Alhamisi 6 Novemba 2025 - 00:25
Kikao Kilichokuwa na Maudhui Isemayo “Ujumbe wa Kibinadamu” Chafanyika Nchini India

Hawza/ Kikao kilichopewa jina la “Ujumbe wa Kibinadamu” kimefanyika katika mji wa Kolkata, India, kwa ushiriki wa kundi la wanazuoni na wanaharakati wa kiutamaduni.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, kikao cha kielimu na kiroho cha “Ujumbe wa Kibinadamu” kiliandaliwa na Jumuiya ya Ujumbe wa Kibinadamu ya India nzima, na kilihudhuriwa na wanazuoni pamoja na wanaharakati wa kidini katika mji wa Kolkata. Lengo la kikao hiki lilikuwa kueneza thamani za kibinadamu, kuimarisha roho ya mshikamano, na kubainisha umuhimu wa maadili na umoja katika jamii ya wanadamu.

Msisitizo juu ya udugu na mshikamano katika jamii ya kibinadamu

Mwanzoni mwa hafla hiyo, Dkt. Sabah Ismail Nadwi, Mkurugenzi wa Shule ya Jibril, India, alibainisha kuwa: “Ujumbe wa ubinadamu ni daraja imara la kuimarisha misingi ya udugu, huruma na kuheshimiana miongoni mwa wanadamu; hizi ni thamani ambazo dunia ya leo inazihitaji kuliko wakati mwingine wowote.” Aidha, alizisifu huduma na shughuli za taasisi hiyo, akizitaja kuwa ni hatua mashuhuri katika kuijenga jamii inayotegemea maelewano, ushirikiano na mafungamano ya moyo.

“Ujumbe wa Ubinadamu”; kielelezo cha mafundisho ya Qur’ani na Sunna

Katika sehemu iliyoendelea ya hafla hiyo, Maulavi Khurshid Jamil Nadwi, mtaalamu wa masuala ya kidini wa Kisunni, huku akiwashukuru waandaaji wa kikao hicho na alisisitiza malengo ya harakati hiyo ya kiroho, alisema: “Ujumbe wa ubinadamu umetokana na mafundisho halisi ya Qur’ani na Sunna; ni ujumbe unaolenga kuunganisha mioyo, kuondoa chuki na kueneza rehema na huruma katika jamii.”

Aliongeza kuwa kuendeleza mazungumzo, upendo na roho ya maelewano ya kibinadamu ni miongoni mwa njia kuu za kuunda mazingira yenye afya, kiroho na ufanisi ndani ya jamii.

Katika sehemu ya mwisho ya kikao hicho, Maulavi Khurshid Alam Nadwi, Mkuu wa Jumuiya ya Ujumbe wa Ubinadamu, alisimulia kumbukumbu na mifano halisi ya shughuli za harakati hiyo akisema:

“Katika njia ya kuhudumia ubinadamu tumeona jinsi mioyo ambayo hapo awali ilikuwa migumu na isiyo na hisia, ilivyokuwa laini na yenye mapenzi baada ya kusikia ujumbe wa upendo, udugu na upendo wa kibinadamu; na kwa uaminifu kabisa wameitikia wito huu.”

Kikao hiki kilihitimishwa kwa ushiriki wa wanazuoni mashuhuri, wanaharakati wa kiutamaduni na sura za kidini za mji huo. Washiriki walikitathmini kikao hicho kuwa ni hatua yenye thamani kubwa katika kueneza utamaduni wa upendo, umoja na uadilifu wa kiroho.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha