Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Yasin Musawi, Imamu wa Ijumaa wa Baghdad na mwalimu mashuhuri wa Hawza ya Najaf Ashraf, amesisitiza kuwa; haiwezekani kuitenganisha Iraq na utambulisho wake wa Kiislamu, madhehebu ya Kishia na Maraji' wake wa kidini.
Akikosoa matumizi ya dhana za utaifa na uzalendo kama nyenzo za kisiasa, kwa namna inayosababisha kudhoofika mafungamano ya kihistoria na kiitikadi ya wananchi wa Iraq na Ahlul-Bayt (as), pamoja na mataifa mengine ya Kiislamu, amepinga mtazamo huo.
Kauli hizo zilitolewa katika hotuba ya kisiasa ya Swala ya Ijumaa ya tarehe 30 Oktoba 2026. Katika hotuba hiyo, Imamu wa Ijumaa wa Baghdad alizungumzia masuala mbalimbali, yakiwemo uhusiano kati ya itikadi za kidini na uzalendo, dhana ya utambulisho wa Kiiraq, uhusiano kati ya Iraq na Iran, pamoja na utendaji wa baadhi ya makundi ya kisiasa na kile alichokiita kusalimu amri kwao mbele ya shinikizo la Marekani.
Vita vya dhana na utambulisho
Ayatullah Musawi alisema kuwa; kuibuliwa kwa mtazamo unaodai kwamba ni lazima kuifanyia kazi Iraq bila kujali dini, madhehebu, kabila na chama, pamoja na swali la iwapo uzalendo unapaswa kutangulizwa mbele ya itikadi za kidini pale zinapokinzana, kunahitajika kupitiwa upya dhana hizo na kubainisha misingi pamoja na marejeo yake ya kimawazo. Si sahihi kuzichukulia dhana hizo kuwa ni mambo yaliyo wazi na yasiyohitaji kujadiliwa, bila ya kuzifanyia uchunguzi na mazungumzo.
Akigusia uzoefu wake wa miaka ya 1990, alieleza kuhusu uandishi wa kitabu chake kilichoitwa Mulahadhat (Mazingatio), ambacho alikiandika kwa ajili ya kutetea itikadi ya Ushia, pamoja na jaribio la kutaka kumuua kutokana na misimamo na maandishi yake.
Imamu wa Ijumaa wa Baghdad alitaka kupanuliwa mijadala na mazungumzo kuhusu dhana zinazotumika katika nyanja za kisiasa na kimawazo, pamoja na kuchunguza kiwango cha usahihi na uhalali wake.
Utaifa na uzalendo katika mizani ya historia
Ayatullah Musawi, akieleza kuwa utaifa na uzalendo katika sura zake za kisiasa na za kisasa viliibuka kutokana na mazingira maalumu ya kihistoria, alibainisha kuwa kuzigawa jamii za Kiislamu katika utambulisho finyu wa kikabila na kitaifa kumechangia kudhoofisha dhana ya Umma mmoja wa Kiislamu.
Akiuliza ni marejeo gani yanayopaswa kurejewa ili kubaini usahihi au kutokuwa sahihi kwa dhana za kisiasa, alisisitiza kuwa kipimo cha kutathmini dhana hizo hakipaswi kuwa misimamo ya wanasiasa na wanaharakati wa vyombo vya habari, bali Qur’ani Tukufu na mafundisho ya Ahlul-Bayt (as) yanapaswa kuwa msingi wa kutoa hukumu.
Aidha, Ayatullah Musawi, akigusia dhana ya “Darul-Islam” katika urithi wa kifiqhi wa Uislamu, alibainisha kuwa utambulisho na uhusiano wa Kiislamu ni mpana zaidi kuliko mipaka ya kisiasa na kikabila iliyopo katika zama za sasa.
Shahidi Muhammad Baqir Sadr na mipaka ya Sykes-Picot
Katika kuendelea na hotuba yake, Imamu wa Ijumaa wa Baghdad aligusia msimamo wa Shahidi Ayatullah Sayyid Muhammad Baqir Sadr wa kuunga mkono Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, na kusema: “Shahidi Sadr aliutetea msimamo wake kwa msingi wa imani yake katika umoja wa Umma wa Kiislamu. Hakuona mipaka iliyochorwa na madola ya kikoloni, ikiwemo mipaka iliyowekwa katika mfumo wa Makubaliano ya Sykes-Picot, kuwa ni msingi wa kukatisha mafungamano kati ya mataifa ya Kiislamu.”
Ayatullah Musawi alisisitiza kuwa; kupinga mipaka hiyo kwa kuichukulia kuwa ni vizuizi vinavyokwamisha mawasiliano kati ya mataifa hakumaanishi kutoa wito wa Iraq kuwa chini ya mamlaka ya nchi nyingine. Bali, lengo ni kuhifadhi uhuru wa Iraq sambamba na kulinda uhusiano wake wa kidini na kihistoria na mataifa mengine ya Kiislamu.
Iraq na kina cha historia yake katika mafundisho ya Ahlul-Bayt (as)
Imamu wa Ijumaa wa Baghdad, akisisitiza nafasi ya pekee ya Iraq katika dhamiri na imani za Mashia duniani kote, alisema kuwa; miji mitakatifu ya nchi hiyo ina uhusiano wa kina na historia ya Ahlul-Bayt (as), na kwamba uwepo wa makaburi matukufu ya Maimamu watukufu pamoja na vituo vya Hawza vimeipa Iraq nafasi ya kipekee.
Akigusia nafasi ya Najaf Ashraf, Karbala Mualla na Samarra, aliongeza kuwa; kuzuru kaburi la Imam Hussein (as) na udongo mtakatifu wa Karbala kuna thamani na nafasi kubwa ya kidini na kiroho miongoni mwa Mashia katika maeneo mbalimbali ya dunia.
Ayatullah Musawi alibainisha kuwa; uhusiano wa wananchi wa Iraq na Ahlul-Bayt (as) si uhusiano wa kijiografia pekee, bali una mizizi katika mwendelezo wa kina na imara wa kihistoria na kiitikadi, ambao hauwezi kutenganishwa na utambulisho na historia ya jamii ya Iraq.
Kupinga kusitishwa uhusiano kati ya Iraq na Iran
Imamu wa Ijumaa wa Baghdad, akikosoa mitazamo inayowasilisha uhusiano kati ya Iraq na Iran kana kwamba ni makabiliano kati ya tambulisho mbili zinazokinzana, alisema kuwa; lengo la makundi hayo ni kudhoofisha mafungamano ya kidini na kijamii kati ya mataifa hayo mawili. Katika muktadha huo, aligusia uwepo wa wapiganaji na makamanda wa Iran waliokuwa pamoja na vikosi vya Iraq na vikosi vya Hashd al-Shaabi katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS).
Ayatullah Musawi alisisitiza kuwa; kutetea mamlaka na uhuru wa kitaifa wa Iraq hakumaanishi kukatiza uhusiano wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ni kwa sababu uhusiano wa nchi hizo mbili unazidi hesabu finyu za kisiasa, na umejengwa juu ya mafungamano ya kina ya kidini, kihistoria na kijamii.
Kukosoa vikwazo dhidi ya mazuwari na shinikizo la Marekani
Aidha, Ayatullah Musawi alizungumzia vikwazo ambavyo, kwa mujibu wa maelezo yake, vinawekwa dhidi ya mazuwari wanaokwenda kuzuru kaburi la Imam Hussein (as). Akikosoa baadhi ya hatua na vikwazo vinavyohusiana na safari za ndege na mipaka ya nchi kavu, alisisitiza: “Haipaswi kuwawekea mazuwari shinikizo kwa kutumia vikwazo vya aina hii, wala hatua hizo hazipaswi kutumiwa kama nyenzo ya kuweka shinikizo katika uhusiano kati ya Iraq na Iran.”
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Imamu wa Ijumaa wa Baghdad alikosoa vikali baadhi ya makundi ya kisiasa huku akiyashutumu kusalimu amri mbele ya matakwa ya Marekani na kutanguliza maslahi yao binafsi na ya vyama vyao mbele ya maslahi ya wananchi.
Akigusia kupanda bei, kuzorota hali ya maisha ya wananchi na kuongezeka mzigo wa matatizo ya kiuchumi, kwa upande mwingine alikosoa mrundikano wa utajiri mikononi mwa baadhi ya viongozi.
Maoni yako