Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, sambamba na kumbukumbu ya mwaka wa kuuwawa kishahidi kwa Bibi Fatimah Zahra (s.a.), msafara wa maombolezo wa kila mwaka wa Fatimiyyah umefanyika katika mji mtakatifu wa Najaf Ashraf, kwa ushiriki wa Ayatullah Al-Udhma Hafidh Bashir Hussein Najafi. Shughuli hiyo ilihudhuriwa na kundi la wanazuoni, walimu, wanafunzi wa Hawza, waumini kutoka nchi mbalimbali za Kiislamu, mazuwari waliotoka katika mikoa mbalimbali ya Iraq, pamoja na baadhi ya masheikh wa makabila.
Msafara huo wa maombolezo ulianza katika ofisi ya Ayatullah Al-Udhma Bashir Najafi na kuelekea kwenye Haram Tukufu ya Amirul-Muuminin, Imam Ali (a.s.). Washiriki, katika mazingira yaliyojaa huzuni na majonzi, waliadhimisha kumbukumbu ya kuuwawa kishahidi Bibi Fatimah Zahra (s.a.), na kwa mara nyingine wakasisitiza mapenzi, Wilaya na uaminifu wao kwa Ahlul-Bayt (a.s.).
Ayatullah Al-Udhma Bashir Najafi, huku akisisitiza umuhimu wa kuendesha maombolezo ya Fatimiyyah, alieleza kuwa shughuli hii ni fursa ya kuifanya upya ahadi ya kushikamana na Ahlul-Bayt (a.s.) na kuonesha ufuasi kwenye dini ya kweli ya Mtukufu Muhammad (s.a.w.w.).
Vilevile, Hujjatul-Islam Sheikh Ali Najafi, mtoto wa mwanazuoni huyo mashuhuri wa kidini na mkurugenzi wa ofisi yake, katika hotuba yake alisema: “Msafara wa maombolezo ya Fatimiyyah ni kielelezo cha kutangaza kujitenga na dhuluma, ukosefu wa uadilifu na ugaidi, pia ni ishara ya kusimama imara katika njia ya haki na uadilifu, pamoja na fursa ya kuendeleza kumbukumbu ya dhuluma alizofanyiwa Bibi Fatimah Zahra (s.a.).”
Maoni yako