Kwa mujibu wa Idara ya Habari za Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, ujumbe wa maulamaa wakubwa wa Kisunni wa Nigeria, ukiongozwa na Ustadh Ibrahim Maqari, Imamu na khatibu mkuu wa Msikiti wa Kitaifa wa Abuja, ambaye pia ni mfuasi wa tarika ya Tijaniyya, siku ya Jumapili tarehe 2 November walitembelea nyumbani kwa Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Waislamu wa Kishia wa Nigeria, mjini Abuja. Ziara hiyo ililenga kuimarisha mshikamano na ushirikiano kati ya maulamaa wa Kiislamu na wafuasi wa madhehebu mbalimbali nchini humo.
Miongoni mwa wajumbe wa ujumbe huo alikuwemo Sheikh Nur Khalid (Imamu wa zamani wa Msikiti wa Bunge la Seneti), Sheikh Sidi Tahir Sokoto (miongoni mwa wanazuoni wakuu wa eneo la Sokoto), na Sheikh Thani Isa (Imamu wa Msikiti wa Wafa Road katika jimbo la Kaduna).
Sheikh Ibrahim Zakzaky aliwapokea wageni hao kwa uso wa furaha na mapokezi mazuri, akawashukuru kwa juhudi zao katika kuimarisha umoja wa Kiislamu, na akawaombea mafanikio katika juhudi zao hizi za kheri. Katika hotuba yake yenye maelezo ya kina na maarifa, kiongozi huyo wa Kishia alisisitiza juu ya umuhimu wa umoja na nafasi yake isiyoweza kubadilishwa katika kuleta utulivu na uimara wa Umma wa Kiislamu na jamii ya kibinadamu kwa ujumla.
Alibainisha kuwa umoja ni jambo la lazima na lisiloweza kupuuzwa, akisema kuwa tofauti za mitazamo na tafsiri za kidini hazipaswi kuwa kikwazo kwa mashirikiano na maelewano baina ya Waislamu.
Sheikh Zakzaky pia alisisitiza kuwa haja ya umoja haipaswi kuishia ndani ya jamii ya Kiislamu pekee, bali inapaswa kuvuka mipaka ya kidini na kijamii, akibainisha kwamba maendeleo ya kitaifa na maboresho ya mahusiano ya kijamii hayawezi kupatikana bila umoja wa mioyo na ushirikiano wa raia wote, bila kujali dini au madhehebu yao.
Mwisho wa kikao hicho, Sheikh Zakzaky aliwazawadia kila mmoja kati ya maulamaa hao nakala ya Qur’ani Tukufu na kitabu cha Mafatih al-Jinan. Wageni hao walionesha furaha yao kubwa kwa ziara hiyo na, baada ya kuagana kwa maelewano na mapenzi ya undugu, walirejea katika miji yao wakiwa wamejawa na matumaini ya kuimarisha zaidi umoja wa Kiislamu.



Maoni yako