Jumamosi 19 Julai 2025 - 10:14
Namna ya Ghaiba ya Imam Mahdi (as)

Hawzah/ Je, ghaiba ya Bwana wa Amri as iko vipi? Je, mwili wake mtukufu umefichika machoni mwa watu? Au kwamba mwili wake huonekana lakini hakuna anayemjua?

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Inapaswa kueleweka kuwa kufichika kwa mwili wa mtu au vitu vingine na kufichika kwa vitendo na mienendo ya mwanadamu machoni mwa waliohudhuria si jambo geni katika historia ya miujiza na karama za Manabii, Mawalii na waumini maalumu; bali jambo hilo limetokea mara nyingi.

Miongoni mwa dalili ni tafsiri ya aya tukufu:

«وَ إِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ جَعَلْنَا بَیْنَکَ وَ بَیْنَ الَّذِینَ لَا یُؤْمِنُونَ بِاْلآخِرَهِ حِجَاباً مَسْتُوراً.»

Na unaposoma Qur’ani, tunaweka baina yako na wale wasioamini Akhera, pazia lililofunikwa. (Isra/45)

Pamoja na kwamba dhahiri ya aya inaonesha kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu alimdhibiti Mtume Mtukufu (saw) asiweze kuonekana na makafiri waliotaka kumdhuru wakati alipokuwa akisoma Qur’ani, katika baadhi ya tafsiri imeelezwa kuwa Mwenyezi Mungu alimficha Mtume (saw) wakati anasoma Qur’ani kuepukana na Abu Sufyan, Nadr bin Harith, Abu Jahl, na Ḥammālat al-hatab, Walikuja na walipita karibu yake lakini hawakumuona. (Ṭabarsī, Majma al-Bayān, j.6, uk. 645; Suyūṭī, al-Durr al-Manthūr, j.4, uk. 186)

Ibn Hishām katika Sīrah amenukuu simulizi ya kufichika kwa Mtume mtukufu (saw) machoni mwa Ummi Jamil Hammālat al-Hatab, ambayo mwishoni mwa simulizi hiyo, amelinukuu tamko hili kutoka kwa Mtume (saw):

«لَقَدْ أَخَذَ اللهُ بِبَصَرِهَا عَنِّی.»

Hakika Mwenyezi Mungu alichukua uwezo wa kuona wake juu yangu. (Ibn Hishām, j.1, uk. 238; na riwaya nyingine)

Wakati wa Hijra kutoka Makka kwenda Madina pia, kwa mujibu wa historia thabiti, washirikina waliokuwa wamesimama mlangoni mwa nyumba ya Mtume (saw) kwa ajili ya kumuua, hawakuweza kumuona. Ilikuwa hivi: baada ya kumwamuru Imam Ali (as) alale kitandani kwake, alitoka nje, akachukua mchanga na kuwatupia vichwani mwao na akasoma:

«یٰس وَ الْقُرْآنِ الْحَکِیمِ.»

hadi

«فَهُمْ لَا یُبْصِرُونَ.»

kisha akapita kati yao, na hakuna aliyemuona.

(Ibn Hishām, j.2, uk. 333; Ibn Saʿd, al-Ṭabaqāt al-Kubrā, j.1, uk. 227–228; Ibn Athīr Jazrī, al-Kāmil fī Tārīkh, j.2, uk. 103)

Na katika tafsiri ya Al-Durr al-Manthūr kuna simulizi ndefu kuhusu habari aliyoisimulia Imam Jaʿfar al-Ṣādiq (as) kutoka kwa baba yake, naye kutoka kwa Imam Zaynul-ʿĀbidīn, naye kutoka kwa Amīr al-Muʾminīn (as), ambayo ni miongoni mwa vielelezo vya jambo hili.

Vilevile katika tafsiri ya aya tukufu:

«وَجَعَلْنَا مِنْ بَیْنِ أَیْدِیهِمْ سَدّاً وَ مِنْ خَلْفِهِمْ سَدّاً فَاَغْشَیْنَاهُمْ فَهُمْ لَایُبْصِرُونَ.»

Na tumeweka mbele yao kizuizi na nyuma yao kizuizi, na tukawafunika, hivyo hawaoni. (Yāsīn/9)


katika vitabu vya tafsiri kuna riwaya zinazothibitisha jambo hili.

(Tusi, al-Tibyān, j.8, uk. 446; Tabarsī, Majmaʿ al-Bayān, j.8, uk. 649–650; Suyūṭī, al-Durr al-Manthūr, j.5, uk. 258–259; na tafsiri nyingine)

Katika historia ya maisha ya Maimamu (as) pia kuna vielelezo vingi vya jambo hili; kama kufichika kwa Imam Zaynul-Ābidīn (as) machoni mwa wapelelezi wa ʿAbdul-Malik bin Marwān, jambo ambalo limenukuliwa si tu na wanachuoni wa Kishia, bali hata wanazuoni wa Kisunni kama Ibn Ḥajar.

(Ibn Ḥajar Haythamī, al-Ṣawāʿiq al-Muḥriqah, uk. 200)

Hivyo basi, suala la kufichika kwa mtu si jambo geni bali limeshatokea kihistoria.

Ama kufichika kwa anuani na kutotambulika mtu bila ya kufichika mwili, hilo ni jambo jepesi na rahisi, na mara nyingi halihitaji miujiza wala kuvunja ada za kawaida. Kila siku huwaona watu waliopo mbele ya macho yetu lakini hatuwatambui.

Baada ya utangulizi huu, tunatoa jibu la swali:

Ingawa falsafa, uhalali na manufaa ya ghaiba hupatikana kwa njia zote mbili (kufichika kwa mwili na kutotambulikana), na lengo la ghaiba kwamba Imam as afichwe au watu wasimtambue au wasiweze kumdhuru, linapatikana katika hali zote mbili, lakini kutokana na mjumuisho wa riwaya na simulizi za watu waliopata bahati ya kuonana na Imam huyo mtukufu, na kutokana na kutafsiriana kwa baadhi ya riwayahizo, 

inadhihirika kwamba ghaiba ya Imam Mahdi (as) imetokea kwa sura zote mbili: (kutoonekana machoni na kutotambulikana). Na hata wakati mwingine, kwa wakati mmoja, aina zote mbili za ghaiba hutokea; yaani mtu mmoja anaweza kumuona lakini asimtambue, na mwingine katika wakati huohuo asimuone kabisa. Kama ilivyokuwa kwa Mtume Mtukufu (saw) katika baadhi ya matukio yaliyoashiriwa: baadhi ya watu walimuona, na baadhi hawakumuona.

Jambo la kuzingatia ni kuwa ghaiba ya mwili haiwezi kutokea pasipo muujiza na kuvunjwa kwa ada, lakini kufichika kwa jina, cheo na kutotambulikana kunaweza kutokea kwa hali ya kawaida, ingawa katika baadhi ya nyakati, kwa ajili ya kudumu kwa ghaiba au kuwazuia watu kuamsha hisia za utafiti na kutafuta utambulisho, panahitajika kuvunjwa kwa ada na kuingiliwa kwa nafsi, jambo ambalo Mwenyezi Mungu Mwenye uwezo hulitekeleza kupitia Imam huyo mwenyewe au moja kwa moja – kwa namna yoyote ile ambayo inafaa – kwa ajili ya kutimiza mapenzi Yake na kumhifadhi mteule Wake as.

Utafiti huu unaendelea…

Imenukuliwa kutoka katika kitabu kiitwacho: "Majibu kwa Maswali Kumi Kuhusu Uimamu", kilichoandikwa na Ayatollah Sāfī Golpāyigānī – huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha