Jumanne 4 Novemba 2025 - 23:22
Imamu Mahdi katika Vyanzo vya Ahlus-Sunna

Hawzah/ Kwa kupitia kwa muhtasari vitabu vya riwaya vya Ahlus-Sunna, inadhihirika wazi kuwa suala la Imamu Mahdi (a.s.) limetajwa kwa wingi katika vyanzo vyao. Mbali na hadithi nyingi zilizomo katika vyanzo vya Kisunni, pia kuna vitabu maalumu vilivyoandikwa na wanazuoni wao kuhusu Imam Mahdi (a.s.), jambo linaloonesha hadhi ya juu ya dhana ya Mahdiyyah katika mtazamo wao.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, mfululizo wa Tafiti za Mahdiyyah chini ya anuani isemayi “Kuielekea Jamii Bora”, zimeandaliwa kwa lengo la kusambaza mafundisho na maarifa yanayohusiana na Imam Mahdi (a.t.f.s.), na zinawasilishwa kwa wasomi na wapenda elimu wote.

Imamu wa Mahdi katika Vyanzo vya Ahlus-Sunna

Itikadi ya Mahdiyyah na wazo la kuonekana kwa Imam Mahdi (a.t.f.s.) — kinyume na dhana ya baadhi ya watu — si jambo lililohusishwa na Shia pekee, bali ni sehemu muhimu ya imani ya Kiislamu iliyojengeka katika madhehebu yote ya Kiislamu, kwa mujibu wa bishara za Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w).

Katika nyanja za itikadi ya Kiislamu, ni vigumu kupata jambo jingine lililopewa umuhimu mkubwa kama hili. Hadithi zinazomhusu Imam Mahdi (a.t.f.s.) zimekuja katika vitabu vingi mashuhuri vya Ahlus-Sunna. Katika vitabu hivyo, yamezungumzwa mambo kama sifa na maisha ya Imam Mahdi (a.t.f.s.), alama za kudhihiri kwake, eneo atakapoonekana, kiapo cha utiifu (bay‘ah), idadi ya wafuasi wake, na masuala mengineyo yanayohusiana naye.

Waislamu, katika historia yote, wamekubaliana kwamba katika zama za mwisho atadhihiri mwanaume mmoja anaetokana na Ahlul-Bayt (a.s.) ambaye ataeneza uadilifu duniani. Waislamu watamfuata, naye atatawala nchi za Kiislamu. Jina lake ni “Al-Mahdi.”
(Abdurrahman Ibn Khaldun, “Muqaddimat Al-‘Ibar”, uk. 245)

Hata hivyo, kuna wachache waliokataa kukubali dhana ya Mahdiyyah kwa ujumla, na kwa hoja dhaifu wakaitupilia mbali wakidai kuwa ni fikra ya Kishia. Lakini kwa kuchunguza vitabu vya riwaya vya Ahlus-Sunna, inadhihirika wazi kuwa suala la Mahdiyyah limezungumziwa kwa wingi humo. Mbali na hadithi nyingi zilizotawanyika, wanazuoni wao wameandika vitabu maalumu vya hadithi vinavyomhusu Imam Mahdi (a.s.), jambo linalothibitisha nafasi ya heshima kubwa ya Mahdiyyah katika mtazamo wa Kisunni.

Vitabu vya Kisunni Kuhusu Mahdiyyah

Vyanzo vya Kisunni kuhusu mjadala wa Mahdiyyah vinaweza kugawanywa katika makundi mawili makuu:

1. Vitabu vya Jumla:

Hivi ni vitabu ambavyo vimegusia suala la Mahdiyyah sambamba na masuala mengine mbalimbali. Miongoni mwa mambo yaliyotajwa ndani yake ni: Hadithi zinazothibitisha kuwa Imam Mahdi (a.s.) atatokana na kizazi cha Mtume Muhammad (s.a.w.w), na kwamba ni katika kizazi cha Imam Ali (a.s.) na Bibi Fatima (a.s.),

Sifa zake, mwenendo wake, namna atakavyodhihiri, dola yake, n.k. Baadhi ya vitabu ambavyo hadithi nyingi kuhusiana na Imam Mahdi (a.s.) zimekusanywa ndani yake ni:

1. al-Muṣannaf – cha Abdul-Razzāq

Kitabu hiki kimeandikwa na Abuu Bakr ‘Abdul-Razzāq bin Hammām as-San‘ānī (aliyefariki mwaka 211 H). Ndani yake ametenga mlango maalumu unaoitwa “Bāb al-Mahdī”, na amesimulia zaidi ya hadithi kumi kuhusiana na Imam Mahdi. Baada ya mlango huo, ametenga mlango mwingine uitwao “Bāb Ashrāṭ as-Sā‘ah” (alama za Qiyama), ambapo amegusia mada zingine. Hiki ndicho kitabu cha kwanza cha Kisunni kilichokusanya hadithi za Imam Mahdi (a.t.f.s.) kwa mpangilio maalumu.

2. Kitabu al-Fitan

Kimeandikwa na Hāfiz Abu ‘Abdillāh Nu‘aym bin Hammād al-Marwazī (aliyefariki mwaka 229 H). Ndani yake, mwandishi amepokea hadithi nyingi kuhusiana na Imam Mahdi (a.t.f.s.), sifa zake, tabia zake na matukio ya zama zake. Mwandishi ametenga sehemu kumi (10) kwa anuani tofauti zinavyohusiana na fitina za zama za mwisho. Sehemu nne za mwanzo zinahusu matukio na fitina zilizotajwa katika hadithi, na kuanzia sehemu ya tano kuendelea ndimo zilimo hadithi nyingi zaidi kuhusiana na Imam Mahdi (a.t.f.s.).

3. al-Muṣannaf fī al-Aḥādīth wa al-Āthār

Kimeandikwa na Hāfiz ‘Abdullāh bin Muhammad bin Abī Shaybah al-Kūfī (aliyefariki mwaka 235 H). Ndani ya sura ya 37, mwandishi ametenga sehemu maalumu iitwayo “al-Fitan”. Humo amesimulia hadithi zinazomhusu Imam Mahdi (a.t.f.s.) na masuala yanayohusiana naye. Baadhi ya hadithi zinamtaja Imam Mahdi kwa jina lake kamili.

Miongoni mwa mambo yaliyotajwa katika hadithi hizo ni: Sifa za nasaba na kimaadili za Imam Mahdi (a.t.f.s.), Muda wa utawala wake na umri wake, hali ya dunia kabla ya kudhihiri kwake, alama za kudhihiri, na sifa za kipindi cha utawala wake baada ya kudhihiri.

4- Musnad Ahmad

Ahmad bin Hanbal Abu ‘Abdillāh ash-Shaybānī (aliyefariki mwaka 241 Hijria) ni mmoja wa viongozi wakuu wanne wa madhehebu ya Kisunni. Katika kitabu chake mashuhuri “Musnad Ahmad”, amesimulia hadithi nyingi na tofauti zinazomhusu Imam Mahdi (a.t.f.s.). Hadithi hizo, kwa pamoja na zile zilizomo katika kitabu “al-Bayān fī Akhbār Ṣāḥib az-Zamān”, zimekusanywa na kuchapishwa kwa jina la “Aḥādīth al-Mahdī min Musnad Aḥmad bin Hanbal”. Miongoni mwa vitabu vya mwanzo kabisa vya hadithi, Musnad Ahmad ndicho kinachobeba idadi kubwa zaidi ya hadithi kuhusu Imam Mahdi (a.t.f.s.).

5- Sunan Ibn Mājah

Muhammad bin Yazīd Abu ‘Abdillāh al-Qazwīnī (aliyefariki mwaka 275 H) alikuwa mtaalamu na msimuliaji mashuhuri wa hadithi kwa Ahlus-Sunna, na kitabu chake “Sunan Ibn Mājah” ni miongoni mwa vitabu sita sahihi (as-Siḥāḥ as-Sitta). Ndani ya sehemu ya al-Fitan, ameitenga sura maalumu yenye anuani isenayi “Bāb Khurūj al-Mahdī” (Kudhihiri kwa Mahdi), akasimulia humo hadithi kadhaa zinazomhusu Imam Mahdi (a.t.f.s.).

6- Sunan Abī Dāwūd

Kitabu hiki nacho ni miongoni mwa as-Siḥāḥ as-Sitta za Ahlus-Sunna, kilichoandikwa na Sulaimān bin al-Ash‘ath Abu Dāwūd As-Sijistānī (aliyefariki mwaka 275 H). Ndani ya mkusanyiko huo, ameitenga sehemu huru yenye anuani “Kitāb al-Mahdī” (Kitabu cha Mahdi). Hadithi zilizomo katika Sunan Abī Dāwūd zinachukuliwa kuwa miongoni mwa vyanzo muhimu kabisa kuhusiana na dhana ya Mahdiyyah katika mtazamo wa Kisunni.

7- Al-Jāmiu As-Sahih

Hiki ni miongoni mwa vitabu sita sahihi vya Ahlus-Sunna vilivyoandikwa na Muhammad bin ‘Īsā Abu ‘Īsā at-Tirmidhī as-Sulamī (aliyefariki mwaka 279 H). Ingawa hadithi kuhusu Imam Mahdi (a.t.f.s.) si nyingi ndani ya mkusanyiko huu, lakini kwa kuzingatia uaminifu wa misururu ya wapokezi wake (asānīd), hadithi chache hizo ni muhimu sana na zinatoa taarifa kamili kuhusiana na Imam Mahdi (a.t.f.s.).

8- Al-Mustadrak ‘alā aṣ-Ṣaḥīḥayn

Kitabu hiki kimeandikwa na Muhammad bin ‘Abdillāh Abu ‘Abdillāh al-Ḥākim an-Nayshābūrī (aliyefariki mwaka 405 H). Hadithi zinazomhusu Imam Mahdi (a.t.f.s.) amezitaja katika sura maalumu ndani ya “al-Fitan wal-Malāḥim” na pia katika sehemu nyinginezo kwa mtawanyiko.

Katika hadithi hizo, mwandishi amezungumzia mambo mengi yanayomhusu Imam Mahdi (a.t.f.s.), yakiwemo: Nasaba yake, sifa za kimaumbile, hali ya dunia kabla ya kudhihiri, asili ya kudhihiri kwake, na masuala mbalimbali yanayohusiana naye.

9- Kanz al-‘Ummāl fī Sunan al-Aqwāl wal-Af‘āl

Alā’uddīn ‘Alī al-Muttaqī bin Ḥisām ad-Dīn al-Hindī (aliyefariki mwaka 975 H) ni miongoni mwa wanazuoni maarufu wa hadithi wa Kisunni aliyejipatia sifa kwa kuandika kitabu kikubwa “Kanz al-‘Ummāl”, mojawapo ya mikusanyiko mashuhuri zaidi ya hadithi za Kisunni.

Mwandishi huyu, ambaye pia aliandika kitabu kingine maalumu kumhusu Imam Mahdi (a.t.f.s.) kiitwacho “al-Burhān fī ‘Alāmāt al-Mahdī al-Ākhir az-Zamān”, ndani ya Kanz al-‘Ummāl ameweka mlango maalumu uitwao “Khurūj al-Mahdī” (Kudhihiri kwa Mahdi), na humo amekusanya makumi ya hadithi kutoka katika vyanzo mbalimbali.

2. Vitabu Maalumu vya Hadithi Kuhusiana na Imam Mahdi (a.t.f.s.)

Wanazuoni wa Ahlus-Sunna — sawa na wanazuoni wa Kishia — hawakuridhika tu na kuwepo kwa hadithi za Mahdiyyah katika vitabu vya jumla, bali waliandika vitabu mahsusi vilivyomuhusu Imam Mahdi (a.t.f.s.).
Baadhi ya kazi hizo adhimu ni kama zifuatazo:

1. Arba‘ūn Ḥadīth (Hadithi Arobaini)

Kitabu hiki kiliandikwa na Abu Nu‘aym Al-Iṣfahānī (aliyefariki mwaka 420 H), mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Kisunni aliyekuwa na kazi nyingi za kielimu. Ingawa kitabu Arba‘ūn Ḥadīth hakipatikani tena leo, ‘Allāmah al-Arbalī amekinukuu ndani ya kitabu chake Kashf al-Ghummah fī Ma‘rifat al-A’immah.

Kabla ya kunukuu hadithi hizo, al-Arbalī aliandika: "Namenukuu hadithi arobaini ambazo Abu Nu‘aym al-Iṣfahānī alizikusanya kuhusiana na Imam Mahdi (a.t.f.s.), kwa usahihi kamili jinsi alivyopanga yeye mwenyewe."

2. Al-Bayān fī Akhbār Ṣāḥib az-Zamān (as)

Kitabu hiki kiliandikwa na Abu ‘Abdillāh Muhammad al-Ganjī ash-Shāfi‘ī (aliyefariki mwaka 658 H). Ndani yake, amekusanya hadithi kuhusu Imam Mahdi (a.t.f.s.) pamoja na sifa zake maalumu kwa mpangilio mzuri na katika milango iliyo na utaratibu kamili.

Katika utangulizi wa kitabu chake, mwandishi alieleza wazi kuwa lengo lake ni kukanusha madai kwamba dhana ya Mahdiyyah ni ya Kishia, na kuthibitisha kuwa ni itikadi ya Kiislamu. Akasema wazi kwamba amekusanya tu hadithi zilizopokelewa kwa njia za Ahlus-Sunna, akiepuka kabisa kutumia riwaya za Kishia. Jumla ya hadithi alizokusanya ni 70, akazigawa katika milango 25, na hata amegusia baadhi ya mambo madogo madogo yanayomhusu Imam Mahdi (a.s).

Jambo la kuvutia ni kwamba, licha ya wanazuoni wengi wa Kisunni kukataa kuzaliwa kwa Imam Mahdi (a.t.f.s.), mlango wa mwisho wa kitabu chake ameuita: 


“في الدلالة على جواز بقاء المهدي حيا” 

“Ushahidi juu ya uwezekano wa Imam Mahdi kubaki hai.”

Kwa msingi huu, mwandishi huyu si tu kwamba alikubali kuzaliwa kwa Imam Mahdi (a.t.f.s.), bali pia alikataa hoja yoyote inayodai kutowezekana kwa uhai wa muda mrefu wa Imam huyo.

3- ‘Iqd ad-Durar fī Akhbār al-Muntaẓar

Kitabu hiki kimeandikwa na Yūsuf bin Yaḥyā bin ‘Alī bin ‘Abd al-‘Azīz al-Maqdisī ash-Shāfi‘ī (aliyefariki mwaka 658 H). ‘Iqd ad-Durar ni moja ya vyanzo vyenye upeo mpana na kamilifu sana, kiasi kwamba kimekuwa rejea muhimu kwa vitabu vingi vilivyokuja baadaye.

Mwandishi wa kitabu "al-Bayān fī Akhbār Ṣāḥib az-Zamān", katika utangulizi wake anaeleza sababu ya kuandika kitabu hiki kwa maneno haya: “Ufisadi wa zama, matatizo na misukosuki ya watu, pamoja na kukata tamaa kwao kuhusu kurekebishwa kwa hali ya mambo, na chuki zilizopo baina yao, si mambo yatakayodumu hadi Siku ya Kiyama. Kuondoka kwa matatizo hayo kutatimia kwa kudhihiri na kutoka kwa al-Mahdi. ... Baadhi ya watu wamekanusha jambo hili kabisa, na wengine hudhani kuwa hakuna Mahdi yeyote isipokuwa Isa (Yesu).”

Mwandishi anapinga kwa upana mitazamo yote miwili hii, akithibitisha kwa hoja thabiti kwamba mawazo hayo hayawezi kukubalika. Kisha anaanza kukusanya hadithi zinazomhusu Imam Mahdi (a.t.f.s.) bila ya kutaja misururu ya wapokezi (isnād), lakini akibainisha vyanzo vya msingi ambamo hadithi hizo zimepokelewa. Katika hadithi nyingi, hakutoa maoni yoyote kuhusu udhaifu au usahihi wake; bali aliridhika tu kwa kuziorodhesha. Baada ya utangulizi wake wenye thamani, mwandishi amepanga mjadala wa Mahdiyyah katika sura kumi na mbili zilizowekwa kwa mpangilio makini.

4- Al-‘Arf al-Wardī fī al-Akhbār al-Mahdī (‘alayhi-s-salām)

Kitabu hiki kimeandikwa na Jalāluddīn ‘Abd ar-Raḥmān bin Abī Bakr as-Suyūṭī (aliyefariki mwaka 911 H). Ndani yake, amekusanya hadithi kuhusiana na Imam Mahdi (‘a.s.) kwa upana na kwa maelezo ya kina.

Kitabu hiki kimejumuishwa ndani ya mkusanyiko wa risala kumi (10) uitwao “ar-Rasā’il al-‘Ashr”, ambacho kwa pamoja kimechapishwa ndani ya kazi kubwa ya Suyūtī inayojulikana kama “al-Ḥāwī lil-Fatāwā.”

Katika utangulizi wa risala hii, Suyūṭī anaandika: “Hii ni sehemu ambayo nimekusanya ndani yake hadithi na athar kuhusiana na Imam Mahdi. Nimefupisha hadithi arobaini ambazo al-Hāfiz Abu Nu‘aym alizitaja, na nimeongeza zile ambazo yeye hakuzileta, kisha nikaziashiria kwa herufi (ك) kama alama yangu.”

5- Al-Burhān fī ‘Alāmāt Mahdī Ākhir az-Zamān

Kitabu hiki ni miongoni mwa vitabu vya kina zaidi vya hadithi kuhusu Imam Mahdi (a.t.f.s.), kikiwa na zaidi ya hadithi 270. Kimeandikwa na ‘Alā’uddīn ‘Alī bin Ḥisām ad-Dīn, maarufu kwa jina la al-Muttaqī al-Hindī (aliyefariki mwaka 975 H) — ambaye pia ndiye mwandishi wa Kanz al-‘Ummāl. Kitabu hiki kinaeleza kwa kina alama na matukio yatakayomtangulia Imam Mahdi, sifa zake, na masharti ya kudhihiri kwake, kwa msingi wa hadithi nyingi kutoka vyanzo vya Kisunni.

Tafiti hizi zinaendelea...

Imenukuliwa kutoka katika kitabu kiitwacho “Darsnāmeh-ye Mahdaviyyat” kilichoandikwa na Khudā-Murād Salīmiyān, huku kikifanyiwa marekebisho kiasi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha