Jumamosi 1 Novemba 2025 - 06:44
Ujumbe kutoka Haram ya Imam Husayn (a.s.) watembelea kanisa la kihistoria nchini Pakistan

Hawza/ Ujumbe kutoka katika Haram Tukufu ya Imam Husayn (as), kwa lengo la kuimarisha maelewano na mazungumzo ya kidini, umetembelea kanisa la kihistoria lililoko katika mji wa Rawalpindi, na kufanya mkutano wa kirafiki na viongozi pamoja na wawakilishi wa jamii ya Wakristo katika mji huo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, ujumbe huo kutoka Haram Tukufu ya Imam Husayn (a.s.) ulifanya ziara hiyo kwa madhumuni ya kuimarisha maelewano na mazungumzo ya amani baina ya wafuasi wa dini mbalimbali. Katika ziara hiyo, pande zote mbili walibadilishana mawazo kuhusu njia za kukuza mazungumzo yenye tija, huku wakisisitiza umuhimu wa kuheshimiana, kuishi kwa amani, na kushirikiana kwenye manufaa ya pamoja kati ya wafuasi wa dini tofauti.

Wawakilishi wa kanisa, wakiisifu hatua hiyo walisema kwamba; mikutano kama hii hujenga mazingira ya kuaminiana, kuimarisha urafiki, na kukuza uhusiano wa kibinadamu katika jamii yenye dini nyingi kama Pakistan.

Mkuu wa kanisa, akionesha furaha yake, aliongeza kuwa: “Uhusiano wa aina hii hauchangii tu katika kuunda mazingira ya maelewano na mshikamano, bali pia hubeba ujumbe wa amani, urafiki, na heshima kati ya wanadamu.” Alieleza matumaini yake kwamba mwenendo huu chanya utaendelea siku za usoni kupitia vikao na shughuli za pamoja.

Mwisho wa ziara hiyo, wajumbe wa Haram ya Imam Husayn (a.s.) walitembelea sehemu mbalimbali za kanisa hilo la kihistoria lililoko Rawalpindi — jengo linalochukuliwa kuwa alama ya utofauti wa kidini, kitamaduni na ya kuishi kwa amani nchini Pakistan.

Hatimaye, pande zote mbili zilisema kwa msisitizo kwamba heshima ya pande zote, mazungumzo ya wazi, na huduma kwa binadamu ndio nguzo halisi za amani ya kudumu na maelewano ya kiroho katika jamii za kisasa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha