Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran, asubuhi ya leo, katika mnasaba wa siku ya 13 Aban — “Siku ya wanafunzi na Siku ya Kitaifa ya Mapambano dhidi ya Ubeberu wa Kimataifa” — alipokutana na maelfu ya wanafunzi wa shule na wa vyuo vikuu pamoja na familia kadhaa za mashahidi wa vita vya siku 12, aliitaja kumbukumbu ya kuchukuliwa kwa ubalozi wa Marekani, uliokuwa kituo cha njama na mipango dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu mnamo tarehe 13 Aban 1358 (Novemba 4, 1979), kuwa ni “siku ya fahari na ushindi” na siku ya “kufichuliwa kwa utambulisho wa kweli wa serikali ya kimabavu ya Marekani.”
Kiongozi huyo, alisisitiza umuhimu wa kuhifadhi kumbukumbu ya 13 Aban katika historia ya taifa, na kwa kueleza historia ya uadui wa Marekani dhidi ya watu wa Iran, ambao ulianza tangu mapinduzi ya kijeshi ya 28 Mordad 1332 (1953) na unaendelea hadi leo, alisema: “Tofauti kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Marekani ni tofauti ya kimsingi na ni mgongano wa maslahi kati ya mikondo miwili – Marekani na Jamhuri ya Kiislamu – na ni tu ikiwa Marekani itakata kuunga mkono utawala wa kizayuni ulio laaniwa, kuondoa kambi zake za kijeshi kutoka eneo hili na kuacha kuingilia mambo yake, ndipo ombi lolote la ushirikiano nalo litaweza kuzingatiwa katika siku zijazo.”
Kiongozi wa Mapinduzi pia alisisitiza: “Suluhisho la matatizo mengi na kinga ya kweli kwa nchi ni kwa njia ya kuwa na nguvu – ya kiutawala, kielimu, kijeshi, na motisha. Serikali inapaswa kutekeleza majukumu yake kwa uthabiti na nguvu katika maeneo inayohusiana nayo.”
Ayatollah Khamenei, katika mkutano huu, alieleza historia ya uadui wa Marekani dhidi ya taifa la Iran na maelezo ya tukio muhimu la kihistoria la kuchukuliwa kwa lango la ujasusi (ubalozi wa Marekani) tarehe 13 Aban 1358, akasema: “Kuchukuliwa kwa ubalozi wa Marekani na vijana wa Iran kunaweza kuchunguzwa kutoka nyanja mbili — ya kihistoria na ya kitambulisho.”
Kutoka mtazamo wa kihistoria, alitaja tarehe 13 Aban 1358 na hatua ya kishujaa ya wanafunzi waliouteka ubalozi wa Marekani kuwa ni siku ya fahari na ushindi wa taifa la Iran, akisisitiza: “Katika historia ya Iran, zipo siku za ushindi na pia siku za udhaifu na anguko; zote hizi zinapaswa kuhifadhiwa katika kumbukumbu ya taifa.”
Ayatollah Khamenei alikumbushia mifano ya siku zenye fahari kama vile kughairiwa mkataba wa kikoloni wa tumbaku na Mirza Shirazi, au kubatilishwa kwa mkataba wa Vosough al-Dowleh na ushindi dhidi ya Waingereza kupitia jitihada za marehemu Ayatollah Modarres na wenzake, akawasihi wanafunzi, wanafunzi wa vyuo vikuu, na wapenzi wa vitabu kusoma na kujadili matukio haya. Aliongeza kuwa sambamba na kuhifadhi matukio ya kupendeza, “lazima tuwe waangalifu tusisahau matukio machungu kama mapinduzi ya Kiingereza ya mwaka 1299 (1921) yaliyoletwa na Reza Khan, na kisha kupanda kwake kwenye kiti cha ufalme, yaliyosababisha maafa, dhulma, udikteta usio na kifani na utawala wa wageni nchini.”
Alisisitiza kuwa ni lazima tukio la tarehe 13 Aban 1358 na kuchukuliwa kwa ubalozi wa Marekani lihifadhiwe katika historia na kumbukumbu ya taifa, na watu waelimishwe kuhusu umuhimu wake.
Kuhusiana na utambulisho wa tukio hili kuu, alisema: “Kuchukuliwa kwa ubalozi wa Marekani kulifahamisha wazi dhamira yaa kweli ya serikali ya Marekani na vilevile utambulisho halisi na asili ya Mapinduzi ya Kiislamu.”
Kiongozi wa Mapinduzi, akitaja asili ya neno “Istikbār” (ubeberu) katika Qur’ani, alilielezea kuwa linamaanisha kujiona bora kuliko wengine, akasema:
“Wakati mwingine mtu au serikali hujiona bora lakini haivamii maslahi ya wengine — hali hiyo haiibui uadui. Lakini wakati mwingine, kama vile Uingereza katika baadhi ya nyakati au Marekani katika zama hizi, inajipa haki ya kuingilia maslahi muhimu ya mataifa mengine, kuamua mambo yao, kuanzisha kambi za kijeshi katika nchi zisizo na serikali imara au watu wenye uelewa, au kupora mafuta na rasilimali za mataifa — huo ndio ubeberu tunaoupinga na dhidi yake tunapaza sauti zetu.”
Akiendelea kuelezea historia ya uadui wa Marekani dhidi ya taifa la Iran, alisema: “Baada ya Mapinduzi ya Kikatiba, kwa takribani miaka 40, Iran ilikuwa aidha katika hali ya machafuko na ghasia, au chini ya uvamizi wa mataifa ya kigeni, au chini ya udikteta mkali wa Reza Khan. Hata hivyo, karibu mwaka 1329 (1950), kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, serikali ya kitaifa ya Dk. Mossadegh ilipata madaraka, ikasimama imara dhidi ya Waingereza na kufanikiwa kutaifisha mafuta ya nchi ambayo karibu yalikuwa yanatolewa bure kwao.”
Ayatollah Khamenei alitaja njama za Uingereza na washirika wake za kuiangusha serikali ya Dk. Mossadegh, akakumbusha upole na uzembe wa Mossadegh alipokuwa akiomba msaada wa Marekani ili kuikomboa Iran kutoka katika uovu wa Waingereza, na akaongeza:
“Wamarekani walimchekea Mossadegh kwa unafiki, lakini kwa kushirikiana na Waingereza walipanga mapinduzi ya kijeshi na kuiangusha serikali ya kitaifa, kisha wakamrejesha shaha (Mfalme) aliyekuwa amekimbilia nje ya nchi.”
Akasema kwamba kuangushwa kwa serikali ya kitaifa lilikuwa pigo kubwa kwa taifa la Iran, na akaongeza: “Kupitia mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 28 Mordad 1332 (1953), taifa letu liliifahamu Marekani, tabia yake ya kibeberu na hatari yake. Baada ya mapinduzi hayo na kurejea kwa Shaha, utawala wa kidikteta na wa kikatili wa Muhammad Reza Shaha uliendelea kwa miaka 25 kwa msaada na ulinzi wa Marekani.”
Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi alilitaja tukio la kwanza la Marekani kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni uamuzi wa uhasama uliopitishwa na Seneti ya Marekani, na akasema:
“Wakati Marekani ilipoamua kumpokea Muhammad Reza katika nchi yao, hasira kubwa kwa wananchi wa Iran ilizuka. Wairani walihisi kwamba kwa kumpa makazi Muhammad Reza, Marekani ilikuwa inapanga kurudia mapinduzi ya tarehe 28 Mordad na kumrudisha tena madarakani. Kwa sababu hiyo, wananchi wenye hasira walijitokeza mitaani, na sehemu ya maandamano hayo ilihusisha wanafunzi ambao hatimaye waliteka ubalozi wa Marekani.”
Akasema: “Madhumuni ya awali ya wanafunzi yalikuwa ni kukaa katika ubalozi huo kwa siku mbili au tatu tu, ili kuonesha hasira ya watu wa Iran duniani, lakini walipopata nyaraka ndani ya ubalozi huo, waligundua kwamba jambo hilo lilikuwa kubwa zaidi ya walivyodhani. Walibaini kuwa ubalozi wa Marekani kilikuwa kituo cha njama na mipango ya kuyaangamiza Mapinduzi ya Kiislamu.”
Ayatollah Khamenei alibainisha kuwa: “Kazi ya kawaida ya ubalozi duniani ni kukusanya taarifa na kuzipeleka kwa nchi zao, lakini tatizo la ubalozi wa Marekani halikuwa tu kukusanya taarifa. Ulianzisha chumba cha njama kwa ajili ya kuandaa upya mabaki ya utawala wa kifalme uliopita, baadhi ya wanajeshi na watu wengine ili wapange vitendo vya uadui dhidi ya Mapinduzi. Wanafunzi walipopata ufahamu huu, waliamua kuendelea kushikilia ubalozi huo.”
Kiongozi wa Mapinduzi aliikosoa tafsiri ya kusema kwamba “kuchukuliwa kwa ubalozi wa Marekani ndio chanzo cha matatizo kati ya Iran na Marekani,” akasema: “Si sahihi. Tatizo letu na Marekani lilianza tarehe 28 Mordad 1332, si tarehe 13 Aban 1358 (1979). Aidha, kuchukuliwa kwa ubalozi kulisababisha kufichuliwa njama kubwa dhidi ya Mapinduzi, ambayo wanafunzi walifanikiwa kuibaini na kuifichua kwa kukusanya na kuchambua nyaraka hizo.”
Ayatollah Khamenei alisema sababu kuu ya uadui na njama nyingi dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ni: “Marekani kupoteza tonge tamu lililokuwa mdomoni mwake — yaani, kumalizika kwa udhibiti wake juu ya rasilimali za Iran. Hawakuwa tayari kuiacha Iran kwa urahisi, kwa hiyo tangia mwanzo walichochea uadui, si tu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu bali hata dhidi ya taifa lote la Iran.”
Akaendelea kusema kuwa: “Uadui endelevu wa Marekani dhidi ya watu wa Iran baada ya Mapinduzi ni ushahidi wa ukweli wa maneno ya Imam Khomeini aliyesema:
‘Pazeni sauti zenu zote za hasira dhidi ya Marekani.’ Uadui wao haukuwa maneno matupu; walitumia kila njia waliyo nayo — vikwazo, njama, kusaidia uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, kumchochea Saddam aishambulie Iran na kumpa msaada wa kila aina, kuipiga risasi ndege ya abiria ya Iran yenye abiria 300, vita vya kisaikolojia, na hata mashambulizi ya kijeshi ya moja kwa moja — yote haya kwa lengo la kuidhoofisha Iran. Kwa sababu asili ya ubeberu wa Marekani haiwezi kuendana na roho huru na ya kujitegemea ya Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa hivyo, tofauti kati ya Marekani na Jamhuri ya Kiislamu si ya kimkakati, bali ni tofauti ya kimsingi na ya asili.”
Ayatollah Khamenei aliwajibu wale wanaodai kwamba “kauli mbiu ‘Mauti kwa Marekani’ ndiyo imeiletea Iran uadui dhidi ya Marekani,” akisema:
“Huu ni upotoshaji wa historia. Marekani haiwi na uhasama na sisi kwa sababu ya kauli hiyo; tatizo la Marekani ni mgongano wa kimsingi wa maslahi na asili yake isiyoweza kuendana na Mapinduzi ya Kiislamu.”
Akaendelea kwa kujibu swali la baadhi ya watu wanaouliza, “Sisi hatujajisalimisha kwa Marekani, lakini je, tutabaki bila uhusiano nayo milele?” Akasema:
“Kwanza, asili ya ubeberu wa Marekani haikubali chochote isipokuwa kujisalimisha. Marais wote wa Marekani walitaka jambo hilo, ingawa hawakulisema waziwazi. Lakini rais wa sasa wa Marekani amelisema kwa uwazi, na hivyo kufichua sura ya kweli ya Marekani.”
Ayatollah Khamenei aliongeza kuwa: “Kutarajia taifa la Iran lijisalimishe, licha ya uwezo wake mkubwa, utajiri wake, urithi wake wa kielimu na kiakili, na vijana wake wenye uelewa na ari kubwa, ni jambo lisilo na maana. Kuhusu siku za usoni za mbali, hatuwezi kutabiri; lakini kwa sasa, kila mtu anatakiwa ajue kwamba suluhisho la matatizo mengi ni kuwa na nguvu.”
Akaendelea kusisitiza: “Nchi lazima iwe imara. Serikali katika sekta zake mbalimbali, majeshi katika masuala ya kijeshi, na vijana katika elimu na taaluma lazima wafanye kazi kwa nguvu. Kwa sababu ikiwa nchi itakuwa imara na adui atahisi kwamba si tu hatapata faida kwa kuishambulia, bali ataathirika, basi bila shaka nchi itapata kinga na usalama kamili.”
Hivyo basi, nguvu za kijeshi, kielimu, kiutawala, na hasa nguvu ya ari na imani ya vijana ni ya lazima.
Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, akizungumzia baadhi ya kauli za viongozi wa Marekani kuhusiana na “hamu ya kushirikiana na Iran,” alisisitiza kuwa: “Ushirikiano na Iran hauwezi kuambatana na ushirikiano na msaada wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni ulio laaniwa.”
Aliongeza kwamba kuendeleza msaada, ulinzi na uungaji mkono wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni — licha ya fedheha na kulaaniwa kwake na fikra za umma duniani — kunalifanya ombi la Marekani la kushirikiana na Iran kuwa jambo lisilo na maana na lisilokubalika. Akasema:
“Iwapo Marekani itakomesha kabisa uungaji mkono wake kwa utawala wa Kizayuni, iondoe kambi zake za kijeshi katika eneo hili na iachane na kuingilia mambo ya mataifa mengine, basi jambo hilo linaweza kuzingatiwa — japokuwa si kwa sasa wala katika siku za karibu zijazo.”
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Ayatollah Khamenei aliwashauri vijana kuongeza maarifa na uelewa wa masuala muhimu ya kisiasa ya jana, leo na kesho ya nchi, kwa kuunda vikundi vya kielimu na vya maarifa, na kujadili matukio mema na machungu ya taifa. Alisema:
“Elimu lazima iendelee kupiga hatua nchini. Miaka michache iliyopita, mwendo wetu wa maendeleo ya kielimu ulikuwa mzuri sana, lakini sasa umeanza kushuka kidogo. Viongozi wa vyuo vikuu, watafiti na wanafunzi hawapaswi kuruhusu kasi ya kielimu ya nchi ishuke.”
Akiendelea, alisisitiza juu ya kuimarisha nguvu za kijeshi za taifa, akisema: “Sehemu ya kijeshi, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, inafanya kazi usiku na mchana na inaendelea kusonga mbele; na itaendelea zaidi ili kuthibitisha kwamba taifa la Iran ni taifa lenye nguvu ambalo hakuna nguvu yoyote duniani inayoweza kulilazimisha au kulipigisha magoti.”
Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, katika sehemu nyingine ya hotuba yake — alipolitaja jina la Bibi Zahra (a.s.) na Bibi Zaynab (a.s.) — aliwasisitizia vijana kufuata vitendo njia na mwenendo wa wanawake hawa wawili watakatifu na mashuhuri katika historia ya Kiislamu. Akasema:
“Wahimizeni wale walioko karibu nanyi kuwa na mazingatio na kujifunza kutoka katika mwenendo wa hawa watukufu.”
Ayatollah Khamenei alieleza kwamba kwa vijana, mambo yafuatayo ni ya lazima: “Kuswali kwa unyenyekevu kama wanavyoswali waja wema wa Mwenyezi Mungu; kuzingatia hijabu kama jambo la kidini, la Fatimiyyah na la Zaynabiyyah; kuwa na urafiki wa karibu na Qur’ani kwa kuisoma kila siku; na kudumisha uhusiano na masuala ya kiroho.”
Akaongeza kuwa: “Katika zama hizi zilizojaa changamoto, kijana wetu ataweza kweli kusema ‘Mauti kwa Marekani’ na kusimama imara mbele ya nguvu na vitisho vya mafir’aun wa zama hizi pale tu atakapokuwa mwenye nguvu kiimani, kidini, kiitikadi na kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu.”
Mwisho, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi alisisitiza kuwa kuendeleza uhusiano wa kiroho na wa moyoni kati ya vijana na Mola wao ni sababu ya kuendelezwa kwa maendeleo ya taifa na kuongeza uwezo wa kukabiliana na maadui.
Mwisho wa ujumbe.
            
                
Maoni yako