Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, kutokana na kuendelea kwa maandamano na kuenea machafuko mitaani, serikali ya Ufaransa imetangaza kuweka vizuizi vipya vya kutotoka nje. Uamuzi huo umechukuliwa wakati maandamano ya wanafunzi yakiingia katika wiki yake ya nne, huku madai ya waandamanaji yakivuka mipaka ya kutaka kuboreshwa mazingira ya shule.
Sébastien Lecornu, Waziri Mkuu wa Ufaransa, alitangaza Jumanne kupitia akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba utekelezaji wa kanuni maalumu za kutotoka nje katika maeneo husika ulisaidia kurejesha utulivu katika usiku uliotangulia.
Alisema: “Usiku wa leo, katika maeneo ambayo hali itahitaji hatua hiyo, kanuni mpya za kutotoka nje zitawekwa. Maamuzi haya yatafanywa katika ngazi za maeneo husika na wakuu wa mikoa, kwa uratibu na madiwani wa miji.”
Siku ya Jumatatu, maafisa wa Ufaransa waliweka kanuni za kutotoka nje katika miji kadhaa ya kaskazini mwa nchi hiyo na pia katika jiji la Lyon. Hatua hizo zilichukuliwa sambamba na kuwekwa vizuizi vya usafiri na kupigwa marufuku mikusanyiko ya maandamano katika baadhi ya vitongoji vya Paris.
Aidha, kwa ombi la Sébastien Lecornu, kanuni maalumu za kutotoka nje watu walio chini ya umri wa utu uzima zilianza kutekelezwa katika jiji la Nice. Uamuzi huo ulifuatia vitendo vya vurugu vilivyotokea wakati wa maandamano ya hivi karibuni nchini Ufaransa.
Mwishoni mwa juma, Ufaransa ilishuhudia kuongezeka maandamano na kuenea vurugu katika miji kadhaa nchini humo. Huko Paris, mikusanyiko ya waandamanaji ilisababisha hata kuzibwa lango la kuingia katika Jumba la Makumbusho la Louvre.
Miongoni mwa waandamanaji walikuwepo wanafunzi wa shule ya Louvre, ambao walijitokeza kuonyesha mshikamano wao na vuguvugu la wanafunzi wa shule za sekondari na kupinga kile wanachokiita “ukandamizaji wa polisi.”
Matukio haya yanajiri katika muktadha wa vuguvugu la maandamano ambalo limeendelea kwa wiki nne. Hapo awali, wanafunzi wa shule za sekondari walianza maandamano hayo wakitaka kuboreshwa mazingira ya shule zao. Hata hivyo, wigo wa madai yao umeongezeka na sasa unajumuisha pia maandamano dhidi ya kupanda kwa kasi gharama za maisha.
Wakati huohuo, Laurent Nuñez, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, alikiri Jumatatu kwamba vikosi vya polisi vilishindwa kudhibiti hali katika baadhi ya miji wakati wa vurugu zilizotokea pembezoni mwa maandamano ya mwishoni mwa juma.
Pia alitangaza kuwa siku ya Jumamosi, takribani askari 60,000 wa polisi na gendarmerie walikuwa wamepelekwa katika maeneo mbalimbali nchini kote ili kukabiliana na machafuko.
Maoni yako