Ijumaa 29 Agosti 2025 - 00:13
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq ataka wafungwa wa Iraq walioko Saudi Arabia waachiliwe huru

Hawza/ Fuad Hussein, katika barua aliyoandika kwa waziri wa Saudi Arabia, ameitaka serikali ya Riyadh kuwaachilia huru wafungwa wa Iraq walioko gerezani nchini humo

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Fuad Hussein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, aliikabidhi barua hiyo kwa Faisal bin Farhan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, akitaka kuachiliwa kwa wafungwa wa Iraq walioko katika magereza ya Saudi Arabia.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq ilieleza kwamba Fuad Hussein, ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu, alikutana na kufanya mazungumzo huko Jeddah na Faisal bin Farhan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia.

Katika taarifa hiyo ilibainishwa kuwa pande zote mbili walijadili njia za kukuza uhusiano wa pande mbili kati ya nchi hizo na umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa pamoja katika nyanja mbalimbali, pia wakazungumzia haja ya kuitisha haraka kikao cha kamati ya pamoja ya kisiasa na kiusalama kati ya Jamhuri ya Iraq na Saudi Arabia, ambayo ina jukumu muhimu katika kuimarisha mafungamano ya ushirikiano na uratibu.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa Fuad Hussein alimkabidhi Faisal bin Farhan barua iliyo na ombi la kuachiliwa kwa raia wa Iraq walioko gerezani Saudi Arabia, katika barua hiyo pia kumeoneshwa nia ya dhati ya serikali ya Iraq kufuatilia suala hilo kwa namna itakayozidisha uhusiano wa kindugu kati ya mataifa hayo mawili.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha