Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Dkt. Nāhīd Tayyibī, katika kikao cha “Nusu iliyo fichika” kilichoandaliwa na Idara ya Utamaduni ya Jihād Chuo kikuu cha Qum Iran, alisema: Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran, jukumu la wanawake wapiganiaji lilihamia nyuma ya safu za vita, na hili halikuwa na maana ya kupungua kwa hadhi ya mwanamke katika Mapinduzi ya Kiislamu.
Aliendelea kusema: Muundo wa kimaumbile wa mwanamke na mwanaume unatofautiana, kwa hiyo hatupaswi kulinganisha nafasi zao wala kuzifanya sawa. Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu hakukuwa na vita, bali kulikuwa na mapambano dhidi ya dhuluma na utawala dhalimu. Kadhalika, jihadi na vita havikuwajibishwa kwa mwanamke, lakini kupambana na dhuluma ni wajibu wa kimsingi kwake pia.
Aliongeza kusema: Watafiti wengi wa Magharibi wameashiria nafasi ya kuamua ya wanawake katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Napoleon Bonaparte alipima maendeleo ya jamii kwa fikra za wanawake wa jamii hiyo. Kwa hivyo, nafasi ya mwanamke katika jamii ni yenye ushawishi mkubwa. Kwa hakika, ushiriki wa wanawake katika Mapinduzi ya Kiislamu ulikuwa wenye athari kubwa na wa kuunda mwelekeo.
Mwalimu wa Chuo cha Jāmi‘atuz-Zahrā (a.s) alisema: Tabia ya mwanadamu huundwa katika muktadha wa mazingira. Ikiwa uwepo wa wanawake katika medani za vita ulikuwa wa moja kwa moja au usioonekana, wale waliowalea – mashahidi na wapiganaji – walikuwepo moja kwa moja katika medani za vita. Nafasi ya wanawake ilidhihirika kwa njia nyingine, ulinganisho wa kipindi cha kabla ya Mapinduzi na baada yake, hasa kwa mtazamo wa idadi ya mashahidi au uwepo wa moja kwa moja vitani, ni ulinganisho usiofaa.
Aliendelea kusema: Ushiriki wa wanawake katika Defā‘-e Moqaddas haukumaanisha uwepo wa kimwili katika medani za vita pekee. Wanawake wengi nyuma ya safu walishiriki katika maandalizi, ushonaji wa nguo, ufungaji wa vyakula, upangaji wa barua na uangalizi wa familia za wapiganaji. Aina hii ya ushiriki, ingawa haikuonekana wazi, ilikuwa na athari kubwa katika kuendeleza Vita vya Kujihami.
Tayyibī akiwataja wanawake ambao baada ya kuuwawa waume zao waliolewa na wana au ndugu wa mashahidi ili kuwatunza watoto wao, alisema: Wanawake hawa walipigana hadi mwisho wa maisha yao, ilhali wapiganaji walipigana kwa miaka minane tu wakiwa na silaha mikononi. Hii ni jihadi ya kijamii na kiutamaduni ambayo haipaswi kusahauliwa.
Mwalimu wa hawza aliongeza kusema: Jihadi siyo tu kushika silaha na kwenda vitani. Kulea watoto na kuhifadhi familia kunahesabiwa kuwa ni jihadi ya kiutamaduni. Mwanamke Mwislamu wa kweli si yule anayekaa pembeni akimsubiria mume wake, wala si yule anayebadilishwa kuwa chombo cha mfumo wa kibepari, bali ni mwanamke ambaye sambamba na kulea watoto na kutekeleza wajibu wake wa kifamilia, ana ushiriki wa kijamii pia.
Alipoulizwa jinsi ya kutumia mifano ya wanawake walioshiriki Defā‘-e Moqaddas ili kuwavutia vijana wa kizazi kipya, – hasa wasichana na wanawake vijana – katika njia ya thamani za Mapinduzi na muqāwamah, alisema: Ili kufikisha ujumbe kwa kizazi cha leo, ni lazima kwanza tuelewe lugha yao. Leo vijana wako katika ulimwengu wa kidijitali; tusipoweza kuzungumza kwa lugha yao, ujumbe wetu hautawafikia.
Aliongeza kusema: Upendo wa pamoja kama “Iran” katika vita vya siku 12 uliwakusanya wote pamoja; vijana wanapaswa kuwa pamoja. Kwa mfano, kama vijana wanataka kuleta mageuzi katika hali ya leo, ni lazima tumtambulishe Mkombozi wa ulimwengu (a.t.f.s) kwa lugha yao wenyewe. Tukibaki nje ya mtandao (offline), hatutaweza kutekeleza wajibu wetu ipasavyo.
Mtafiti wa masuala ya Defā‘-e Moqaddas aliendelea kusema: Ili kuwasilisha ujumbe huu, tunapaswa kufanya utafiti na uchunguzi. Kumbukumbu nyingi za Defā‘-e Moqaddas bado hazijaandikwa, na kumbukumbu hizo ndizo historia ya mdomo ya taifa letu. Tunapaswa kuzihifadhi kwa kutumia vifaa vya kisasa kama sauti na picha kupitia simu zetu na kuziwasilisha katika vizazi vijavyo.
Alisema: Ni lazima tuwatambue na tuwajulishe wanawake mashuhuri na wenye athari za kipindi cha VitaDefā‘-e Moqaddas. Wanawake hawa wanaweza kuwa mifano kwa kizazi kipya, na kadiri mifano hiyo inavyokuwa karibu na zama zetu, ndivyo mawasiliano yatakavyokuwa bora zaidi. Tunapaswa kutoa kumbukumbu na tajriba zao kutoka katika historia kwa mfumo maalumu na kuziandika kwa ajili ya vizazi vijavyo, kama alivyoeleza shahidi Bāqirī: “Ni lazima tuwe na kitu cha kusema kwa ajili ya historia.”
Tayyibī alipoulizwa, kwa kuzingatia mabadiliko ya kizazi na mageuzi ya vyombo vya habari, ni zana gani zinaweza kusaidia zaidi katika kueleza simulizi za wanawake wa Defā‘-e Moqaddas kwa ufanisi mkubwa zaidi, alisema: Watu wanaofaulu ni wale wanaovunja mipaka ya mazingira yao. Kitabu “Akhbār al-Wāfidāt min an-Nisā’ ‘alā Mu‘āwiyah” cha ‘Abbās bin Bakkār aḍ-Ḍabbī kinahusu wanawake 16 waliokuwa upande wa Imamu ‘Alī (a.s) katika vita vya Ṣiffīn, waliokuwa wakijihusisha na kazi mbalimbali.
Mwalimu wa chuo na wa hawza alisema: Wanawake hao walitekeleza majukumu yao kulingana na mazingira ya zama zao. Kutengeeza mustakbal huanza na mtu mmoja na kisha kuendelea. Kuwatambua wanawake waliokuwa na mchango mkubwa ni jambo linalohitajika kwa ajili ya kuweka mifano ya kuigwa katika jamii. Vilevile, kadiri mifano hiyo inavyokuwa karibu zaidi na kizazi cha vijana na zama zao, ndivyo ushawishi wake unavyokuwa mkubwa zaidi.
Tanbihi:
Defā‘-e Moqaddas: Ni istilahi maarufu nchini Iran, inayorejelea vita vilivyo piganwa kati ya Iran na Iraq (1980–1988). Vita hivyo huitwa “Difa‘-e-Muqaddas” kwa sababu vilihesabiwa kuwa jihad ya kujihami — yaani ulinzi wa taifa la Kiislamu dhidi ya uvamizi wa Saddam Hussein, na vilichukuliwa kuwa suala takatifu la kuilinda dini, ardhi, na heshima ya Waislamu.
Maoni yako