Jumanne 27 Oktoba 2026 - 19:00
Iqbal Lahori Ameonesha Mapenzi na Upendo Wake kwa Bibi Fatima Zahra (s.a.) Kupitia Mashairi Mazuri

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sajid Ali Naqvi, katika ujumbe wake, ameuelezea mwenendo wa Bibi Fatima Zahra (s.a.) kuwa ni mfano wenye thamani kubwa katika kuhifadhi utu na haki za wanawake, pamoja na kueneza maadili mema katika jamii.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni wa Shia Pakistan, katika ujumbe wake kwa mnasaba wa siku za kukumbuka kuuwawa kishahidi binti wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w.), Bibi Fatima Zahra (s.a.), amesema kuwa; utu na hadhi tukufu ya Bibi Fatima Zahra (s.a.), kwa mtazamo wowote ule, vinamfanya kuwa mfano bora na shakhsia timilifu kwa wanawake wote duniani katika nafasi ya binti, mke na mama. Mwenendo wake, matendo yake na mafundisho yake ni nuru inayowaongoza wanawake katika kila zama.

Ameongeza kusema: Miongoni mwa majina na lakabu maarufu za Bibi Fatima Zahra (s.a.) ni Zahra, Batul, Sayyidatun-Nisaa, Tahira, Adhra, Muhadditha, Muadhdhama na Ummu Abiha. Kwa sababu yeye ni binti wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w.), shakhsia yake tukufu ni kitovu cha imani na heshima miongoni mwa Waislamu. Kwa upande mwingine, kutokana na matendo yake na mwenendo wake safi, atabaki kuwa mfano wa kipekee kwa wanawake wote duniani hadi Siku ya Kiyama.

Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Shia Pakistan, akirejelea mashairi ya Allamah Muhammad Iqbal Lahori, amesisitiza upendo na mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo mshairi huyo kwa Bibi Fatima Zahra (s.a.). Amesema kuwa Allamah Iqbal, akieleza utukufu na nafasi ya Bibi Fatima Zahra (s.a.), anasema katika mashairi yake:

مزرع تسلیم را حاصل بتول(سلام الله علیها)

مادران را اسوهٔ کامل بتول(سلام الله علیها)

Yaani; Bibi Fatima Zahra (s.a.) ndiye matunda na zao la shamba la kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu na kuridhia mapenzi Yake, na pia ni mfano kamili kwa akina mama wote.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sajid Ali Naqvi, katika sehemu inayofuata ya ujumbe wake, amesema kwamba; Allamah Iqbal alivutiwa mno na utukufu wa Bibi Fatima Zahra (s.a.) kiasi kwamba, kupitia maneno yake, alimpatia heshima na mapenzi ya hali ya juu kabisa. Katika mashairi yake, Iqbal anajiona kuwa na wajibu wa kulinda Sheria ya haki na kutekeleza amri za Mtume Mtukufu (s.a.w.w.), na kupitia hilo anaueleza upendo wake kwa Bibi wa ulimwengu. Anasema:

رشتهٔ آئین حق زنجیر پاست

پاس فرمان جناب مصطفی است

ورنه گرد تربتش گردیدمی

سجده‌ها بر خاک او پاشیدمی

Yeye anasema: Kushikamana na dini ya haki ni kama mnyororo uliofungwa miguuni mwangu, na wajibu wangu ni kulinda na kuhifadhi amri za Mtume (s.a.w.w.). La sivyo, kama kusingekuwa na kizuizi hicho, ningezunguka kuzunguka kaburi lake na kusujudu mara nyingi juu ya udongo wa kaburi hilo.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sajid Ali Naqvi, katika ujumbe wake, akizungumzia changamoto za kimawazo na kijamii zinazowakabili wanawake katika zama hizi, amebainisha kwamba: Kwa sasa, wanawake wanakabiliwa na mkanganyiko wa kimawazo na chini ya kaulimbiu za maendeleo na usasa, wanakumbana na matatizo ya unyonyaji wa wanawake katika jamii mbalimbali, hususan katika jamii za Magharibi.

Katika mazingira kama haya, mwenendo na matendo ya Bibi Fatima Zahra (s.a.) vinatoa kanuni muhimu za mwongozo kwa wanawake, ili waweze kujilinda dhidi ya upotovu wa kimawazo, unyonyaji na kudorora maadili.

Kuhusu uhuru wa wanawake, jamii mbalimbali zimeweka kanuni na mipaka yake. Hata hivyo, kwa mujibu wa mtazamo huo, dhana ya uhuru inapaswa kuhusishwa na uzingatiaji wa tabia njema, masharti ya kisheria na uhifadhi wa utu wa mwanadamu. Kulinda heshima na hadhi ya wanawake, pamoja na kueneza maadili katika jamii, ni jambo lenye umuhimu wa msingi kabisa.

Wanawake Waislamu wanapaswa kuiga mwenendo wa Bibi Fatima Zahra (s.a.) na kujitahidi kuhifadhi haki zao, heshima yao, staha yao na nafasi yao katika jamii. Alilelewa katika nyumba ya Utume, na maisha yake ni kielelezo dhahiri cha imani, uchamungu, elimu, subira, kujisitiri na kulinda usafi wa maadili, kuwajibika katika masuala ya familia na kusimama imara katika upande wa haki.

Wanawake wanapaswa kuuweka mbele ya macho yao mwenendo wa Bibi Fatima Zahra (s.a.) katika hatua zote za maisha yao, kuanzia masuala binafsi na ya kifamilia hadi mambo ya kijamii. Kwa kuiga mafundisho yake na matendo yake ya kivitendo, itawezekana kulea vizazi vyema ambavyo vitakuwa na nafasi yenye matokeo katika kueneza maadili na kuijenga jamii bora zaidi, yenye staha na iliyo na uwiano.

Mwishoni, amesisitiza kwamba: Kumuenzi Bibi Fatima Zahra (s.a.) na kuhuisha ujumbe wake hakupaswi kuishia katika kudhihirisha imani na upendo kwake pekee. Bali, jambo hilo linapaswa kujidhihirisha kwa kufuata kwa vitendo njia ya matendo mema, mwenendo wake na mafundisho yake matukufu katika maisha ya kila siku.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha