Shirika la Habari la Hawza - Wakati inaposemwa katika hesabu za kidini, za Mwenyezi Mungu na za Qur'ani kwamba Iran ndiyo nguvu ya kwanza duniani, dai hili linategemea vigezo na vipengele gani?
Naibu wa Masuala ya Kimataifa wa Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kuhsari, alisema kuwa katika uchunguzi wake amefikia mihimili saba. Aliongeza: “Ninataka kulinganisha vigezo hivi na hali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya leo, na kuchunguza iwapo vipengele hivi vinapatikana katika hali ya sasa ya nchi, na iwapo matokeo ya jumla ya vipengele hivyo yanatufikisha kwenye hitimisho kwamba Iran, kwa kuzingatia vigezo vya kidini na vya Qur'ani, ndiyo nguvu ya kwanza katika medani ya kimataifa au la.”
Kigezo cha Kwanza: Mwendelezo wa Wilaya ya Mwenyezi Mungu na Utawala wa Kidini
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kuhsari alikitaja kigezo cha kwanza cha nguvu kuwa ni mfumo wa utawala kuwa katika mwendelezo wa wilaya ya Mwenyezi Mungu na kutekeleza utawala wa Mwenyezi Mungu alisema: “Miongoni mwa vigezo vya hesabu za kidini na za Qur'ani ni kuchunguza ni kwa kiwango gani nchi imejipanga katika mwendelezo wa wilaya na utawala wa Mwenyezi Mungu.”
Akizungumzia ngazi mbalimbali za wilaya kwa mtazamo wa kidini, aliongeza: “Katika aya za Qur'ani, wilaya ya Mwenyezi Mungu inaendelea kupitia wilaya ya Manabii wa Mwenyezi Mungu. Wilaya ya Manabii wa Mwenyezi Mungu inaunganishwa na wilaya ya Maimamu Maasumu (a.s.), na njia hii inaendelea kupitia wilaya ya waja wema wa Mwenyezi Mungu.”
Mwanazuoni huyo wa Hawza, akizungumzia nadharia ya Wilayat al-Faqih katika maandiko ya kidini na ya kimapinduzi, alifafanua: “Nadharia ya Wilayat al-Faqih imewasilishwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa muundo huu, na inahesabiwa kuwa mojawapo ya dhihirisho na vipengele vya nguvu inayotokana na Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu katika mfumo huu, utawala unafafanuliwa kwa kuzingatia wilaya ya Ahlul-Bayt (a.s.) na wilaya ya Manabii wa Mwenyezi Mungu.”
Akisisitiza kwamba kigezo hiki kinapaswa kuchunguzwa ndani ya mfumo wa misingi ya kiitikadi na ya Qur'ani, alisema: “Kwa mtazamo wangu, kwa kuzingatia kipengele hiki, tunaweza kuitathmini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa katika nafasi ya pekee miongoni mwa nchi za dunia, kwa sababu mfumo wake wa utawala umejengwa kwa msingi wa nadharia ya Wilayat al-Faqih na mwendelezo wa wilaya ya Mwenyezi Mungu.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Husayni Kuhsari aliendelea kuchambua mwelekeo wa uongozi ndani ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kuzingatia mfumo huo. Akimtaja Imam Khomeini (r.a.), Kiongozi aliyeuawa kishahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kiongozi wa sasa, Ayatullah Sayyid Mujtaba Husayni Khamenei, aliuzungumzia mwelekeo huo kwa mtazamo wa mwendelezo wa wilaya ya Mwenyezi Mungu.
Alikitaja kipengele hiki kuwa ndicho kigezo cha kwanza katika kutathmini nafasi ya Iran kwa mujibu wa hesabu za nguvu zinazotokana na Qur'ani. Alisisitiza kwamba ili kuelewa nguvu kwa mtazamo wa dini, ni lazima pia kuzingatia misingi na muundo wa utawala pamoja na vigezo vingine.
Kigezo cha Pili: Kusimama Imara Dhidi ya Madhalimu na Mifumo ya Utawala wa Kijahili, Pamoja na Kupata Msaada wa Mwenyezi Mungu
Naibu wa Masuala ya Kimataifa wa Hawza alikitaja kigezo cha pili kuwa ni kusimama imara dhidi ya madhalimu na mifumo ya utawala inayotumia nguvu kuwatawala wengine. Alisema: “Katika mfumo wa hesabu za Mwenyezi Mungu, nguvu inayosimama dhidi ya madhalimu wakubwa na mikondo mikuu ya uovu na uonevu, kwa mtazamo wa Qur'ani, huwekwa katika nafasi ambayo suala la kupata msaada wa Mwenyezi Mungu na kuungwa mkono na kanuni za Mwenyezi Mungu huhusishwa nayo.”
Akizungumzia mikondo miwili ya wilaya ya Mwenyezi Mungu na wilaya ya Shetani katika mfumo wa Qur'ani, alisema: “Kama ambavyo Qur'ani inazungumzia wilaya ya Mwenyezi Mungu, wilaya ya Manabii wa Mwenyezi Mungu, wilaya ya Maimamu Maasumu (a.s.) na wilaya ya waja wema wa Mwenyezi Mungu, upande mwingine pia kuna mfumo wa wilaya ya Shetani, wilaya ya madhalimu na mikondo inayopinga haki.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Husayni Kuhsari, akikitumia kigezo hiki katika kuchambua hali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alisema: “Tunapochunguza hali ya dunia, tunaona kwamba kuna uadui na chuki kubwa dhidi ya serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”
Akizungumzia utawala wa Kizayuni, Uzayuni wa kimataifa, Marekani na kile alichokieleza kuwa ni uadui wa kina zaidi wa baadhi ya sehemu za ustaarabu wa Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, alisema: “Kwa mtazamo wa uchambuzi wa Qur'ani unaojadiliwa hapa, mapambano haya ni miongoni mwa vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa katika kutathmini nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu.”
Mwanazuoni huyo wa Hawza alisisitiza msingi wa uchambuzi wake na kuongeza: “Kadiri, kwa mujibu wa mfumo huu wa hesabu, ukweli na uhalali wa msimamo wa mkondo fulani unavyokuwa mkubwa zaidi, na madhalimu pamoja na nguvu zinazotawala wengine zinavyokuwa na uadui mkubwa zaidi dhidi yake, ndivyo suala la mkondo huo kunufaika na msaada wa Mwenyezi Mungu na kuungwa mkono na majeshi ya Mwenyezi Mungu linavyojitokeza ndani ya mfumo huu.”
Naibu wa Masuala ya Kimataifa wa Hawza alifafanua kwamba; kusimama imara dhidi ya mikondo inayotawala wengine na uhusiano wa msimamo huo na msaada wa Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa vipengele vya kutathmini nguvu kwa mtazamo wa Qur'ani, na kwamba vinapaswa kuchunguzwa pamoja na vigezo vingine.
Kigezo cha Tatu: Uhusiano Kati ya Imam na Umma, na Kiwango cha Wananchi Kumuunga Mkono Kiongozi
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kuhsari alikitaja kigezo cha tatu cha nguvu inayotokana na Mwenyezi Mungu kuwa ni uhusiano kati ya Imam na umma, pamoja na kiwango cha wananchi kumuunga mkono wali wa Mwenyezi Mungu, Nabii wa Mwenyezi Mungu na waja wema wa Mwenyezi Mungu.
Alisema: “Kwa mtazamo wa Qur'ani, miongoni mwa vigezo muhimu vya nguvu ni kiwango ambacho wananchi wanashirikiana na walii wa Mwenyezi Mungu, Nabii wa Mwenyezi Mungu na waja Wake wema.”
Ili kufafanua suala hili, mwanazuoni huyo wa Hawza alirejelea kisa cha Nabii Musa (a.s.) na watu wa Bani Israil, alisema: “Katika Qur'ani, watu wa Bani Israil wanalaumiwa kwa kutomuunga mkono Nabii Musa (a.s.). Walipojibu wito wa Nabii wao, walisema:
«فَاذْهَبْ أَنْتَ وَرَبُّکَ فَقَاتِلَا إِنَّا هَاهُنَا قَاعِدُونَ»
“Basi nenda wewe na Mola wako, mkapigane; hakika sisi tumekaa hapa.”
Naibu wa Masuala ya Kimataifa wa Hawza, akitumia mfano huu wa Qur'ani, alitaja uungwaji mkono wa wananchi kwa uongozi wa Mwenyezi Mungu kuwa ni mojawapo ya vigezo muhimu vya nguvu. Aliongeza kwamba kile tunachoweza kukitaja leo kuwa ni ushiriki na uungwaji mkono wa wananchi kwa wingi, kinapata umuhimu ndani ya mfumo huu.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kuhsari, akikitumia kigezo hiki katika kuchambua hali ya Iran, alisema: “Ikiwa tunataka kuitazama hali hii kwa mtazamo huo, tunapaswa kuzingatia kiwango cha wananchi wa Iran kumuunga mkono walii wa Mwenyezi Mungu, umoja wao, mshikamano wao, mwendelezo wa uhusiano wao na utii wao kwa wilaya.”
Akizungumzia imani ya Mashia kuhusu ghaiba ya Imam wa Zama (a.j.) na nafasi ya Wali al-Faqih kama naibu wa Imam, alisema: “Kwa mtazamo huu, wananchi wanafuata uongozi ambao wengi wao hawajawahi kukutana moja kwa moja na Imam, na kimsingi hawajawahi kumwona Imam wao. Hata hivyo, ufuasi wao na uhusiano wao wa kiitikadi hujengwa ndani ya mfumo wa imani ya wilaya na uwakilishi wa Imam.”
Mwanazuoni huyo wa Hawza, akizungumzia pia uungwaji mkono wa wananchi katika nchi nyingine, alisema: “Nchini Iraq, Lebanon, Pakistan na Yemen pia kuna harakati na uungwaji mkono unaoonekana. Hata hivyo, harakati hizi zinaunganishwa na mkondo wa wilaya na mfumo ulioanzishwa ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”
Akizungumzia ushiriki mkubwa wa wananchi wa Iraq katika shughuli za mazishi ya mwili wa Kiongozi aliyeuawa kishahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alitaja idadi ya takribani watu milioni 11. Alitaja ushiriki huo kuwa ni miongoni mwa mifano aliyozingatia katika kuchunguza uhusiano wa kiitikadi na kijamii.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Husayni Kuhsari aliongeza: “Nchini Lebanon pia kuna aina fulani ya harakati na uungwaji mkono unaoonekana. Vilevile, nchini Iraq, Pakistan na Yemen, wananchi wanashiriki katika matukio na harakati mbalimbali. Hata hivyo, mabadiliko haya yanachambuliwa ndani ya mfumo wa uhusiano kati ya Imam na umma, pamoja na uhusiano wake na wilaya.”
Alisisitiza: “Tunapokiweka kigezo hiki pamoja na vipengele vingine, mshikamano wa kijamii, utii kwa wilaya na uhusiano endelevu kati ya wananchi na uongozi huwa miongoni mwa vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa katika kutathmini nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”
Kigezo cha Nne: Misingi ya Kiakili, Maarifa na Uwezo wa Kifikra wa Kuunda Mwelekeo wa Kifikra
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kuhsari alikitaja kigezo cha nne cha nguvu kuwa ni misingi ya kiakili ya maarifa na ya kifikra ya nchi, slisema: “Miongoni mwa mihimili muhimu katika kuchunguza nguvu ni kuangalia nchi inaungwa mkono na misingi gani ya kiakili, maarifa, kifalsafa na kifikra.”
Akizungumzia uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maarifa ya Ahlul-Bayt (a.s.) pamoja na mafundisho ya mawalii wa Mwenyezi Mungu, aliongeza: “Kwa baraka ya uhusiano huu, tunacho kiwango fulani cha maarifa, fikra, falsafa, irfani na hekima ambacho kinaweza kuzingatiwa kwa mtazamo wa kigezo hiki.”
Mwanazuoni huyo wa Hawza alisema: “Kwa mtazamo huu, tunaweza kutumia hazina hii ya kiakili na maarifa tuliyonayo kuzingatia uwezo wetu wa kifikra na kuuchukulia kuwa ni miongoni mwa vipengele vya nguvu.”
Naibu wa Masuala ya Kimataifa wa Hawza, akisisitiza kwamba maarifa haya hayawahusu Wairani pekee, alisema: “Uwezo huu, kutokana na uhusiano wake na maarifa ya Ahlul-Bayt (a.s.), Maimamu Maasumu (a.s.) na Mtume Mtukufu wa Uislamu (s.a.w.w.), hauzuiliwi na mipaka ya Iran, bali unaweza kuzingatiwa katika medani pana zaidi ya mipaka ya nchi.”
Katika kufafanua vipengele vya nguvu hii ya kifikra, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kuhsari aliashiria Uislamu halisi, Uislamu jumuishi, Uislamu wa kistaarabu, madhehebu ya Ashura, Uislamu wa kimapinduzi na fikra za Muqawama, alisema kwamba mkusanyiko huu ni miongoni mwa hazina za kiakili na maarifa zinazoiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Aliongeza kwamba misingi hii, mbali na upande wake wa kiitikadi, ina umuhimu pia katika uundaji wa nadharia na kujenga mwelekeo maalumu wa kifikra. Kwa hiyo, inapaswa kuzingatiwa katika ulinganisho kati ya nchi mbalimbali.
Mwanazuoni huyo wa Hawza, akiitaja China kuwa ni mojawapo ya nguvu za kiuchumi na kisiasa duniani, alisema: “China ina nguvu za kiuchumi na kisiasa, lakini kwa upande wa nguvu ya kifikra, maarifa na uwezo wa kuunda nadharia, si lazima tuweze kuhusisha nayo sifa hizo hizo.”
Pia alizungumzia ustaarabu wa Magharibi na kusema: “Katika kipindi fulani, ustaarabu wa Magharibi ulidai kuwa na hazina kubwa ya ustaarabu. Hata hivyo, leo unakabiliwa na migogoro katika nyanja za kiakili na maarifa. Kwa mtazamo huu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kutokana na misingi yake ya Kiislamu na fikra zake, iko katika nafasi inayostahili kuzingatiwa.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kuhsari alikitaja kipengele hiki kuwa ni mojawapo ya vigezo muhimu vya nguvu. Alisisitiza kwamba katika hesabu za Qur'ani, nguvu haipaswi kupimwa kwa vigezo vya kiuchumi, kisiasa au kijeshi pekee, bali misingi ya maarifa na fikra pia inapaswa kuzingatiwa katika kutathmini nafasi ya nchi mbalimbali.
Kigezo cha Tano: Mshikamano, Kusaidiana, Kujitolea na Kujinyima kwa Ajili ya Wengine
Naibu wa Masuala ya Kimataifa wa Hawza alikitaja kigezo cha tano cha nguvu kuwa ni kiwango cha mshikamano, kusaidiana, kujitolea na kujinyima kwa ajili ya wengine katika jamii.
Alisema: “Miongoni mwa dhihirisho la nguvu inayotokana na Mwenyezi Mungu ni kuenea hisia za mshikamano na utayari wa kujitoa mhanga miongoni mwa wananchi.” Akizungumzia kampeni ya Jan-Fada (Kujitoa kwa Ajili ya Wengine), alisema: “Leo tunakabiliwa na hali ambayo watu wengi wanatangaza utayari wao wa kujitoa mhanga na kujinyima kwa ajili ya wengine.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kuhsari, akizungumzia mashahidi katika nyanja mbalimbali, aliongeza: “Katika sehemu mbalimbali za jamii yetu tuna mashahidi wa utumishi, mashahidi wa afya, mashahidi wa usalama na mashahidi katika nyanja ya elimu na malezi. Mifano hii inaonyesha kwamba kujitolea na kujitoa mhanga kunaweza kujitokeza miongoni mwa makundi na matabaka mbalimbali ya jamii.”
Alisema: “Jambo muhimu ni kuhakikisha kwamba hisia ya kuwajibika na utayari wa kujitoa mhanga haviishii katika tabaka fulani tu, bali katika ngazi ya taifa, roho ya kujitolea na kujinyima kwa ajili ya wengine inaenea katika jamii.”
Mwanazuoni huyo wa Hawza, akirejelea aya isemayo:
«إِنْ تَنْصُرُوا اللَّهَ يَنْصُرْكُمْ»
“Ikiwa mtamnusuru Mwenyezi Mungu, Atakunusuruni,”
Alisisitiza kwamba; katika mantiki ya Qur'ani, msaada wa Mwenyezi Mungu unahusiana na kuinusuru dini Yake na watu kujitokeza katika njia ya haki. Kwa hiyo, kujitolea na kujitoa mhanga pia ni miongoni mwa vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa katika kutathmini nguvu kwa mtazamo wa Qur'ani.
Naibu wa Masuala ya Kimataifa wa Hawza alitaja kiwango hiki cha utayari wa kujitoa mhanga kuwa ni mojawapo ya vipengele ambavyo vikichunguzwa pamoja na vigezo vingine, vinaweza kutumika katika kuchambua nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kigezo cha Sita: Subira, Ustahimilivu na Uwezo wa Taifa Kuvumilia Shinikizo
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kuhsari alikitaja kigezo cha sita cha nguvu kuwa ni subira, ustahimilivu na uwezo wa taifa kuvumilia shinikizo na matatizo.
Alisema: “Kwa mtazamo wa Qur'ani, ikiwa taifa lina sifa ya ustahimilivu, uimara huo unaweza kuwa sababu ya kupokea msaada wa Mwenyezi Mungu.”
Akisisitiza umuhimu wa kudumu imara katika njia ya malengo na maadili, aliongeza: “Subira na uwezo wa kuvumilia shinikizo ni miongoni mwa vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa katika hesabu za nguvu kwa mtazamo wa kidini. Hii ni kwa sababu tathmini ya nafasi ya taifa haiishii tu katika hali yake ya muda mfupi, bali kiwango cha uimara wake mbele ya matatizo pia kina umuhimu.”
Mwanazuoni huyo wa Hawza alifafanua: “Wakati taifa linapokuwa na ustahimilivu na uwezo wa kuvumilia shinikizo pamoja na vipengele vingine, sifa hii inaweza kuwa na nafasi katika kuchambua nguvu ya taifa hilo kwa mujibu wa mfumo wa hesabu za Qur'ani.”
Naibu wa Masuala ya Kimataifa wa Hawza aliitaja subira na ustahimilivu, pamoja na kiutii wilaya, nguvu ya kifikra, kujitolea na kujitoa mhanga, kuwa ni mihimili inayopaswa kuchunguzwa kwa pamoja badala ya kuitazama kila mmoja kivyake.
Kigezo cha Saba: Umoja na Mshikamano wa Pande Zote
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kuhsari alikitaja kigezo cha saba cha nguvu kuwa ni umoja na mshikamano wa pande zote. Akirejelea aya ya Qur'ani Tukufu isemayo:
«وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ»
“Wala msizozane, msije mkashindwa na nguvu zenu zikaondoka,”
Alisema kwamba Qur'ani inaonya waziwazi kuwa tofauti na migogoro vinaweza kusababisha kushindwa na kupoteza nguvu na uwezo.
Aliongeza: “Ikiwa jamii itakumbwa na mgawanyiko na kuacha umoja wake, nguvu na heshima yake vitapungua. Kwa hiyo, umoja ni mojawapo ya vigezo muhimu vya nguvu katika hesabu za Qur'ani.”
Mwanazuoni huyo wa Hawza, akikitumia kigezo hiki katika kuchambua hali ya Iran, alisema: “Leo umoja na mshikamano kati ya wananchi, viongozi na uongozi mkuu viko katika hali inayostahili kuzingatiwa, na suala hili linapaswa kuchunguzwa pamoja na vipengele vingine.”
Akizungumzia uhusiano kati ya makundi na mikondo mbalimbali, viongozi wao kwa wao, wananchi na viongozi, pamoja na wananchi na viongozi kwa upande mmoja na uongozi mkuu kwa upande mwingine, alisema: “Kiwango hiki cha uhusiano na mshikamano kinaweza kutathminiwa kwa kuzingatia kigezo cha umoja.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kuhsari, hata hivyo, alifafanua kwamba: “Lengo si kukana kuwepo kwa tofauti zote au hali za kipekee, bali ni kuzingatia matokeo ya jumla ya hali ilivyo.”
Naibu wa Masuala ya Kimataifa wa Hawza aliongeza: “Tukiitazama hali ya jamii kwa mtazamo wa kigezo cha umoja, tunaweza kuzungumzia kiwango cha mshikamano kati ya wananchi, viongozi na uongozi mkuu, na kukichukulia kuwa ni mojawapo ya vipengele muhimu vya nguvu.”
Uwezo wa Kijeshi, Silaha na Sayansi: Vipengele vya Ziada vya Nguvu
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Husayni Kuhsari aliendelea kuzungumzia nafasi ya majeshi na uwezo wa kijeshi, silaha na sayansi, akivitaja vipengele hivi kuwa ni miongoni mwa nyanja nyingine za nguvu.
Alisema: “Ili kuwa na nguvu, uwezo mbalimbali una umuhimu, ukiwemo uwezo wa kijeshi, wa silaha na wa kisayansi. Vipengele hivi pia vinapaswa kuzingatiwa katika kutathmini nafasi ya nchi.”
Mwanazuoni huyo wa Hawza, huku akisisitiza umuhimu wa kuchunguza mkusanyiko wa vigezo, aliongeza: “Tunapozungumzia mfumo wa hesabu za Mwenyezi Mungu, za kidini na za Qur'ani, tunapaswa kuzingatia mkusanyiko wa mambo yanayoweza kuwa na nafasi katika kujenga nguvu na kupata msaada wa Mwenyezi Mungu.”
Naibu wa Masuala ya Kimataifa wa Hawza alifafanua: “Haiwezekani kutathmini nguvu kwa kutumia kigezo kimoja pekee. Ni lazima uwezo wa kijeshi na wa kisayansi uchunguzwe pamoja na vigezo kama vile wilaya ya Mwenyezi Mungu, uungwaji mkono wa wananchi, misingi ya maarifa, kujitolea, ustahimilivu na umoja.”
Matokeo ya Jumla ya Vigezo vya Qur'ani: Msingi wa Uchambuzi wa Iran Kuwa Nguvu ya Kwanza Duniani
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kuhsari, akihitimisha maelezo yake, alisema: “Tukiweka vigezo hivi pamoja, inawezekana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikawa katika nafasi ya kwanza katika baadhi yake na ikawa na nafasi ya kipekee katika vingine. Hata hivyo, jambo lenye umuhimu ni matokeo ya jumla ya vipengele vyote hivi.”
Akizungumzia mfumo wa kiakili na maarifa, muundo wa kisiasa, mshikamano na umoja, hazina ya kifikra inayotokana na Uislamu halisi na Uislamu wa kistaarabu, kujitolea na kujitoa mhanga, pamoja na subira na uwezo wa kuvumilia shinikizo, alisema: “Tunapoviweka vipengele hivi vyote pamoja, tunaweza kufikia hitimisho kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa mujibu wa hesabu za kidini na za Qur'ani, ndiyo nguvu ya kwanza katika medani ya kimataifa.”
Mwanazuoni huyo wa Hawza, akizungumzia tofauti kati ya mifumo ya kutathmini nguvu, alisema: “Inawezekana baadhi ya mifumo ya tathmini ya nguvu isivijumuishe vigezo hivi katika vipimo vyake, na badala yake ipange nafasi za nchi kwa kuzingatia vipengele vingine. Hata hivyo, ikiwa vigezo vya Qur'ani na vya kidini ndivyo vinavyowekwa kuwa msingi, nafasi za nchi zinapaswa kupimwa kwa kutumia vigezo hivyo hivyo.”
Katika muktadha huo, alirejelea kauli ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi kuhusu nafasi ya Iran na kuongeza: “Inawezekana kwamba katika baadhi ya mifumo ya hesabu, Iran ikawekwa katika nafasi ya nne kwa upande wa nguvu. Lakini tukiweka pamoja vigezo vya kidini na vya Qur'ani na kulinganisha hali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na vigezo hivyo, tutafikia matokeo tofauti.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kuhsari, akizungumzia hali ya Iran baada ya kuuawa kkshahidi Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alisema: “Katika baadhi ya nyanja hizi, nafasi ya Iran imekuwa dhahiri na yenye kujitokeza zaidi baada ya tukio hilo, Jambo hili pia linapaswa kuzingatiwa katika kuchunguza hali ya sasa ya nchi.”
Naibu wa Masuala ya Kimataifa wa Hawza za Elimu za Kidini alisisitiza: “Tukiweka vigezo hivi pamoja na kufanya tathmini kwa kuzingatia misingi ya Qur'ani na ya kidini, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itakuwa katika nafasi ya kwanza ya nguvu katika medani ya kimataifa, kwa mtazamo wa mfumo huu wa kimahesabu.”
Maoni yako