Ijumaa 7 Novemba 2025 - 10:56
Mchanganyiko wa Damu na Uadilifu: Siku Ambayo Deir Yassin na Bogotá Zilivyoteketezwa na Moto

Hawza/ Tarehe 9 Aprili 1948, mabara mawili yenye lugha tofauti, lakini yenye maumivu yanayofanana, yalitetemeka. Huko Palestina, kijiji cha Deir Yassin kiliteketezwa kwa moto wa Wazayuni, na huko Kolombia, risasi ilinyamazisha sauti ya haki ya Jorge Eliécer Gaitán.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, tarehe 9 Aprili 1948 ni siku ambayo historia katika pande mbili za dunia — Palestina na Kolombia — ilichuruzika damu. Wakati risasi jijini Bogotá ilipomuua Jorge Eliécer Gaitán, mwanasiasa maarufu na msemaji wa maskini, huko Deir Yassin kandokando ya Quds (Yerusalemu), makundi ya kijeshi ya Kizayuni Irgun na Lehi yalivamia wanavijiji wasio na silaha na kufanya mauaji yaliyokuja kujulikana baadaye kama “Nakba” (Janga Kuu).

Huko Deir Yassin, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Msalaba Mwekundu, washambuliaji hawakutofautisha kati ya wanaume na wanawake, watoto na wazee; walivamia nyumba zote. Mashahidi waliripoti matukio ya ubakaji, mauaji na kuzika miili kwenye visima. Mwanahistoria Muisraeli Ilan Pappé alieleza kuwa tukio hilo halikuwa ajali ya kijeshi, bali lilikuwa sehemu ya mpango wa “Usafishaji wa kikabila” uliolenga kuwaondoa Wapalestina katika ardhi yao. Kuanzia siku hiyo, safari ya uhamaji na mapambano ilianza — na kumbukumbu ya maumivu hayo bado haijawahi kufutika.

Wakati huohuo, katika upande mwingine wa dunia, mauaji ya Gaitán katika mitaa ya Bogotá yalikuwa kama cheche iliyolipua ghala la hasira za watu. Ghasia kubwa zilizoitwa “Bogotazo” ziliukumba mji mzima; magari ya tramu yalichomwa moto, na kuta za majengo zikajaa kauli za wananchi wenye ghadhabu. Mwandishi wa habari wa Kolombia Eduardo Zalamea aliandika kuhusu siku hiyo akisema: “Mji uligeuka kuwa kama tundu la volkano lililokuwa limeficha hasira za karne nyingi; haukuwa na kiongozi, wala mpango — bali ni hasira tu.”

Lakini majibu ya wenye mamlaka katika nchi zote mbili yalikuwa sawa: ukatili na ukandamizaji. Kutoka siku hiyo huko Kolombia, ulizaliwa kipindi kirefu cha ukatili wa kisiasa. Tume ya Ukweli ya nchi hiyo katika ripoti yake ya mwaka 2022 iliandika:
“Kifo cha Gaitán kwa Kolombia kilikuwa sawa na Deir Yassin kwa Palestina — ni wakati ambapo watu walitambua kuwa mamlaka inapohofia haki, huua lugha ya mazungumzo.”

Kadiri miaka ilivyopita, bado kuna muungano usioonekana kati ya Quds na Bogotá. Sehem zote mbili, nguvu za kisiasa zilijaribu kuwatenganisha watu na historia yao, lakini kumbukumbu zao zilibaki hai. Mwanafalsafa wa Kipalestina Edward Said aliita Deir Yassin “dhambi ya kwanza ya taifa lililojengwa juu ya kusahaulika kwa wengine,” na mwanahistoria wa Kolombia Herbert Braun akaandika:
“Bogotazo ilikuwa kilio cha mwisho cha imani kwa neno, na mwanzo wa imani katika moto.”

Leo, mahali palipokuwa kijiji cha Deir Yassin kumejengwa kitongoji cha Kiyahudi cha Israeli, na eneo alikouawa Gaitán limegeuzwa kuwa jumba la makumbusho tulivu. Lakini chini ya mawe na saruji za maeneo yote mawili, bado kuna sauti inayonong’ona: “Uadilifu haufi — hujificha tu ardhini.”

Kila mwaka, tarehe 9 Aprili, Wapalestina huadhimisha kumbukumbu ya Nakba, na Wacolombia huenzi Siku ya Waathirika; mataifa mawili, lugha mbili, lakini kumbukumbu moja ya mateso na mapambano.

Miaka sabini na saba imepita, lakini miale ya siku ile bado haijazimika; kutoka Ghaza hadi Bogotá, historia bado inauliza: “Je, inawezekana kuuhuisha ubinadamu kutoka kwenye majivu ya Haki?”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha