na ujio wa ujumbe kutoka Haram Quds Razavi katika eneo la Baltistan nchini Pakistan, bendera tukufu ya kuba la Haram takatifu ya Imam Ridha(a.s) ililetwa katika mji wa Skardu na kupokewa kwa mapokezi makubwa kutoka kwa wanazuoni, shakhsia za kidini na wapenzi wa Ahlul-Bayt(a.s); ujio ambao ulijaza mazingira ya eneo hilo kwa hali ya kiroho, mapenzi na utii kwa kizazi cha Mtume(s.a.w.w).
Ardhi ya Baltistan nchini Pakistan ilishuhudia mazingira yaliyojaa hali ya kiroho na mapenzi kwa Ahlul-Bayt (a.s), ambapo ujumbe wa wageni kutoka Haram tukufu ya Imam Ridha(a.s), ukiwa umeambatana na bendera tukufu ya kuba ya Imam huyo, uliingia katika mji wa Skardu Baltistan na kupokewa kwa uchangamfu mkubwa na wanazuoni pamoja na makundi mbalimbali ya wananchi.
Katika ujumbe huo walikuwemo Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Jalal Husayni, Naibu wa Usimamizi wa Haram Quds Razavi mjini Mashhad tukufu, Dkt. Kashani Mkuu wa Kitengo cha Kimataifa cha Haram Quds Razavi, pamoja na Muhammad Ridha Shafii, msomaji wa kimataifa wa Haram tukufu ya Razavi. Ujumbe huo pia uliileta bendera tukufu ya kuba ya Imam Ridha (a.s) hadi Baltistan Pakistan.
Mara tu walipowasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mji wa Skardu, Baltistan Pakistan, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Baqir al-Husayni, Mkuu wa Jumuiya ya Imamiyya Baltistan, Sheikh Zahid Husayn Zahidi, Naibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Sheikh Muhammad Jawad Hafidhi, Naibu wa Imam wa Sala ya Ijumaa ya Skardu, pamoja na kundi la wanazuoni na shakhsia za kidini waliwapokea wageni wa Haram ya Razavi.
Baada ya hapo, katika eneo la Ghambe Bazaar Skardu pia, chini ya uongozi wa Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Ahmad, Mkuu wa Jumuiya ya Imamiyya Ghambe Skardu, kundi la wanazuoni na waumini liliufanyia ujumbe huo mapokezi makubwa. Katika hafla hiyo, wageni wa Haram ya Razavi walihudhuria.

Kwa kuingia kwa ujumbe huo katika Msikiti Mkuu wa kati wa mji wa Skardu, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Muhammad Hasan Ja‘fari, Imam wa Sala ya Ijumaa na Jamaa wa Skardu anayejulikana kwa jina la “Mlinganiaji wa Umoja”, aliwapokea wageni hao. Baada ya kusimamishwa sala za Adhuhuri na Alasiri, hafla kubwa iliyohudhuriwa na wananchi wengi pamoja na wanazuoni ilifanyika.
Hafla hiyo ilianza kwa kisomo cha kupendeza cha aya za Qur’ani Tukufu kutoka kwa qari wa kimataifa Muhammad Ridha Shafii, jambo lililopokewa kwa pongezi na kuvutia hisia za waliohudhuria.
Baadaye, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Jalal Husayni katika hotuba yake kwa lugha ya Kifarsi alisema kuwa; anajiona kuwa mtumishi mdogo katika Haram tukufu ya Imam Ridha (a.s), na kwamba kilemba alichovaa ni zawadi kutoka katika mkono mubarak wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi.
Alisema kuwa; uwepo wake miongoni mwa wapenzi wa Ahlul-Bayt (a.s) ndani ya Baltistan ni fahari kwake, lakini wakati huo huo akataja kuondokewa na Kiongozi Shahidi kuwa ni huzuni kubwa.
Mwanazuoni huyo mashuhuri wa kidini alisisitiza kuwa, mfumo wa Kiislamu unasimama imara kwa nguvu na uthabiti, na kwamba mhimili wa Muqawama bado uko imara na unaendelea kutenda kazi.
Akirejelea kauli ya kihistoria ya Sayyidush-Shuhadaa Imam Hussein (a.s) aliposema: «مثلی لا یبایع مثله», alibainisha kuwa yale aliyoyaona nchini Pakistan ni taswira wazi ya utiifu kwa Wilayah, mapenzi kwa Ahlul-Bayt(a.s), na mafungamano ya kina ya wananchi na uongozi wa kidini.
Hujjatul-Islam Jalal Hussein pia, kwa niaba ya Astana Quds Razavi na taifa la Iran, aliwashukuru wanazuoni, waumini, wanawake, wasomi na wananchi wa Pakistan na kusema: Taifa la Pakistan katika mazingira magumu limesimama pamoja na Iran kama ndugu wa kweli na wa karibu.
Mwisho wa hafla hiyo, bendera tukufu ya kuba ya Haram takatifu ya Imam Ridha (a.s) iliwekwa mbele ya wananchi. Katika nyakati hizo, shauku, mapenzi na utii wa wapenzi wa Imam Ridha (a.s) vilitengeneza mandhari yaliyojaa hisia za kidini na hali ya kiroho, na mazingira ya mkutano huo yakajaa harufu ya imani na mapenzi.
Inafaa kutajwa kuwa ujumbe huu kutoka Haram tukufu ya Imam Ridha (a.s) umesafiri kwenda eneo la Baltistan kwa lengo la kutoa pole kwa familia za mashahidi waliojitolea maisha yao, pamoja na kuwajulia hali majeruhi wa matukio na maandamano ya hivi karibuni.
Maoni yako