Jumanne 27 Oktoba 2026 - 16:00
Kufungwa Mpaka wa Al-Shaib Kumezorotesha Ajira na Kulemaza Shughuli za Biashara Mkoani Maysan

Hawza/ Jasim al-Alawi, akionya kuhusu madhara makubwa ya kiuchumi yanayotokana na uamuzi wa Serikali ya Iraq wa kufunga kituo cha mpaka wa Al-Shaib (Chadhabah) kinachounganisha Iraq na Iran, amesisitiza kuwa hatua hiyo imesababisha kudorora biashara na kuongezeka kiwango cha ukosefu wa ajira katika Mkoa wa Maysan, Aidha ametaka uamuzi huo ubatilishwe mara moja.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Jasim al-Alawi, mbunge wa Iraq, jana Jumatatu amesisitiza kwamba hatua ya Serikali ya Shirikisho la Iraq ya kufunga kituo cha mpaka waa Al-Shaib (Chadhabah) unachounganisha nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kumesababisha madhara makubwa ya kiuchumi na athari zisizoweza kurekebishwa katika shughuli za biashara na hali za maisha ya wananchi wa Mkoa wa Maysan.

Al-Alawi amesema kuwa hatua iliyochukuliwa na taasisi za Serikali ya kusimamisha shughuli na kufunga mpaka huo muhimu kumesababisha kudorora kiwango kikubwa cha biashara, kusimama mtiririko wa bidhaa na kusitishwa shughuli za maelfu ya wafanyakazi, madereva wa malori na watu wanaojishughulisha na kazi za kujitegemea. Ameeleza kuwa hali hiyo imeongeza kiwango cha ukosefu wa ajira na kuzidisha mzigo wa kiuchumi unaowakabili wakazi wa mkoa huo.

Ameongeza kuwa kituo cha mpaka wa Al-Shaib ni sehemu muhimu ya kiuchumi na kimkakati kwa Mkoa wa Maysan na mikoa jirani, amesema kuwa kuchukuliwa maamuzi ya ghafla na yasiyo na tahadhari ya kukifunga kituo hicho kunaathiri vibaya mapato na mzunguko wa shughuli katika soko la ndani. Mbali na hayo, hatua hizo zinatishia maisha ya kundi kubwa la watu wanaofanya kazi kwa bidii, ambao riziki zao zinategemea kikamilifu biashara inayofanyika kupitia mpaka huo.

Al-Alawi ameitaka Serikali na taasisi zinazohusika kufuta mara moja uamuzi wa kufunga mpaka huo na kuufungua tena, pia ameitaka Serikali kupanga upya usimamizi wake kwa namna itakayohakikisha kuwa shughuli za biashara zinaendelea kwa kuzingatia mifumo ya kisheria na taratibu za forodha, badala ya kutumia njia ya kufunga mpaka huo ambayo gharama zake kubwa zinabebwa na wananchi pamoja na uchumi wa mkoa huo.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha