Jumapili 16 Novemba 2025 - 22:58
Hafla ya kumbukizi ya shahada ya Bibi Fatima Zahra (as) Yafanyika Tehran Irani Huku Mke wa Sheikh Ibrahim Zakzaky Akihutubia

Hawza/ Mke wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, katika hafla ya kumbukumbu ya shahada ya Bibi Fatima Zahra (A.S) iliyofanyika Tehran, huku akisisitiza ulazima wa kutekeleza malengo na misingi ya Bibi Zahra (A.S), alisema: “Shida zote za leo za Umma wa Kiislamu ni tija ya matukio yaliyotokea baada ya kufariki Mtume Mtukufu (saww).”

Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, hafla iliyoandaliwa kwa kuhudhuria kundi la wanafunzi wa Hawza na walimu wa dini kwa mnasaba wa siku za shahada ya Bibi wa ulimwengu, Fatima Zahra (as), ilifanyika katika Chuo Kikuu cha Shahid mjini Tehran. Hafla hii iliandaliwa na kituo cha Al-Basirah Nigeria pamoja na kundi la wanafunzi wanaoongozwa na Sheikh Ibrahim Yakubu Zakzaky.

Shughuli zilianza kwa kisomo cha Aya za Qur’ani Tukufu, kisha zikafuatiwa na kisomo cha Ziyarat Ashura, Dua Tawassul, Ziyarat Bibi Zahra (A.S) na dua nyenginezo. Baadaye, waombolezaji wa misiba ya Ahlul Bayt (A.S) walisoma nauha za maombolezo ya kuhuzunisha.

Katika hafla hii, “Ummush-Shuhadaa” Bi Zainatuddeen Ibrahim, mke wa Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Waislamu wa Kishia Nigeria, alitoa hotuba.

Katika utangulizi wa hotuba yake, Bi Zainab alizungumzia falsafa ya kukumbusha dhulma aliyopata Bibi Zahra (as) na akasisitiza: “Faida ya kukumbuka majonzi haya ni kuiga mfano wake katika kutetea haki ambayo ndiyo iliyosababisha maafa hayo kumshukia.” Akaongeza: “Haitoshi kuonesha huzuni juu ya misiba ya Bibi Zahra (as) lakini kushindwa kusimama kwa ajili ya kulinda njia aliyouawa kwa ajili yake. Maombolezo kama hayo hayana faida.”

Mke wa Sheikh Zakzaky, akibainisha kuwa “hata ikiwa mtu hafiki kwenye majlisi ya maombolezo lakini anasimama kidete na kutetea njia yake, na kupambana na dhulma, thamani ya kazi yake ni kubwa zaidi kuliko yule anayehudhuria majlisi lakini akawa yuko pamoja na madhalimu,” alieleza: “Shida na misukosuko yote ya leo katika Umma wa Kiislamu ni tija ya matukio yaliyofuata baada ya kufariki Mtume Mtukufu (saww). Lau watu wangelifuata wasia wa Mtume wa Rehema, dunia leo isingekuwa imekumbwa na maafa haya yote.”

Akiendelea, alikanusha madai ya baadhi ya watu kuhusu malengo ya kidunia ya Bibi Zahra (as), akisema: “Mwanamke muumini anayemfahamu Mungu na anayejua uzito wa jukumu la uongozi, hawezi kutamani utawala kwa ajili yake au kwa ajili ya mume wake. Kwa hivyo, Bibi Zahra (as) alisimama kutekeleza amri na wasia wa Mtume Mtukufu (saww), sio kwa maslahi ya kidunia.”

Bi Zainatuddeen, akisisitiza ulazima wa kujisalimisha kikamilifu kwenye amri ya Mwenyezi Mungu, alisema: “Iwapo mtu atasalimika kwa asilimia 99 lakini kwa makusudi akaacha asilimia 1, basi amali yake haina thamani.”

Mke wa Sheikh Zakzaky katika hitimisho alisema: “Dini hii nchini Nigeria itadumu na kusimama imara,” na akasisitiza: “Hakuna nguvu yoyote — si Marekani, si Israel wala Japan — inayoweza kuizuia.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha