Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, waratibu wa mikusanyiko ya vuguvugu la Mavazi ya Njano nchini Ufaransa wametoa wito wa kufanyika duru ya pili ya maandamano tarehe 24 Oktoba. Wito huo umetolewa baada ya maandamano ya tarehe 17 Oktoba na wakati ambapo kutoridhika wananchi kutokana na gharama za maisha kunazidi kuongezeka, miongoni mwa madai yaliyotolewa ni Rais Macron kujiuzulu.
Waratibu wa mikusanyiko ya “Mavazi ya Njano ya tarehe 17 Oktoba”, ambao waliandaa maandamano ya Jumamosi iliyopita, wamechapisha wito unaowahimiza wananchi kushiriki katika siku nyingine ya maandamano itakayofanyika Jumamosi, tarehe 24 Oktoba. Harakati hii imetajwa kuwa “Duru ya Pili”, huku maandishi ya wito huo yakimtaka Rais wa Ufaransa ajiuzulu.
Waratibu hao pia wamechapisha ramani inayoonyesha maeneo yaliyopangwa kufanyika maandamano ya tarehe 24 Oktoba. Kwa sasa, ramani hiyo tayari inaonyesha shughuli kadhaa za maandamano, zikiwemo makumi ya mikusanyiko iliyopangwa kufanyika katika maeneo mbalimbali.
Kwa mujibu wa waandishi wa wito huo, tarehe 17 Oktoba, watu 800,000 walishiriki katika shughuli za maandamano zaidi ya 1,700 zilizofanyika kote nchini Ufaransa. Maandamano hayo yalifanyika katika maeneo mbalimbali, yakiwemo mizunguko ya barabarani, vituo vya mafuta, vituo vya kulipia ushuru wa barabara, maghala na viwanda vya kusafisha mafuta. Wito huo umetolewa kufuatia hotuba ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, iliyotolewa Jumapili, tarehe 18 Oktoba.
Kulaani Ukatili wa Polisi
Katika wito huo, inadaiwa kuwa kabla ya waandamanaji kuanza maandamano yao, gesi ya kutoa machozi ilitumika katika Uwanja wa Jamhuri mjini Paris. Aidha, huko Strasbourg, vikosi vya polisi vinadaiwa kuwashambulia waandamanaji waliokuwa wakifanya maandamano ya amani.
Waandishi wa wito huo pia wametaja matukio kadhaa ya majeraha mabaya yaliyodaiwa kusababishwa wakati wa maandamano, miongoni mwa matukio hayo ni mtu mmoja kukatwa mkono katika mji wa Saint-Étienne, mtu mwingine kupoteza jicho katika mji wa Mulhouse, kijana mwenye umri wa miaka 15 kukatwa mkono katika mji wa Lens, na mwanafunzi wa shule ya sekondari mwenye umri wa miaka 16 kupoteza uwezo wa kuona katika mji wa Tours.
Maandishi hayo pia yanaripoti kukamatwa watu zaidi ya 550 mjini Paris na katika vitongoji vinavyouzunguka. Waandishi wa wito huo wameeleza pia kuhusu kifo cha mmoja wa wanachama wa kikundi cha wahudumu wa huduma za dharura mitaani kinachojulikana kama “Street Medics”, ambaye inadaiwa alifariki kutokana na ukatili wa polisi.
Madai ya Waandamanaji
Waliotia saini wito huo wamewasilisha madai mbalimbali, miongoni mwa madai hayo ni kuheshimiwa haki ya kufanya maandamano, kukusanyika na kugoma, kulaaniwa ukatili wa polisi, kupigwa marufuku matumizi ya mabomu ya kutawanya waandamanaji kwa nguvu katika maeneo ya kuzingirwa, kukomeshwa ukamataji wa watu wengi na kuwekwa kizuizini kwa muda watu walio chini ya umri wa utu uzima; pamoja na kujiuzulu Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron. Pia wametaka “mfumo huu wa demokrasia ya uwakilishi ukomeshwe.”
Katika wito huo, waandishi wamehusisha marufuku ya mikusanyiko na hali ya hatari mamekumbusha kuwa sheria ya hali ya hatari nchini Ufaransa ilipitishwa tarehe 3 Aprili 1955. Sheria hiyo imetumika wakati wa vita vya Algeria, mwaka 2005, na baadaye kuanzia mwaka 2015 hadi 2017.
Historia ya Maandamano ya Tarehe 17 Oktoba
Siku ya Jumamosi, tarehe 17 Oktoba, ilikuwa siku ya uhamasishaji na maandamano ya kitaifa nchini Ufaransa dhidi ya “kupanda gharama za maisha.” Maandamano hayo yalihusu masuala mbalimbali, yakiwemo mfumuko wa bei, kupanda kwa kasi bei za mafuta na nishati, uwezo wa wananchi kumudu gharama za maisha na huduma za umma.
Siku hiyo, makundi mbalimbali yaliungana katika maandamano hayo. Makundi hayo yalijumuisha wanachama wa zamani wa vuguvugu la Mavazi ya Njano, wanafunzi wa shule za sekondari, vyama vya wafanyakazi—hasa Shirikisho Kuu la Wafanyakazi (CGT)—wanafunzi wa vyuo vikuu, wastaafu na wanaharakati wenye mielekeo mbalimbali. Vuguvugu la wanafunzi nalo limekuwa likiendelea tangu mwishoni mwa Septemba, huku likijikita zaidi katika masuala yanayohusu mazingira ya elimu.
Maandamano mengi yalifanyika bila mapigano. Hata hivyo, siku hiyo pia ilishuhudia vitendo vya vurugu, uporaji wa maduka, mapigano na mashambulizi dhidi ya majengo ya umma katika miji kadhaa ya Ufaransa, ikiwemo Paris, Marseille na Lyon.
Maoni yako