Jumapili 16 Novemba 2025 - 22:52
Mwanazuoni Mashuhuri wa Lebanon Aitaka Serikali Kuchukua Msimamo Jasiri

Hawza/ Mufti wa Jaafari na mwanazuoni mashuhuri wa Kishia nchini Lebanon amesema: Hakuna shaka kwamba tajriba ya mwisho ya eneo na dunia imetuweka sisi Walebanon mbele ya ukweli mmoja wa kitaifa: kwamba hakuna mbadala wa Lebanon.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Sheikh Ahmad Qabalan, Mufti mkuu wa Jaafari na mwanazuoni mashuhuri wa Kishia nchini Lebanon, katika hotuba yake kwenye Msikiti wa Imamu Hussein (a.s) huko Burj al-Barajneh, alisema: "Hakuna shaka kwamba tajriba ya mwisho ya eneo na kimataifa imetuweka sisi Walebanon mbele ya ukweli wa kitaifa kwamba hakuna mbadala wa Lebanon. Na aina yoyote ya kuvunja ukweli huu inaiweka Lebanon na watu wake katikati ya majaribu makubwa na upotevu wa mwelekeo."

Aliongeza kuwa: “Kwa msingi huu, tofauti za kisiasa za ndani zinapaswa kusalia ndani ya kanuni ya kuilinda Lebanon na kuhakikisha masharti ya ushiriki wa kitaifa na mamlaka ya Lebanon, mbali na michezo ya maneno matupu, mitego ya kisiasa na maafikiano ya maslahi.”

Alisisitiza kwamba; baadhi wanapaswa kutambua hili ili wasije wakafeli katika mtihani wa kitaifa, hususan kwa kuzingatia kuwa Lebanon ni nchi ndogo yenye rasilimali chache katikati ya mazingira magumu ya eneo. Suluhisho ni kukazia “Ulebanoni wetu” — mbali na tamaa za madaraka, mali, ushawishi wa uchaguzi, chuki zinazoenezwa, na miradi ya Marekani ambayo haileti chochote isipokuwa machafuko na uharibifu.

Wito Kwa Umoja wa Kitaifa Dhidi ya Israel

Sheikh Qabalan alisisitiza kuwa; tunachohitaji leo ni umoja wa kitaifa dhidi ya Israel na uvamizi wake, pamoja na kujitahadhari dhidi ya njama za kigeni zinazotaka kuidhoofisha Lebanon katika ngazi ya eneo kwa gharama ya Wenye-Lebanon wote.

Akasema: “Suala ni Lebanon, siyo madhehebu fulani. Majuto hayatasaidia, na kosa lolote katika hili litatuweka katikati ya majanga makubwa.”

Alisema hakuna nguvu ya Lebanon iliyo kubwa zaidi kuliko umoja wa kitaifa unaolenga kuunga mkono juhudi za usalama na ulinzi wa taifa, bila utegemezi wa ahadi za nje zenye madhara.

Aliongeza: “Sasa ni wakati wa kuwa familia moja — Waislamu na Wakristo, Masunni na Mashia, Druze na madhehebu yote ya Kikristo. Msikiti na Kanisa, na maeneo yote ya ibada, yanapaswa kuchukua misimamo madhubuti ya kulinda nchi yetu dhidi ya ugaidi wa Kizayuni na miradi ya Marekani, ambayo ni hatari sana na inalenga kuharibu nchi za eneo kwa faida ya Israel.”

Ukosoaji wa Ukimya wa Kisiasa

Alisema kuwa vyama na makundi ya Lebanon yanapaswa kuwa na msimamo wazi kuhusu kinachoendelea kusini, Bekaa na katika masuala ya mamlaka ya kitaifa.

Akaonya kuwa: “Ukimya wa makusudi wa kisiasa ni hatari, hasa ukimya wa watu na viongozi waliokwepa kwa makusudi majukwaa ya kisiasa.” Katika hilo, alisisitiza kuwa serikali lazima ichukue misimamo ya jasiri kuonesha mshikamano wa mamlaka, kuunga mkono wananchi wa Kusini na Bekaa, na kulinda uamuzi wa kitaifa.

Madai ya Mageuzi ya Ndani na Huduma za Kijamii

Sheikh Qabalan alibainisha kuwa sera za kijamii, kiafya, kielimu na kiusalama ni lazima ili kuiweka serikali katika kiini cha uwajibikaji wa kijamii, kwani bila sera za maendeleo ya kijamii na kiuchumi Lebanon haiwezi kusimama.

Akasema: “Sasa ni wakati wa kuziendesha taasisi za serikali kwa nguvu na ufanisi, na kuzuia ufisadi mkubwa uliomo. Kauli mbiu pekee hazitoshi, wala nia njema hazifai.”

Aliashiria kuwa suluhisho liko katika: Serikali inayotoa huduma kwa umma, taasisi zenye uwezo wa kiutendaji, na mageuzi ya kidijitali, kwani kile kinachowaumiza Walebanon kimepita kiwango cha udhalilishaji.

Kuhusu Nchi na Utawala wake

Mwisho, Sheikh Qabalan alisema: “Kwa yeyote anayejali, Rais Nabih Berri ni mwamba wa demokrasia ya Lebanon, na mdhamini mkubwa wa taifa katika ngazi ya uwakilishi kiutendaji. Juhudi za baadhi yao za kubomoa ngome za uchaguzi ni usaliti wa wazi na biashara kwa faida ya wengine. Suluhisho la mwisho ni ama uwakilishi wa haki wa kitaifa au uchaguzi usiofungwa kwa mipaka ya kimadhehebu.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha