Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Claudia Sheinbaum, Rais wa Mexico, Jumanne katika mkutano na waandishi wa habari alitangaza kuwa, nchi yake inakataa kujiunga na “Kamati ya Amani katika Ukanda wa Ghaza” iliyoanzishwa kwa pendekezo la White House kwa ajili ya kuamua hatima ya ujenzi upya na usimamizi wa ukanda huo.
Kwa mujibu wa ripoti ya tovuti ya Infobae, Sheinbaum akirejelea kwamba; Mexico inaitambua Palestina kama dola huru, alisisitiza kuwa, uwepo wa Palestina katika mpango wowote wa amani unaohusiana na Ghaza ni “muhimu” kwa ushiriki hai wa nchi yake. Akifafanua msimamo huo alisema: Tunatafuta amani katika kila jukwaa, lakini inapozungumziwa amani katika Mashariki ya Kati, ushiriki wa nchi zote mbili, yaani Israel na Palestina, ni muhimu, na kikao hiki hakikuundwa kwa mtazamo huo.
Uwepo wa Kialama Badala ya Ushiriki Rasmi
Licha ya kukataa uanachama kamili, Rais wa Mexico alitangaza kumteua Héctor Vasconcelos, mwakilishi wa nchi yake katika Umoja wa Mataifa, kuhudhuria kikao hicho kama mwangalizi. Lengo la hatua hiyo limetajwa kuwa ni kufuatilia mchakato wa mazungumzo na maamuzi yanayoweza kufikiwa mjini Washington, D.C..
Mkakati huu ni sawa na msimamo uliochukuliwa na Umoja wa Ulaya, ambapo hapo awali ilitangaza kuwa badala ya uanachama kamili, itahudhuria kikao hicho kama mwangalizi tu.
Mwaliko wa Trump na Wasiwasi Kuhusu Ukosefu wa Ukamilifu wa Mchakato wa Amani
Donald Trump, Rais wa Marekani, alimwalika binafsi Sheinbaum kujiunga rasmi na kamati hiyo. Kamati hiyo ambayo ilipangwa kufanya kikao chake Alhamisi tarehe 19 Februari mjini Washington, D.C., ilikuwa na jukumu la kubuni mfumo wa ujenzi upya na usimamizi wa ukanda wa Ghaza katika kipindi cha baada ya vita.
Vyombo vya habari vya Mexico viliandika kuwa; msimamo wa Mexico umechukuliwa katika hali ya kuwepo kwa ukosoaji wa kimataifa dhidi ya mchakato wa amani unaokosolewa kwa kukosa jukwaa jumuishi la mazungumzo. Kutokuwepo kwa Palestina kama upande rasmi wa mazungumzo katika kikao hicho kumewatia wasiwasi si Mexico pekee, bali pia wadau wengine wa kimataifa.
Kwa uamuzi huu, Mexico imesisitiza moja ya misingi ya sera yake ya mambo ya nje, nayo ni ushiriki wa wahusika wote wanaohusika katika mazungumzo yanayolenga kutatua migogoro ya kimataifa.
Maoni yako