Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kuna vichocheo vingi vinavyochangia kumfanya binadamu atoke kwenye njia ya fitrah na kuukataa ukweli, na mizizi ya mambo haya imo ndani ya mioyo ya wanadamu.
Sababu za Kukengeukaka Kutoka katika Fitrah
Neno “kāfir” limetokana na mzizi wa Kiarabu “kafara” ambalo lina maana ya kufunika. Anayeitwa kāfir ni yule ambaye amefunika fitrah yake, na kwa sababu hiyo hawezi kuuona ukweli. Huku kufunika” ndiko kunakompelekea mwanadamu kupotoka kutoka kwenye fitrah, na hizi ndizo sababu kuu zinazo sababisha kupotoka ambazo baadhi tutazieleza hapa chini:
1. Kujitosheleza katika Mambo ya Uongo
Wakati mwengine watu hujaza hisia zao za kupenda kuabudu na kumpenda kiumbe mkuu asiye na haja, kwa vitu vya uongo. Mfano, baadhi hudhani kwamba masanamu ndio viumbe vya juu, na hivyo huyainamia na kuridhisha hisia zao za ibada kwa njia hiyo.
2. Ujeuri na Ukaidi
Baadhi ya watu, ingawa wamepata na kuelewa ukweli, bado wanaamua kuukataa kwa sababu ya ukaidi wao. Qur’ani inasema:
«وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَیْقَنَتْهَا أَنْفُسُهُمْ»
“Walikataa wazi, ilhali nafsi zao zilikuwa na yakini nayo.
(An-Naml: 14)
Kwa hiyo, ujeuri na ukaidi ni sababu nyingine inayowazuia watu kukubali ukweli.
3. Ukinzani na Kufuata Mababu Bila Uchambuzi
Wakati waliambiwa waamini, baadhi ya makafiri walisema:
«حَسْبُنَا مَا وَجَدْنَا عَلَیْهِ آبَاءَنَا»
Yatutosha yale tuliyowakuta nayo baba zetu.
(Al-Mā’idah: 104)
Taasubi ya kubaki katika njia za mababu — hata kama walikuwa katika ujinga — iliwazuia kupokea haki.
4. Kushindwa Kudhibiti Hisia na Matamanio
Mfano wa kihistoria ni kuua watoto wa kike katika jamii za kijahiliya kwa kisingizio cha kulinda heshima. Baadhi ya watu hukataa Mungu na Akhera si kwa sababu ya hoja, bali kwa kutaka uhuru wa kufanya maovu bila mipaka.
Qur’ani inasema:
«بَل یُرید الإنسان لِیَفْجَرَ أمامَهُ ، یَسْئَلُ أیّانَ یَومَ القیامة»
Bali mwanadamu anataka kufanya maovu bila kizuizi chochote, na huuliza: Siku ya Kiyama itakuwa lini?
(Al-Qiyāmah: 5–6)
Katika zama zetu, kujiunga na makundi ya waabudu shetani, madhehebu mapya potofu na mitazamo mingine iliyo potoka, mara nyingi ni njia ya kutoroka majukumu na kutaka uhuru wa matamanio. Watu kama hao hutaka kuishi bila mipaka ya Swala, Saumu na wajibu mwingine, wakijiendesha katika matamanio kama wanyama.
Lakini, Qur’ani na historia zinashuhudia kwamba siku itafika ambapo watatambua makosa yao, lakini majuto hayo hayatakuwa na faida tena.
Kwa Nini Baadhi ya Wataalamu wa Sayansi Hawamkubali Mungu?
1. Si wote wako hivyo. Wengi wao wanamkubali Mungu, kama vile:
Einstein,
Alexis Carrel,
Jean-Jacques Rousseau,
Darwin,
Newton, n.k.
2. Baadhi hawatilii maanani. Mfano ni daktari wa upasuaji wa macho ambae kila siku hukutana na undani wa chombo hiki, lakini hazingatii mbinu ya uumbaji wake na Muumba wake.
3. Wengine wameathiriwa na kujitosheleza kwa mambo ya uongo au sababu nyingine za upotofu zilizotajwa hapo juu.
Hitimisho
Kumjua Mungu ni asili ya ndani ya mwanadamu (fitrah), lakini vizuizi vya ndani ya moyo na akili, kama ujuaji wa uongo, ukaidi, taasubi, matamanio, na kutozingatia, ndivyo vinavyomfanya mtu atoke kwenye njia ya asili na kuukataa ukweli.
Rejea:
Qur’ani Tukufu: An-Naml 14; Al-Mā’idah 104; Al-Qiyāmah 5–6
Uṣūl ʿAqāʾid wa Pāsokh be Porsesh-hā-ye Iʿtiqādī – Muhammad Tarsalī
Maoni yako