Jumatatu 23 Februari 2026 - 13:40
Chemli ya Ramadhani | Surat Aal-Imran; toleo la Qur’ani katika kukabiliana na mashambulizi ya kitamaduni na kijeshi

Hawza/ Juzuu ya tatu ya Qur’ani Tukufu inajumuisha Surat Al-Baqara kuanzia aya ya 253 hadi mwisho wa sura, na Sura Aal-Imran hadi aya ya 93. Sura Aal-Imran, kwa kusisitiza umoja wa neno (tawhidi ya msimamo) na subira, inazungumzia kisa cha ukoo wa Imran, tukio la Mubahala, na aya “Shahida Allah” na “Malik al-Mulk”, na imesisitizwa kusomwa na kutafakariwa aya hizi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, katika masika ya Qur’ani, jalada la “chemli ya Ramadhani” pamoja na maelezo mafupi na yenye matumizi ya aya za Qur’ani Tukufu, yatakayotolewa na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ali Zarei, mwalimu wa Hawza na mtaalamu wa elimu za Qur’ani, litawasilishwa katika meza yenu ya futari enyi wasomi.

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu; tupo katika juzuu ya tatu ya Qur’ani Tukufu. Juzuu hii inarejelea Surat Al-Baqara kuanzia aya ya 253 hadi mwisho wa sura, na Sura Aal-Imran kuanzia mwanzo wa sura hadi aya ya 93.

Sura Tukufu ya Aal-Imran imeteremshwa Madina na ina aya 200. Mada ya msingi ya sura hii inalenga kubainisha kwamba; umoja, msimamo, subira na ustahimilivu ni mambo ya lazima kwa Waislamu katika kukabiliana na mashambulizi ya kitamaduni na kijeshi ya maadui. Bila umoja wa kauli, uvumilivu na subira, mwanadamu atashindwa mbele ya mashambulizi ya kitamaduni na kijeshi ya maadui.

Neno “Aal-Imran” limetajwa mara moja tu katika Qur’ani, nalo ni katika aya ya 33 ya sura hii:

“إِنَّ اللَّهَ اصْطَفَیٰ آدَمَ وَنُوحًا وَآلَ إِبْرَاهِیمَ وَآلَ عِمْرَانَ عَلَی الْعَالَمِینَ”


Hakika Mwenyezi Mungu alimchagua Adam na Nuh na ukoo wa Ibrahim na ukoo wa Imran juu ya walimwengu.

Imran alikuwa katika kizazi cha Nabii Ibrahim (amani iwe juu yake), na ni baba wa Maryam (amani iwe juu yake). Sura hii inasimulia kisa cha mke wa Imran na binti yao, ambaye ni Maryam (amani iwe juu yake). Pia ndani yake kuna kisa cha mjadala wa Mtume Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake na Aali zake) na Wakristo wa Najran, tukio la Mubahala, pamoja na kutajwa kuzaliwa kwa Maryam (amani iwe juu yake).

Aya ya kwanza na ya pili ya sura hii zinasema:


“بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِیمِ الم؛ اللَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَیُّ الْقَیُّومُ”

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Alif Lam Mim. Mwenyezi Mungu, hapana mola apasaye kuabudiwa isipokuwa Yeye, Aliye Hai, Msimamizi wa kila kitu.

Kwa mujibu wa Mtume Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake na Aali zake), aya hizi ni miongoni mwa Jina Kuu (Ism al-A’dham) la Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na amesema kwamba Jina Kuu la Mwenyezi Mungu limeteremshwa katika sura tatu:

Moja lipo katika Sura Tukufu ya Al-Baqara, nayo ni Ayatul-Kursi; Moja lipo katika sura hii, nayo ni aya hizi za mwanzo; Na jengine lipo katika Sura Taha ambapo amesema:


“وَعَنَتِ الْوُجُوهُ لِلْحَیِّ الْقَیُّومِ”


Na nyuso zote zitanyenyekea mbele ya Aliye Hai, Msimamizi wa kila kitu.

Aya ya 18 ya Sura Tukufu ya Aal-Imran inajulikana kama aya ya “Shahida Allah”:


“شَهِدَ اللَّهُ أَنَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ وَالْمَلَائِکَةُ وَأُولُوا الْعِلْمِ قَائِمًا بِالْقِسْطِ  لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِیزُ الْحَکِیمُ”

Mwenyezi Mungu anashuhudia kwamba hapana mola isipokuwa Yeye, hali ya kuwa ni Mwenye kusimamisha uadilifu; na malaika na wenye elimu pia wanashuhudia kwamba hapana mola isipokuwa Yeye, Mwenye nguvu asiyeshindika, Mwenye hekima.

Mtume Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake na Aali zake) amesema kwamba yeyote atakayeisoma aya hii, Mwenyezi Mungu Mtukufu ataumba malaika sabini elfu watakaomuombea msamaha msomaji huyo hadi Siku ya Kiyama.

Aya ya 26 na 27 za sura hii zinasema:


“قُلِ اللَّهُمَّ مَالِکَ الْمُلْکِ تُؤْتِی الْمُلْکَ مَنْ تَشَاءُ وَتَنْزِعُ الْمُلْکَ مِمَّنْ تَشَاءُ وَتُعِزُّ مَنْ تَشَاءُ وَتُذِلُّ مَنْ تَشَاءُ  بِیَدِکَ الْخَیْرُ  إِنَّکَ عَلَیٰ کُلِّ شَیْءٍ قَدِیرٌ”

Sema: Ewe Mwenyezi Mungu, Mmiliki wa ufalme! Unampa ufalme umtakaye na unamnyang’anya ufalme umtakaye; unamtukuza umtakaye na unamdhalilisha umtakaye; kheri yote iko mkononi Mwako; hakika Wewe ni Muweza juu ya kila kitu.

“تُولِجُ اللَّیْلَ فِی النَّهَارِ وَتُولِجُ النَّهَارَ فِی اللَّیْلِ  وَتُخْرِجُ الْحَیَّ مِنَ الْمَیِّتِ وَتُخْرِجُ الْمَیِّتَ مِنَ الْحَیِّ  وَتَرْزُقُ مَنْ تَشَاءُ بِغَیْرِ حِسَابٍ”


Unaingiza usiku katika mchana na unaingiza mchana katika usiku; unamtoa aliye hai kutoka kwa mfu na unamtoa mfu kutoka kwa aliye hai; na unamruzuku umtakaye bila hesabu.

Imam Ja'far al-Sadiq (amani iwe juu yake) amesema kwamba: Mtume Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake na Aali zake) amesema: Pale Mwenyezi Mungu Mtukufu alipokusudia kuteremsha Fatihatul-Kitab, Ayatul-Kursi na aya hizi mbili za Aal-Imran, aya hizo zilijining’iniza kwenye Arshi kwa namna kwamba hapakuwa na pazia kati yao na Mwenyezi Mungu, na zikase­ma: “Mola wetu! Unatutuma katika makazi ya dhambi na kwa watu wanaokuasi, ilhali sisi tumeambatanishwa na Arshi na utakatifu Wako?”

Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: “Kwa izza na utukufu Wangu, hakuna mja yeyote atakayewasoma baada ya Sala za faradhi isipokuwa nitamweka katika Pepo ya juu pamoja na neema zake; na nitamtazama kila siku mara sabini; na kila siku nitamtimizia haja zake sabini, ndogo zaidi ikiwa ni kumsamehe; na nitamlinda dhidi ya kila adui na nitamnusuru juu ya maadui zake; na hakuna kitakachomzuia kuingia Peponi isipokuwa kifo.”

Ni muhimu kuhifadhi aya hizi, kuzisoma na kuzitafakari, jambo ambalo ni wosia uliosisitizwa wa Maimamu Maasumina (amani iwe juu yao) kwa Mashia.

Na amani iwe juu yenu na rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka Zake.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha