Jumatano 21 Oktoba 2026 - 11:20
Ufaransa Katika Hatihati ya Mlipuko wa Machafuko: Je, Jinamizi la Mei 1968 na Kuanguka Serikali Litajirudia?

Hawza/ Maandamano ya wanafunzi nchini Ufaransa, huku mapigano yakizidi kushika kasi na madai ya waandamanaji yakivuka mipaka ya masuala ya elimu, yamefufua kumbukumbu za vuguvugu la Mei 1968. Harakati hizo zilianza katika vyuo vikuu na, baada ya wafanyakazi kujiunga nazo, zikageuka kuwa mgogoro mpana katika nyanja za kijamii na kisiasa nchini Ufaransa. Sasa, wakati uchaguzi wa rais wa mwaka 2027 unapokaribia, swali linalojitokeza ni iwapo machafuko ya sasa yanaweza kusababisha mgogoro wa kisiasa na hata kuanguka serikali.

Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, mwandishi wa Morocco, Muhammad Adil al-Tatu, amechapisha ripoti inayochunguza kuenea maandamano ya wanafunzi nchini Ufaransa na uwezekano wa maandamano hayo kugeuka kuwa mgogoro wa kisiasa na kijamii.

Maandamano ya wanafunzi nchini Ufaransa yamefufua tena kumbukumbu za Mei 1968. Hasira za wanafunzi zimevuka mipaka ya shule na kuibua swali la iwapo mgogoro wa elimu unaweza kugeuka kuwa vuguvugu kubwa zaidi la kijamii na kisiasa, wakati ambapo Ufaransa inajiandaa kwa uchaguzi wa rais utakaofanyika katika majira ya kuchipua ya mwaka 2027.

Serikali ya Ufaransa inakabiliwa na mtihani mgumu katikati ya madai ya kuboreshwa elimu ya umma na kuongezeka mvutano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama. Kuenea maandamano na uwezekano wa makundi mengine ya kijamii kujiunga nayo kumeongeza wasiwasi kuhusu uwezekano wa harakati hizi kugeuka kuwa mgogoro mpana zaidi.

Katika muktadha huo, uchambuzi uliofanywa na Kituo cha Kiarabu cha Utafiti na Mafunzo ya Sera unaonesha kuwa maandamano ya wanafunzi ya mwezi huu wa Oktoba yanavuka mipaka ya madai ya kielimu. Aidha, yanaashiria kuongezeka ukosefu wa usawa wa kijamii na kupungua imani katika uwezo wa serikali wa kuhakikisha fursa zilizo sawa kwa wote.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wimbi la maandamano lilianza tarehe 5 Oktoba, na kufikia tarehe 6 Oktoba, idadi ya washiriki ilizidi watu 250,000, kulingana na makadirio ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa. Maandamano hayo yalianza kutokana na uhaba wa walimu, msongamano wa wanafunzi madarasani, hali isiyoridhisha ya baadhi ya shule na kupunguzwa matumizi ya serikali katika elimu ya umma. Hata hivyo, mikusanyiko ilipozidi kuenea na walimu, wafanyakazi wa shule, wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na vyama vya kitaaluma kujiunga nayo, wigo wa maandamano hayo ulivuka madai ya moja kwa moja yanayohusu elimu.

Mgogoro wa Elimu: Taswira ya Ukosefu wa Usawa wa Kijamii

Uchambuzi huu unahusisha maandamano hayo na mgogoro wa kiuchumi na kijamii uliokusanyika nchini Ufaransa katika miaka ya hivi karibuni. Athari za janga la COVID-19, vita kati ya Urusi na Ukraine, kupanda bei za nishati na mfumuko wa bei vimechangia kuzidisha mgogoro huo.

Kwa mtazamo wa kituo hicho, mgogoro wa elimu hauishii katika uhaba wa walimu au kushuka ubora wa ufundishaji pekee. Badala yake, unatia shaka pia uwezo wa shule za umma wa kuhakikisha fursa zilizo sawa kwa wanafunzi wote na kuwawezesha kupiga hatua katika maisha ya kijamii.

Familia zenye uwezo wa kifedha zinaweza kuwapatia watoto wao chaguo bora zaidi za kielimu, ilhali familia zenye kipato cha chini hutegemea zaidi shule za umma. Shule hizo zinakabiliwa na uhaba wa rasilimali na vifaa. Hali hii inaweza kuwanyima watoto wa familia hizo fursa za kujiunga na elimu ya juu na kupata ajira zenye nafasi nzuri katika soko la kazi.

Kwa mujibu wa uchambuzi huo, shule ambazo zinapaswa kupunguza tofauti za kijamii zinaweza, badala yake, kugeuka kuwa taasisi zinazozalisha upya ukosefu huohuo wa usawa.

Kutoka Katika Madai ya Elimu Hadi Maandamano ya Kisiasa

Kuenea kwa maandamano na utofauti wa washiriki wake kunaashiria kuongezeka kutoridhika miongoni mwa sehemu ya vijana. Hata hivyo, hali hiyo haimaanishi kwamba vuguvugu hilo lina mpango mmoja wa kisiasa unaowaunganisha washiriki wake wote.

Katika suala hili, Kituo cha Kiarabu cha Utafiti na Mafunzo ya Sera kinaelekeza kwenye maandamano ya Mei 1968, tukio lililoleta mabadiliko makubwa ya kijamii na kisiasa nchini Ufaransa. Hata hivyo, kukumbuka kipindi hicho hakumaanishi kwamba historia lazima ijirudie.

Mwelekeo wa baadaye wa maandamano ya sasa utategemea uwezo wa waandamanaji kuratibu madai yao, kuvutia makundi mengine ya kijamii na kudumisha uhuru wao dhidi ya ushindani wa vyama vya kisiasa.

Kadiri uchaguzi wa rais wa majira ya kuchipua ya mwaka 2027 unavyokaribia, umuhimu wa maandamano haya unazidi kuongezeka, hasa kwa sababu washiriki wengi bado hawajafikia umri unaoruhusiwa kisheria kupiga kura. Hata hivyo, vijana wanaweza kuathiri mijadala ya umma na kuzishinikiza zaidi vyama vya kisiasa pamoja na wagombea kuzingatia masuala kama vile elimu, haki ya kijamii na mustakabali wa kizazi kipya.

Bendera ya Palestina Katika Mikusanyiko ya Wanafunzi

Miongoni mwa mambo yanayovutia katika maandamano haya ni kwamba baadhi ya kaulimbiu zimevuka masuala ya elimu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika baadhi ya mikusanyiko, bendera ya Palestina na kaulimbiu zinazohusu mabadiliko ya tabianchi, vita na migogoro ya kimataifa zimeonekana. Jambo hili linaashiria kuwa sehemu ya vijana wa Ufaransa wanajali masuala ya haki na uadilifu yanayotokea nje ya mipaka ya nchi yao.

Hata hivyo, kuwepo kwa alama hizo hakumaanishi kwamba waandamanaji wote wana misimamo sawa ya kisiasa. Badala yake, kunaonyesha kuwa sehemu ya vijana wanayaona masuala yanayohusu maisha yao ya kila siku kuwa yanahusiana na mabadiliko ya kijamii na kisiasa yanayotokea duniani.

Operesheni za Usalama na Nafasi ya Mitandao ya Kijamii

Kusambazwa video zinazoonyesha mapigano kati ya wanafunzi na vikosi vya usalama kwenye mitandao ya kijamii kumeibua mijadala kuhusu namna polisi wanavyoingilia maandamano na mipaka ya matumizi ya nguvu. Kukamatwa kwa watu wengi pia kumezua maswali kuhusu iwapo hatua za kiusalama zina uwiano unaofaa na aina ya maandamano yanayofanyika, hasa ikizingatiwa kwamba sehemu kubwa ya washiriki bado hawajafikia umri unaotambuliwa kisheria kuwa mtu mzima.

Uchambuzi huu unaonya kuwa hatua kali za kukabiliana na waandamanaji zinaweza kupunguza idadi ya washiriki katika muda mfupi. Hata hivyo, wakati huohuo, zinaweza kuongeza hisia za kutendewa isivyo haki na kuimarisha mshikamano na waandamanaji.

Hali Tatu Zinazoweza Kujitokeza Katika Mustakabali wa Maandamano

Kituo cha Kiarabu cha Utafiti na Mafunzo ya Sera kinataja njia tatu zinazoweza kuchukuliwa na mwenendo huu:

Kwanza: Kudhibiti maandamano kupitia mwitikio wa kiasi wa serikali. Katika hali hii, serikali itajaribu kuzuia kuenea maandamano kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi katika sekta ya elimu na kuboresha hali ya shule. Hata hivyo, kujibu madai ya haraka hakutakuwa na uhakika wa kutatua matatizo ya kimuundo yaliyopo katika mfumo wa elimu.

Pili: Kuendelea maandamano ya hapa na pale, ikiwa serikali haitafanikiwa kudhibiti mgogoro kikamilifu na waandamanaji nao hawataweza kuunda vuguvugu lenye mshikamano na mpangilio thabiti, mikusanyiko inaweza kuendelea kujitokeza kwa vipindi tofauti na kuanza tena kila kunapotokea malalamiko mapya.

Tatu: Kupanuka vuguvugu na kugeuka kuwa mgogoro wa kijamii na kisiasa. Kujiunga vyama vya kitaaluma na makundi mengine ya kijamii, au kuongezeka mshikamano na wanafunzi kufuatia hatua za vikosi vya usalama, kunaweza kupanua wigo wa maandamano. Katika hali hiyo, harakati hizi zinaweza kuonesha baadhi ya sifa za vuguvugu la Mavazi ya Njano (Yellow Vests) la mwaka 2018, ambalo lilivuka madai yake ya awali na kuvutia makundi mengi zaidi ya kijamii.

Hatimaye, umuhimu wa maandamano ya wanafunzi nchini Ufaransa hauishii katika idadi ya washiriki au athari zake zinazoweza kujitokeza katika uchaguzi ujao. Suala kuu ni uwezo wa shule za umma kuhakikisha fursa zilizo sawa kwa kizazi kipya.

Mbali na kudhibiti machafuko yanayotokea mitaani, serikali ya Ufaransa inapaswa kuwahakikishia vijana kwamba mustakabali wao haujaamuliwa mapema kwa kutegemea mazingira yao ya kijamii na kifamilia.

Chanzo: Gazeti la Al-Omq la Morocco.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha