Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Ibn Hassan Amilwi, rais wa Baraza la Wanazuoni wa India, kupitia tamko rasmi, amelaani vikali kitendo cha hivi karibuni cha kituo cha televisheni "India TV" cha kusambaza madai ya uongo na ya matusi dhidi ya Ayatollah Khamenei, na kukitaja kitendo hicho kuwa ni uvunjaji wa wazi wa maadili, dini, na kanuni za kitaaluma za vyombo vya habari.
Katika tamko hilo imeelezwa kuwa: “Uislamu ni dini iliyotambulishwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kama dini inayopendeza, na Mtume wa Uislamu (saw) katika kueleza falsafa ya utume wake amesema: ‘Nimetumwa ili kukamilisha maadili mema.’ Kwa mtazamo wa Uislamu, mtu hawezi kufikia ukamilifu wa maadili hadi atakapojiweka mbali na maradhi ya kimaadili na kiroho kama vile kusingizia, uongo na uzushi.”
Aidha, tamko hilo limefafanua kwa uwazi kuwa: “Kusingizia na kutoa tuhuma za uongo dhidi ya watu, katika Uislamu ni miongoni mwa madhambi makubwa,” kama Qur’ani Tukufu inavyosema: "Laana ya Mungu iwashukie wasema urongo" (Aal Imran: 61).
Vilevile, kwa mujibu wa riwaya ya Amirul-Mu’minin (as), “kusingizia kwa dhulma dhidi ya watu wasio na hatia ni dhambi nzito mno kiasi kwamba mbingu haziwezi kubeba uzito wake.”
Uzushi dhidi ya Marjaa mkubwa wa Ushia, ni kitendo kisichosameheka
Kwa mujibu wa tamko hilo, kituo cha "India TV" mnamo tarehe 27 Julai 2025, katika moja ya vipindi vyake, kilisambaza madai ya uongo na ya matusi dhidi ya shakhsia tukufu ya Ayatollah Khamenei, uzushi huu ambao hapo awali ulikuwa umetolewa na shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni (Mossad), ulichapishwa na chombo hicho cha habari cha Kihindi bila kufanya uchunguzi wowote juu ya ukweli wake.
Rais wa Baraza la Wanazuoni wa India katika kulaani kitendo hiki alisema:
“Chombo cha habari ambacho kinapaswa kuwa sauti ya ukweli, maadili na uelewa, kinawezaje kusambaza uongo wa wazi, tena dhidi ya shakhsia kama Ayatollah Khamenei – kiongozi na Marjaa wa mamilioni ya Waislamu duniani – bila hata kufikiria? Kitendo hiki hakioneshi tu ujinga wa kidini wa baadhi ya watu wa vyombo vya habari, bali pia kinaonesha upungufu wa kuelewa nafasi ya Marjaa wa Ushia katika ulimwengu wa Kiislamu.”
Katika sehemu nyingine ya tamko hilo, kwa kuashiria hadhi ya kielimu, kifiqhi na kiroho ya Ayatollah Khamenei, imeelezwa kuwa:
“Ayatollah Khamenei si tu kiongozi mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, bali pia ni Marjaa mashuhuri na faqihi mkubwa miongoni mwa Mashia duniani, mwenye sifa zote za marjaa, ikiwemo uadilifu, taqwa, elimu, akili, busara na usafi wa nasaba. Mashia duniani kote, wakiwemo wa India, huweka picha zake kwa heshima majumbani, kwenye Huseinia na katika sherehe za kidini, na humfuata kama Marjaa wao wa kidini.”
Wito rasmi wa kuomba msamaha na kuchukuliwa hatua za kisheria
Mwisho wa tamko hilo, Hujjatul-Islam Ibn Hassan Amilwi, kwa kuonesha masikitiko makubwa juu ya matusi haya ya wazi dhidi ya marjaa, alitangaza kuwa:
“Tunataka kituo cha "India TV" kimuombe msamaha rasmi na hadharani Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na Mashia wote duniani, hususan Mashia wa India. Vilevile, tunatarajia serikali ya India ichukue hatua za kisheria dhidi ya chombo hiki cha habari, kwani kitendo hiki si tu ni matusi dhidi ya shakhsia ya kidini, bali pia ni kudhalilisha mmoja wa viongozi mashuhuri wa kisiasa na kidini duniani, jambo ambalo linaweza kuleta athari za ndani na za kimataifa.”
Mwisho wa tamko hilo, akivihutubia vyombo vya habari vya Kihindi, ameeleza: “Ikiwa nyumba yenu ni ya vioo, msitupie mawe nyumba za wengine. Kufata maadili, dini na maadili ya kitaaluma katika vyombo vya habari ni matarajio ya msingi ya watu kutoka kwenu.”
Hujjatul-Islam Ibn Hassan Amilwi,
Rais wa Baraza la Wanazuoni na Wahubiri wa India.
Maoni yako