Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Mtukufu Ayatullah Javadi Amoli katika maandiko yake yenye maudhui isemayo “Hijabu ni Haki ya Mwenyezi Mungu” amejibu hoja iliyoibuliwa katika uwanja huo na kusema:
“Hoja inayojitokeza katika fikra za baadhi ya watu ni kudhani kwamba hijabu ni kizuizi na kifungo ambacho familia au mume wamemwekea mwanamke, na kwa hivyo huiona hijabu kama ishara ya udhaifu na mipaka kwa mwanamke.”
Akaendelea kueleza kuwa: “Suluhisho la hoja hii, na ufafanuzi wa hijabu katika mtazamo wa Qur’ani Tukufu, ni kwamba mwanamke anatakiwa kufahamu vyema kuwa hijabu yake si jambo linalomhusu yeye binafsi hadi aseme ‘nimeacha haki yangu’; hijabu ya mwanamke si ya mwanaume hadi aseme ‘nimeridhika’; wala si ya familia hadi wao watoe ridhaa — hijabu ya mwanamke ni haki ya Mwenyezi Mungu.”
Ayatullah Javadi Amoli ameongeza kuwa: “Heshima ya mwanamke si mali yake binafsi, wala ya mume wake, wala ya kaka au watoto wake. Hata wote wakiridhia, Qur’ani haitaridhika. Kwa sababu heshima na hadhi ya mwanamke ni katika muktadha wa Haqqullah — haki ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Mtukufu amemuumba mwanamke akiwa na hazina ya huruma na hisia ili awe mwalimu wa upole na mjumbe wa mapenzi. Ikiwa jamii itaacha somo hili la huruma na kufuata matamanio ya kijinsia, watakumbwa na maovu yale yale yaliyodhihiri katika ulimwengu wa Magharibi.”
Kisha akabainisha kwamba: “Kwa hiyo, hakuna yeyote mwenye haki ya kusema, ‘nimeridhia kutovaa na hijabu.’ Kwa kuwa Qur’ani Tukufu inasema kwamba hata kama watu wote wameridhia uovu fulani, bado mipaka ya Mwenyezi Mungu lazima itekelezwe, inadhihirika wazi kwamba usafi na utukufu wa mwanamke ni haki ya Mwenyezi Mungu.
Kwa asili yake, wanachama wote wa familia, wanajamii, na hasa mwanamke mwenyewe, ni waaminifu wa amana ya Mwenyezi Mungu. Mwanamke katika mtazamo wa Qur’ani ni mwaminifu wa haki ya Mwenyezi Mungu, yaani Mwenyezi Mungu Mtukufu amempa hadhi na heshima hii kama haki Yake Mwenyewe, na amemwambia: ‘Hii ni haki Yangu, ihifadhi kama amana.’”
Chanzo: Kitabu “Mwanamke katika Kioo cha Utukufu na Uzuri” (Zan dar Ayine-ye Jalal va Jamal), ukurasa wa 437.
Maoni yako