Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, kwa mujibu wa Hani Mahmoud, mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Chuo Kikuu cha Kiislamu katika Jiji la Ghaza yamesababisha watu watatu kuuawwa kishahidi na wengine zaidi ya saba kujeruhiwa. Taarifa zinaeleza kuwa mashambulizi mawili ya anga yaliyofanywa na Israel dhidi ya wanafunzi na walinzi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu katika Jiji la Ghaza, ambacho kilikuwa kikiendelea na shughuli zake kwa idadi ndogo sana ya wafanyakazi, yalisababisha vifo vya watu hao.
Baada ya kushambuliwa kwa mabomu, Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Ghaza kilitangaza kusimamisha shughuli za kiutawala na kitaaluma katika kampasi yake iliyopo Jiji la Ghaza. Mwandishi wa habari wa Al Jazeera aliyekuwa katika eneo la tukio alieleza hali ilivyokuwa akisema kuwa; ndege isiyo na rubani ya Israel ililenga kundi la wanafunzi waliokuwa wamekusanyika ndani ya kampasi ya chuo hicho. Shambulizi hilo lilisababisha majeraha na hofu miongoni mwa wanafunzi pamoja na watu waliokuwa wamekimbia makazi yao na kupata hifadhi katika eneo hilo baada ya nyumba zao kuharibiwa wakati wa vita na mauaji ya kimbari yaliyofanywa na utawala katili wa Israel.
Harakati ya Hamas ililaani mashambulizi ya Israel dhidi ya kampasi ya Chuo Kikuu cha Kiislamu katika Jiji la Ghaza, huku ikiyataja kuwa ni “uhalifu wa kivita” usio wa kibinadamu. Aidha, Hamas iliwataka wapatanishi kuingilia kati mara moja ili kuishinikiza Israel kusitisha uhalifu wake unaoendelea dhidi ya raia.
Wizara ya Elimu na Elimu ya Juu ya Ghaza ilitangaza kwamba wanafunzi walikuwa wakiendelea na masomo yao madarasani wakati mashambulizi ya makombora yalipotokea. Baada ya mashambulizi ya anga, uongozi wa chuo kikuu ulitangaza kusimamisha shughuli za kitaaluma na kiutawala.
Shirika la Utangazaji la BBC liliripoti kwamba jeshi la utawala wa Israel liliiambia gazeti la The Times of Israel kuwa lilikuwa limelenga kile lilichokiita “watu wenye misimamo ya kigaidi”. Hata hivyo, vyanzo vya kitaaluma vilisisitiza kwamba watu watatu waliouawa walikuwa wafanyakazi wa chuo kikuu hicho pekee, na kwamba walikuwa raia wasiokuwa wanajeshi.
Chanzo: newscord.org
Maoni yako