Shirika la Habari la Hawza - Moja ya sifa bainifu za waumini zinazowapelekea kufaulu ni kujiepusha na mambo ya puo. Ndiyo maana Qur’ani Tukufu katika kuelezea sifa zao inasema:
"وَالَّذِینَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ"
“Na wale ambao hujiepusha na upuuzi.” (1)
Sherehe:
Kutokana na Qur’ani Tukufu, neno “laghw” (upuuzi) linatumiwa kwa maana ya maneno yasiyo na maana kwa mfank:
"لا تَسْمَعُ فِیها لاغِیَةً"
“Humo (peponi) hutasikia neno lolote la upuuzi.” (2)
Vilevile, neno hilo linatumika katika matendo yasiyo na faida, kama alivyosema Mwenyezi Mungu:
"وَإِذا مَرُّوا بِاللَّغْوِ مَرُّوا كِرامًا"
“Na wanapopita karibu na upuuzi, hupita kwa heshima (bila kujishughulisha nao).” (3)
Katika zama za Imam Sajjad (a.s.), mjini Madina kulikuwa na mtu wa kuchekesha (mcheshi) aliyekuwa akiwachekesha watu kwa kufanya mambo yasiyo na faida. Siku moja, mtu huyo alimfuata Imam Sajjad (a.s.) kwa nyuma na akavuta joho la Imam kutoka mabegani mwake. Imam (a.s.) hakumjali hata kidogo. Wafuasi wa Imam walimfuata yule mtu, wakalirudisha joho kutoka mikononi mwake, na wakamletea Imam.
Imam Sajjad (a.s.) akauliza: “Mtu huyu ni nani?”
Wakamjibu: “Ni mchekeshaji wa mjini Madina ambaye huwachekesha watu kwa kufanya mambo yake.”
Imam Sajjad (a.s.) akasema: “Mwambieni:
«إِنَّ لِلَّهِ یَوْماً یَخْسَرُ فِیهِ الْمُبْطِلُونَ»
‘Hakika Mwenyezi Mungu ana siku (Kiyama) ambayo watu wanaofanya puo watapata hasara humo.’” (4)
Hivyo basi, mja Muumin — ambaye ameitambua thamani yake katika dunia hii — katika maisha yake hufuata malengo makubwa, na kwa sababu hiyo hujiepusha na chochote kinachoweza kumtoa katika njia sahihi, iwe ni maneno ya upuuzi au vitendo vya upuuzi.
Kama asemavyo Amirul-Mu’minin (a.s.):
«مَنِ اشْتَغَلَ بِالْفُضُولِ فَاتَهُ مِنْ مُهِمِّهِ الْمَأْمُولُ»
“Yeyote anayejishughulisha na mambo yasiyo na maana, atapoteza mambo muhimu anayoyatarajia.” (5)
Rejea:
1. Surat al-Mu’minun, Aya ya 3.
2. Surat al-Ghashiyah, Aya ya 11.
3. Surat al-Furqan, Aya ya 72.
4. Amali ya Shaykh Saduq, Juzuu ya 1, Ukurasa wa 220.
5. Ghurar al-Hikam, Juzuu ya 1, Ukurasa wa 627.
Imeandaliwa na Idara ya Elimu na Utamaduni ya Shirika la Habari la Hawza.
Maoni yako