Jumamosi 14 Februari 2026 - 11:00
Wananchi wa Pakistan washiriki kwa wingi katika matembezi ya kifahari ya maadhimisho ya Mapinduzi ya Kiislamu

Hawza/ Sambamba na maadhimisho ya miaka arobaini na saba tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, miji mbalimbali ya Pakistan ilishuhudia kufanyika matembezi na mikusanyiko mikubwa ambapo washiriki walitangaza mshikamano wao na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, huku wakilaani sera za Marekani na utawala wa Kizayuni.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, kutokana na mnasaba wa kumbukumbu ya miaka 47 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, kutokana na juhudi za Taasisi ya Tehreek Bedari Ummat-e-Mustafa Pakistan, matembezi na mikusanyiko mikubwa ilifanyika katika miji mbalimbali ya Pakistan. Programu hizi zilifanyika katika miji kama Lahore, Islamabad, Peshawar, Sialkot, Faisalabad, Multan, Karachi, Quetta na maeneo ya Gilgit-Baltistan, ambapo washiriki walitangaza mshikamano wao na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Maandamano makuu ya jiji la Lahore yalifanyika kuanzia Msikiti wa Mashuhada hadi jengo la Bunge la Jimbo la Punjab. Katika maandamano hayo, maelfu ya wanaume, wanawake na watoto walishiriki, huku wakipaza sauti za kaulimbiu kuonesha uungaji mkono wao kwa Ayatollah Sayyid Ali Khamenei na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na wakati huo huo wakiilaani Marekani na utawala wa Kizayuni.

Katika hafla hiyo, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Syed Jawad Naqvi, Mkuu wa Taasisi ya Tehreek Bedari Ummat-e-Mustafa Pakistan, katika hotuba yake alisema: “Katika kipindi cha miaka 36 iliyopita, Mapinduzi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Ayatollah al-Uzma Sayyid Ali Khamenei yamesimama imara mbele ya mfumo wa kibabe unaotaka kuyatawala mataifa, kupora rasilimali zao na kunyang’anya uhuru wao. Uadui wa Marekani haujaelekezwa tu dhidi ya nchi moja, mpango wa makombora au suala la nyuklia, bali mizizi yake imo katika kupinga ‘Uislamu halisi wa Muhammadi (s.a.w.w)’, uhuru wa Kiislamu na fikra ya muqawama.”

Aliendelea kusema: “Marekani hutumia kaulimbiu kama mazungumzo, demokrasia na haki za binadamu kama zana za kuongeza mashinikizo na kufanikisha malengo yake ya kisiasa, ilhali kwa vitendo hutumia vikwazo, uingiliaji wa kijeshi na kuzusha machafuko ya ndani ili kuyadhoofisha mataifa huru.”

Mkurugenzi wa Hawza ya Kiislamu ya Urwatul Wuthqa Pakistan pia aliielezea Marekani kuwa ndie mdhamini mkuu wa utawala wa Kizayuni, akisema nchi hiyo inashiriki moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika dhuluma zinazofanywa dhidi ya watu wa Palestina, hasa huko Ghaza. Aidha, alieleza kuwa; ili kuudhoofisha Umma wa Kiislamu, kunachochewa pia migawanyiko ya kimadhehebu, itikadi za kitakfiri na vita vya uwakala.

Rais wa Tehreek Bedari Ummat-e-Mustafa Pakistan alisisitiza zaidi kwa kusema: “Kusalimu amri mbele ya ubeberu ni njia ya fedheha na maangamizi, ilhali muqawama ni njia yenye heshima, endelevu na yenye ufanisi kwa ajili ya uhai na maendeleo ya mataifa.”

Mwisho, alizitaka nchi za Kiislamu, ikiwemo Pakistan, kuwa macho dhidi ya hatari za udini wa kimadhehebu, fikra za kitakfiri na upenyezaji wa kigeni, na kujenga sera zao juu ya misingi ya uhuru wa Kiislamu, maslahi ya wananchi na umoja wa Umma wa Kiislamu. Aliongeza kuwa uzoefu wa kihistoria unaonesha kuwa njia ya heshima na maendeleo haipo katika kufuata madola ya kibabe, bali imo katika kujitegemea, umoja na muqawama wa heshima.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha