Jumapili 27 Julai 2025 - 11:59
Shahidi Nasrallah ni shule ya kifikra na ya kimapinduzi yenye athari ya kiistratejia / “Umanau al-Rusul”; hatua ya kuwafahamisha vijana urithi wa kihistoria

Hawza/ Ayatollah Arafi, akisisitiza nafasi maalumu ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah (r.a.), amemtaja si tu kama kamanda na kiongozi mashuhuri wa muqawama, bali pia kama mmiliki wa shule ya kifikra, kijamii na kisiasa iliyobadilisha hesabu za kieneo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Alireza Arafi, usiku wa Jumamosi tarehe 4 Mordad 1404, katika hafla ya uzinduzi wa bango la wito wa makala kwa ajili ya kongamano la kielimu na kimataifa “Umanau al-Rusul"; Kuheshimu hadhi ya kielimu na kijihadi ya Sayyid al-Shuhada wa Muqawama, Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah”, iliyofanyika katika ukumbi wa vikao wa kituo cha uongozi wa Hawza Qom, kwa kuadhimisha kumbukumbu ya mashahidi wa umma wa Kiislamu, alisema:

Tunaiheshimu na kuikumbuka kumbukumbu ya mashahidi wakubwa wa umma wa Kiislamu; mashahidi waliotoa roho zao katika mapambano dhidi ya uzayuni wa kimataifa, hususan Shahidi mwenye heshima kuu Sayyid Hassan Nasrallah, wanasayansi na makamanda mashahidi, pamoja na wananchi wapendwa na mashahidi wote wa matukio ya hivi karibuni na ulinzi wa kimaadili wa siku 12.

Akiendelea kwa kuashiria hali ya wananchi wa Palestina alisema: Mwanzoni mwa hotuba, tunatangaza mshikamano wetu wa kina na wananchi wa Palestina hususan watu wa Ghaza, hasa watoto, vijana na wapendwa wanaoishi katika hali ngumu zaidi ya maisha huko Gaza. Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aondoe tabu na matatizo haya kutoka mabegani mwao na airudishe shari ya maadui wa umma wa Kiislamu na Iran ya Kiislamu kwao wenyewe.

Mkurugenzi wa Hawza Iran, aliendelea kubainisha malengo ya kongamano la “Umanau’ al-Rusul” na kusema: “Umanau’ al-Rusul” ni mkusanyiko wenye lengo la kutambua na kuwafahamisha wanachuoni wakubwa waliokuwepo hawza na waliokuwa na athari kubwa katika fikra na utamaduni wa Iran na eneo hili, na waliokuwa na nafasi muhimu katika mchakato wa kijamii, kisiasa na kitamaduni. Mkusanyiko huu unajitahidi kuwatambulisha watu hawa kwenye jamii, si tu nchini Iran bali pia katika eneo hili, ukiwa na mtazamo maalumu kwa hawza mbili za Qom na Najaf; hawza mbili kuu na vituo viwili vya kihistoria vya fikra na utamaduni wa Kiislamu, Kiimani na Kishia vinavyoathiri ulimwengu wa Kiislamu, na unakusudia kuzikaribisha zaidi hawza hizi mbili.

Mkurugenzi wa Hawza nchini Irani aliongeza: “Umanau’ al-Rusul” inawatambua wakubwa wa hawza hizi mbili waliokuwa na nafasi ya juu ya kielimu, kitamaduni na kijamii, inasoma upya sera zao na inazifahamisha katika jamii.

Ayatollah Arafi, kisha alielezea kuhusu nafasi ya kihistoria na yenye athari ya hawza ya Qom na Najaf na kusema: Hawza hizi mbili katika historia zimekuwa na nafasi na umaarufu wa kipekee, na katika karne za hivi karibuni, hawza za Qom na Najaf zimekuwa chimbuko na mwanzo wa mageuzi makubwa katika eneo hili; kuanzia harakati ya kikatiba na harakati ya kitaifa ya kutaifisha mafuta hadi mapinduzi ya Kiislamu na matukio muhimu yaliyotokea Iraq na katika eneo hili.

Ayatollah Arafi, akieleza upana wa ushawishi wa hawza hizi mbili, aliongeza: Kuna matukio na misururu ya matukio makubwa ya kijamii na kitamaduni yenye mizizi katika vituo vyetu vya kielimu, kutoka vyuo vikuu hadi hawza, lakini hawza hizi mbili zimekuwa na nafasi muhimu na maalumu na watu wakubwa wametoka humo ambao wamekuwa na athari katika sehemu mbali mbali za dunia.

Mkurugenzi wa Hawza, akieleza malengo ya mkusanyiko wa “Umanau’ al-Rusul” katika kuimarisha mahusiano ya kielimu ya hawza, alisema: Mkusanyiko huu unalenga kuimarisha uhusiano wa taasisi za hawza hizi mbili na unachukua hatua katika kuwatambua watu wanaoweza kuwa mfano wa kuigwa katika kizazi kipya na jamii.

Akiashiria shughuli zilizofanyika katika mwelekeo huu, alibainisha kuwa: Hadi sasa programu kadhaa zimefanyika ambazo zimeonesha matokeo mazuri, machapisho makubwa yametolewa na vikao muhimu vimefanyika Qom na Najaf katika uwanja huu.

Ayatollah Arafi alitangaza mipango mipya ya “Umanau’ al-Rusul” kwa ajili ya kuwakumbuka watu mashuhuri wa umma wa Kiislamu na akasema: Katika hatua mpya iliyojadiliwa katika baraza la sera miezi ya hivi karibuni na kufuatiliwa ni kwamba, upo mpango wa kumkumbuka kila mmoja miongoni mwa watu muhimu, ambao kila mmoja ana nafasi ya kipekee kutoka mtazamo fulani.

Akaendelea kwa kusema: Mtu wa kwanza ni Shahidi Alim Sayyid Hassan Nasrallah (Rahmatullahi Alayh), kamanda mkubwa wa muqawama na sura mashuhuri ya kisiasa na ya kimapinduzi, ambaye utambulisho wa shakhsia yake, nafasi yake ya kielimu na kina cha fikra yake ya kisiasa na kijamii upo katika hatua ya utafiti na uchambuzi. Tunatarajia katika mwaka ujao kufanyika vikao muhimu Qom, Najaf na Lebanon kwa ajili ya kumheshimu mtu huyu mtukufu.

Ayatollah Arafi, akiashiria ujuzi wake wa karibu na shakhsia hii kubwa, alisema: Kuhusu Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, ambaye nilipata heshima ya kuwa na uhusiano wa karibu naye na mara nyingi kushiriki vikao virefu, wakati mwingine hadi usiku wa manane mjini Beirut nikiwa katika huduma yake, kuna mambo kadhaa yanayoweza kutajwa yanayoonyesha umuhimu wa kongamano hili.

Akibainisha vipengele vya kielimu na kifikra vya Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, alisema: Kwanza, Shahidi Nasrallah alikuwa mwanafunzi wa hawza ya Qom na Najaf. Alisoma Najaf na pia alipita kipindi fulani Qom, akifaidika na mitazamo mbalimbali ya kielimu na kitamaduni ya hawza muhimu za Qom na Najaf.

Mkurugenzi wa Hawza aliongeza kuwa: Pili, alikuwa chini ya ushawishi wa marehemu Shahidi Sadr na kwa mwendelezo wake, akawa chini ya kivuli cha fikra za Imam Khomeini (r.a.), uongozi na mapinduzi ya Kiislamu, na haraka akafikia nafasi ya kuwa kiongozi mkubwa nchini Lebanon, katika eneo, ulimwengu wa Kiislamu na miongoni mwa viongozi mashuhuri wa kifikra na kimapinduzi duniani.

Akaendelea kwa kusema: Miongoni mwa sifa mashuhuri katika shakhsia yake ilikuwa ni kuwa na fikra ya kistratejia ya kipekee, kiasi kwamba tunaweza kusema alikuwa mmoja wa sura zilizobadilisha hesabu za kieneo na alicheza nafasi muhimu katika mchakato huo. Pia alikuwa kivutio kikubwa kwa Kiongozi wa Juu wa Mapinduzi ya Kiislamu na sura kubwa ziliibuliwa chini ya malezi yake.

Ayatollah Arafi, akihitimisha hotuba yake kuhusu shakhsia ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, kwa kusisitiza: Kwa hakika Shahidi Nasrallah ni shule ya kifikra, kijamii, kitamaduni, ya kimapinduzi na kisiasa, na kongamano hili linakusudia kusoma upya shule hii na kutambua vipengele na mafundisho ya fikra hii mashuhuri.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha