Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Shakir al-Tamimi, mbunge wa Iraq kutoka muungano wa Mfumo wa Uratibu (Al-Itar al-Tansiqi), jana Jumatatu, katika mahojiano, ametahadharisha kuhusu hatari ya kuendelea uingiliaji wa wazi wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iraq. Amesisitiza kwamba Washington, licha ya kutangaza kuondoa vikosi vyake vya kijeshi, bado inaendelea kutumia mamlaka yake ya kutawala na kuingilia hata maelezo madogo ya maamuzi ya kitaifa. Kwa mujibu wake, hali hiyo ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kujitawala ya Iraq na uhuru wake wa kikatiba.
Al-Tamimi amesema kuwa Marekani bado inaendelea kulazimisha ajenda zake na kujaribu kuathiri mwenendo wa kisiasa, kiusalama na kiuchumi wa Iraq. Amefafanua kwamba tangazo la kuondolewa kwa vikosi vya kijeshi vya Marekani halijakomesha juhudi za nchi hiyo na ubalozi wake mjini Baghdad za kutaka kutawala na kulazimisha matakwa yake.
Ameongeza kuwa mienendo na hatua hizo za Marekani ni ukiukaji wa mikataba yote ya kimataifa na taratibu za kidiplomasia, pamoja na kuwa ni uvunjaji wa moja kwa moja wa mamlaka ya kitaifa ya kujitawala. Amesema kuwa wananchi wa Iraq wametoa damu nyingi ili kulinda na kuhifadhi mamlaka hiyo dhidi ya utegemezi na kutekwa nyara maamuzi yao na mataifa ya kigeni.
Al-Tamimi ameitaka Serikali ya Shirikisho na taasisi zinazohusika kuchukua msimamo wa kitaifa wa ujasiri na thabiti, na kutokubali kwa namna yoyote ile kushindwa na shinikizo au maagizo ya Marekani. Amesisitiza umuhimu wa kusimama kidete dhidi ya uingiliaji huo na kukomesha hatua zenye mashaka za Washington, kwa lengo la kuimarisha mamlaka ya Serikali na uhuru wake wa kufanya maamuzi.
Katika muktadha huo, tovuti ya habari ya Uingereza ya Amwaj Media, ikimnukuu chanzo kimoja cha Serikali, imeripoti kwamba Baghdad imekataa ombi la Wizara ya Hazina ya Marekani la kufunga kabisa mipaka yote na Iran.
Vilevile, hatua ya hivi karibuni ya kufungwa mpaka wa Al-Shaib (Chadhabah) unachounganisha Iraq na Iran imezua hisia na radi amali mbalimbali katika Mkoa wa Maysan. Hussein al-Maryani, mmoja wa wajumbe wa Baraza la Mkoa wa Maysan, amesisitiza kwamba njia hiyo ilifungwa ghafla, bila ya kuufahamisha utawala wa mkoa. Ameeleza kuwa kabla ya kuchukua hatua za aina hiyo, mamlaka za mkoa zilipaswa kupewa taarifa.
Maoni yako