Jumanne 18 Novemba 2025 - 01:01
Sheikh Al-Khatib: Sisi Hatutajisalimisha

Hawza/ Makamu wa Rais wa Baraza Kuu la Kiislamu la Kishia nchini Lebanon alisema: Kudhalilisha sura ya dhehebu la Kishia nchini Lebanon ni njama dhidi ya Lebanon. Tulishika silaha kwa kuwa hakukuwa na serikali, na sisi ndio wenye uaminifu mkubwa zaidi kwa serikali kuliko mtu yeyote.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul Islam wal-Muslimin Sheikh Ali Al-Khatib, Makamu wa Rais wa Baraza Kuu la Kiislamu la Kishia nchini Lebanon, katika hafla ya kumbukumbu iliyofanyika katika mji wa Tamnin al-Tahta, alisisitiza kwamba utamaduni wa “ubinafsi”  ndio unaosukuma mazingira ya nchi. Je, wakati mwili unapopata homa, mwili mzima haufanyi kazi pamoja kupambana na ugonjwa? Ikiwa tunasadiki kwamba sisi ni watoto wa taifa moja, je haipendezi tuungane dhidi ya adui wa Kizayuni? Huko Magharibi, taswira na mtazamo umegeuzwa, lakini sisi tunapaswa kuungana dhidi ya adui muovu anayeua na kuwaangamiza wanadamu, ilhali sisi tunatishiana wenyewe kwa wenyewe. Baadhi wanamchukulia adui wa Kizayuni kuwa mshirika ili kupitia yeye kulipiza kisasi kutoka ndani ya Lebanon, na kwa sababu hiyo wanamwita adui huyo.

Akaongeza: Hapo zamani walialika Syria ije Lebanon, na hali ilipobadilika wakainuka dhidi yake. Vilevile, huko nyuma walimuita adui wa Kizayuni aje dhidi ya ndugu zao hapa nchi, na mauaji yakatokea katika maeneo mengi, na matokeo yakawa kuwa adui wa Kizayuni alipanda mbegu za fitina miongoni mwa wakazi, zikafikia uharibifu na kuleta uhamaji. Sasa kwa nini tunasonga mbele na wito huu wa ndani unaoamsha hisia za kikasumba, fitina, chuki na uharibifu? Tuna tofauti za kisiasa, hili linaeleweka, lakini kwa nini kuchochea migawanyiko ya kimadhehebu, na ni kwa faida ya nani? Na je, uchochezi huu unajenga nchi?! Tuleteeni mpango unaojenga nchi na kuwaunganisha Walebanon kwa misingi ya maslahi ya kitaifa bila kutuonesha chuki.

Sheikh Al-Khatib akiwaelekea Walebanon kutoka madhehebu zote alisisitiza: Wingi wa madhehebu sio tatizo, kwani dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni moja, na wote wanakusanyika katika thamani za kheri. Hakuna sababu ya kuliogopa dhehebu moja au dini nyingine. Hofu ipo katika kutumia dini kama chombo kwa ajili ya mambo hatari, kwa kuwa dini ni ya kuleta ukaribu, si ya kutenganisha.

Makamu wa Rais wa Baraza Kuu la Kiislamu la Kishia, akiuliza: Je, mmewahi kuona katika vitabu vya mbinguni maandishi yanayowazuia watu tofauti kuzungumza na kusikilizana? Akasema: Tunapaswa kukusanyika pamoja kukabiliana na hatari inayotukabili sote. Na iwapo baadhi wanafikiri kwamba kuwaomba wageni ndio wokovu wao, basi tunapaswa kusema: kujitolea na kutegemea wageni kunaleta madhara kwa wote.

Alisisitiza kuwa; baadhi ya wanaozungumza kwa jina la Wakristo, kwa hakika wanawasingizia Wakristo. Wakristo ni ndugu zetu katika imani na ushirikiano. Hatutegemei vibaraka, bali tegemeo letu ni kwa wasomi na wenye uwezo, na wao wanapaswa kutekeleza jukumu lao, si wengine kuwa chini na kufuata madaraka ya kisiasa.

Sheikh Al-Khatib aliendelea: Tatizo letu ni kwamba tunaingia katika vita vya kisiasa vya ndani na hatujifunzi. Nawambia ndugu zangu katika taifa kwamba kudhalilisha sura ya dhehebu la Kishia nchini Lebanon ni njama dhidi ya Lebanon. Tulishika silaha kwa kuwa hakukuwa na serikali, na sisi ndio wenye uaminifu zaidi kwa serikali kuliko wengine wote. Tunataka kuitetea Lebanon na washirika wetu ndani ya Lebanon. Mamlaka ya taifa sio ya Kishia, bali ni mamlaka moja ya kitaifa. Na inapoumizwa sehemu moja, Lebanon yote inaumia.

Akasema: Asidhanie yeyote kwamba mambo yatatengemaa kwa kulivua silaha jeshi la muqawama. Silaha ni kwa ajili ya kuitetea Lebanon. Lebanon ilikaa miaka 60 bila mambo kutengemaa wakati hakuna silaha yoyote. Sababu ya migogoro ya Lebanon sio silaha, bali ni kuwepo kwa adui wa Kizayuni anayekusudia kujenga dola yake kwa gharama ya Syria, Lebanon na eneo lote. Silaha ya Lebanon sio ya Kishia, bali ni ya taifa zima.

Makamu wa Rais wa Baraza Kuu la Kishia akiuliza kuhusu mafanikio ya serikali alisema: Mafanikio ya serikali ni yapi? Je, kusini kume kombolewa, au azimio namba 1701 limetekelezwa? Je, kuna kipengele chochote cha azimio hicho kilichotekelezwa ilhali uvamizi wa adui umeongezeka na ukaliaji umeongezeka baada ya vita, wakati kabla ya hapo ulikuwa ni mita chache tu?

Akaongeza: Je, serikali imetekeleza diplomasia yake? Haina diplomasia yoyote isipokuwa dhidi ya Iran, na inatoa taarifa zinazodaiwa kuwa ni kwa Wairan kwamba wasiingilie mambo yetu ya ndani, ilhali wajumbe kutoka mataifa ya nje wanakuja na kuingilia masuala yetu na kutuamulia. Jukumu la Benki Kuu na serikali limekuwa ni kubana njia kwa muqawama, kuizingira Lebanon na kuidhoofisha. Na hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu kuhusu sarafu zimekuwa kwa lengo la kuwafanya Walebanon wanyenyekee na kwenye utekelezaji wa maamuzi ya mataifa ya kigeni.

Sheikh Al-Khatib alisema: Sisi tunataka mafanikio ya serikali na tuko pamoja nayo, lakini tunataka izingatie maslahi ya Walebanon katika kilimo na mambo mengine, ilhali bidhaa zimejaa kwenye maghala. Siasa ya serikali iko wapi katika jambo hili? Tunataka serikali iwe na siasa wazi kwa manufaa ya Walebanon, si kufanya jitihada tu za kulivua silaha jeshi la muqawama na kutekeleza sera za kigeni. Tunakishika mkono kikosi cha jeshi la Lebanon kinacholinda usalama na kuzuia matatizo ya ndani, na tunampongeza Jenerali Joseph Aoun (Kamanda wa Jeshi) aliyeliagiza jeshi kukabiliana na uvamizi wa adui, na tunaitaka serikali kukabiliana na Israel na kuepuka kufuata maamuzi ya nje.

Akasema: Tatizo letu Lebanon ni tatizo la Uarabu na Uislamu. Hatujaunda utamaduni mmoja Lebanon na kwa sababu hiyo tunaiona migawanyiko hii. Lebanon haikuwa na serikali, hesabu au maandalizi kwa hatua hii, na ndio maana tumefikia hapa. Kuna hatari zinazoitishia nchi ambazo sisi tunaona na wengine hawaoni, bali wengine wanaiona kama fursa ya kumshambulia ndugu yao katika taifa.

Sheikh Al-Khatib akauliza: Nani anawajibika kwa hali hii, na je mmeijenga nchi ya kukabiliana na hatari hizi? Ili kuwe na taifa, tunapaswa kukubaliana juu ya utamaduni mmoja. Kwa hiyo tunatoa wito wa kujenga nchi moja na iliyoungana. Hatutetei sisi pekee yetu dhidi ya adui wa Kizayuni, bali tunailinda Lebanon yote.

Alizungumzia pia maneno ya Rais kuhusu wale wanaokwenda Marekani kuwachafua ndugu zao wa taifa, na kukumbusha jinsi baadhi walivyokuwa wakishirikiana na uwepo wa Syria kiasi kwamba waliwashirikisha viongozi wa Syria katika matatizo yao ya ndani na ya kifamilia.

Makamu wa Rais wa Baraza Kuu la Kiislamu la Kishia akaongeza: Tunatumai kutoka kwa Walebanon na pande zote kwamba watafanya marekebisho ya mwelekeo unaoiongoza Lebanon kuelekea kusalimu amri mbele ya adui wa Kizayuni. Baadhi wanakimbilia silaha, ilhali silaha sio tatizo—tatizo ni adui wa Kizayuni. Tatizo ni mgawanyiko wa kitaifa. Tatizo ni mipango ya ndani inayotumia nguvu za nje kujiimarisha dhidi ya ndani. Tatizo ni katika kujenga taifa, kwa kuwa sote hatuioni Lebanon kwa mtazamo mmoja. Hatukuiandaa Lebanon—jamii, serikali, watu na taasisi—kwa ajili ya vita hii, bali tumeiandaa kwa hali hii ya kushindwa na mgawanyiko wa ndani, hadi adui wa Kizayuni anatulazimisha kile anachotaka.

Sheikh Al-Khatib alisisitiza: Hatutasalimu amri. Tunazingatia uhalisia na maslahi ya kitaifa, na tunawataka Walebanon wote waungane angalau katika kupunguza hasara kwa kukusanyika juu ya msimamo mmoja wa kitaifa utakaouunga mkono msimamo na mantiki ya serikali dhidi ya adui wa Kizayuni, na hivyo kupunguza shinikizo la kiuchumi, kisiasa na kijeshi kwa Lebanon. Hii ndio njia pekee ya kutoka kwenye hali hii ya kusikitisha.

Katika hitimisho lake alisema: Hatuwezi kabisa kulijenga taifa isipokuwa kwa kuanzisha serikali moja ya pamoja yenye msingi wa uraia na kuunda utamaduni mmoja na wa pamoja wa kukabiliana na hatari nzito zilizopo mbele yetu. Hakuna wokovu kwa Lebanon isipokuwa kupitia taifa hili na utamaduni huu. Kwa sababu kukabiliana na changamoto zilizopo kwa hali ya sasa ya mgawanyiko haiwezekani.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha