Jumapili 11 Oktoba 2026 - 17:50
Kundi la Muqawama Lebanon Laitaka Serikali Ichukue Hatua za Kukabiliana na Israel

Hawza/ Kundi la Uaminifu kwa Muqawama katika Bunge la Lebanon limeitaka serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua za vitendo ili kupunguza athari za mashambulizi ya Israel.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Kundi la Uaminifu kwa Muqawama katika Bunge la Wawakilishi la Lebanon, katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano wake wa kawaida na kusomwa na Mbunge Hassan Izzuddin, lilisisitiza kuwa serikali ya Lebanon inapaswa kutekeleza wajibu wake wa msingi kwa wananchi. Aidha, liliitaka serikali ianze kuchukua hatua za kivitendo, kwa kutumia njia na nyenzo zote zinazowezekana ili kupunguza athari za mashambulizi ya Israel kwa wananchi.

Kundi hilo, huku likisisitiza kuwa msimamo wa Hizbullah wa kuiunga mkono familia na wananchi wake pamoja na kuwasaidia utaendelea kuwa thabiti, lilieleza kuwa Hizbullah itaendelea kufanya juhudi zake zote katika suala hilo. Aidha, lilifichua kuwa Hizbullah ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kutekeleza hatua mpya inayolenga kuendeleza misaada ya makazi kwa wananchi waliolazimika kuyahama makazi yao.

Vilevile, Kundi la Muqawama lilieleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu kuzorota hali ya maisha na mazingira ya kijamii ya wananchi wengi wa Lebanon. Lilihusisha hali hiyo na kuenea ufisadi, mlipuko wa bei kwa kiwango kikubwa, kukatika umeme, pamoja na mzigo mzito wa kiuchumi unaowakabili wananchi.

Kutokana na hali hiyo, kundi hilo liliitaka serikali na taasisi za kiserikali kuchukua “maamuzi na hatua madhubuti” za kupambana na aina mbalimbali za ufisadi na ukwepaji wa kodi, pamoja na kuimarisha mapato ya serikali. Lengo la hatua hizo ni kuwezesha utoaji wa vifurushi vya msaada, misaada mbalimbali na punguzo la kodi ili kupunguza athari za mgogoro, hususan kwa wananchi wenye kipato kidogo.

Kuhusu suala la Palestina, kundi hilo lililaani mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Aidha, kundi hilo liliwapongeza wananchi wa Iraq wanaosimama imara katika kukabiliana na changamoto, Marji' wao mwenye busara, vikosi vyao vinavyopigania maslahi ya taifa, pamoja na vikosi vya kishujaa vya Uhamasishaji wa Umma (Hashd al-Shaabi), kwa mnasaba wa kuondoka vikosi vya Marekani nchini Iraq.

Kuhusu Yemen, kundi hilo lililaani kuendelea mzingiro na kurejeshwa vita vilivyolazimishwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen na wananchi wake, hususan katika mji wa Sana'a, Sa'dah na maeneo mengine. Lilitoa wito wa kusitishwa mara moja vita hivyo na kuondolewa mzingiro dhidi ya Yemen, kwa lengo la “kuzuia umwagaji wa damu na kulinda maisha ya binadamu.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha