Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, wimbi jipya la maandamano ya wananchi nchini Ufaransa, licha ya kuwepo vizuizi vingi na uwepo wa maelfu ya askari polisi na askari wa Gendarmerie, serikali ya Macron imekabiliwa tena na changamoto kubwa, nao waandamanaji, kwa kuandaa mgomo wa tarehe 5 Novemba, wanataka harakati za maandamano zipanuliwe zaidi.
Siku ya Jumamosi, tarehe 31 Oktoba, zaidi ya watu 500,000 waliingia tena mitaani na kufanya maandamano katika maeneo mbalimbali ya Ufaransa. Hali hiyo ilijiri wakati ambapo serikali ilikuwa imejaribu kuiweka nchi katika mazingira ya vizuizi na udhibiti mkali. Baada ya siku hiyo mpya ya maandamano, sasa ni muhimu kujiandaa kwa kuanza mgomo kuanzia tarehe 5 Novemba na kuendelea kwake!
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na miungano ya pamoja ya vyama vya wafanyakazi na wanafunzi, siku ya Jumamosi, tarehe 31 Oktoba, zaidi ya watu 500,000 walifanya maandamano katika maeneo mbalimbali ya nchi, licha ya hatua kubwa za ukandamizaji zilizochukuliwa. Serikali ilikuwa imetumia tena juhudi zake zote kuzuia maandamano yasijitokeze. Hatua hizo zilijumuisha kupiga marufuku maandamano au kuyahamishia katika maeneo yaliyo mbali na katikati ya miji, kufanya ukaguzi na upekuzi takribani 40,000 kwa siku nzima, kuwakamata karibu watu 300, kuwatumia askari polisi na Gendarmerie 70,000 pamoja na vikosi vya kupambana na ugaidi, kupeleka magari ya kivita mitaani, na pia kutoa vitisho na kudhibiti maudhui yanayohusiana na maandamano katika mtandao wa TikTok, pamoja na hatua nyinginezo.
Hata hivyo, Lecornu na Macron wameshindwa tena kufikia lengo lao, kwani maandamano yamefanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo kwa ushiriki mkubwa wa wananchi.
Mjini Paris, zaidi ya watu 200,000 waliingia mitaani. Katika mji wa Rennes, miungano ya pamoja ya vyama vya wafanyakazi ilitangaza kuwa waandamanaji 20,000 walishiriki. Katika miji mingine, ambako takwimu sahihi za idadi ya waandamanaji bado hazijatolewa, awamu ya tatu ya harakati za kupinga kupanda gharama za maisha na gharama kubwa za kujikimu nayo ilishuhudia mwitikio mkubwa.
Katika mji wa Le Mans, mamia ya watu walikusanyika mbele ya hospitali ili kufanya mkutano mkuu na kujadili namna ya kuendeleza harakati za maandamano. Katika maeneo mengi pia, waandamanaji walionyesha moyo wa kupambana na azma thabiti. Mfano ni katika mji wa Marseille, ambako waandamanaji waliendelea na maandamano yao licha ya marufuku iliyotolewa na mamlaka ya mkoa. Nao mjini Toulouse, polisi walianza kutawanya mikusanyiko ya waandamanaji tangu mwanzo kabisa wa maandamano hayo.
Mjini Paris, kutokana na marufuku zilizowekwa na serikali, mkusanyiko wa maandamano ulifanyika katika njia iliyopo kati ya malango ya Porte de Bagnolet na Porte de Charenton. Hata hivyo, tofauti na ilivyokuwa tarehe 24 Oktoba, mamia kadhaa ya wanafunzi waliitikia wito wa “Uratibu wa Kikanda wa Wanafunzi wa Île-de-France” na, kwa kupaza kaulimbiu isemayo, “Iwe Nuñez anataka au hataki”, walipinga marufuku ya maandamano.
Baada ya polisi kuwazunguka wanafunzi hao kwa muda mfupi, hatimaye walilazimika kuruhusu umati wa vijana wapatao 1,000 kuungana na maandamano makubwa yaliyokuwa yakifanyika katika lango la kuingilia mjini Paris.
Kwa njia hiyo, vijana walionyesha kwamba inawezekana kubadilisha mizania ya nguvu kwa kutotii maagizo ya serikali na kutokubali vizuizi vinavyowekwa, kwa sharti la kukataa kusalimu amri mbele ya maagizo ya serikali, tofauti na msimamo ambao umekuwa ukichukuliwa hadi sasa na mashirika makubwa ya vyama vya wafanyakazi na kisiasa.
Maoni yako