Jumapili 11 Oktoba 2026 - 16:20
Yemen Iko Tayari Kujilinda; Hatutaki Vita, Lakini Tutapinga Uchokozi

Hawza/ Abdulwahid Abu Ras, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Wahamiaji wa Yemen, ameitaka Saudi Arabia kusitisha vikwazo na mzingiro dhidi ya Yemen, huku akisisitiza kuwa wananchi wa Yemen wanapigania kupata haki zao za msingi, za kitaifa na za kisheria, na kwamba hawatakubali kufanya maafikiano yoyote kuhusu mamlaka ya nchi yao na uhuru wake.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Abdulwahid Abu Ras, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Wahamiaji wa Yemen, katika mahojiano maalumu, alieleza msimamo wa Yemen kuhusu hali ya sasa ya nchi hiyo, mvutano na Saudi Arabia, suala la Palestina, makabiliano na Israel pamoja na Marekani, na pia nafasi inayoweza kutekelezwa na Pakistan na Uturuki.

Alisema kuwa; kwa miaka kadhaa iliyopita, wananchi wa Yemen wamekuwa wakikabiliwa na vita, mashambulizi ya mabomu na mzingiro. Kwa mujibu wake, vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Sana'a, bandari na vituo vya kuvukia mipaka ya nchi kavu vimesababisha matatizo makubwa kwa raia wa kawaida. Aliongeza kuwa dai kuu la Yemen ni kusitishwa mzingiro huo na kuwekwa mazingira yatakayowawezesha wananchi kurejea katika maisha yao ya kawaida.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Wahamiaji wa Yemen alisema kuwa; hapo awali Yemen na Saudi Arabia zilikuwa zimeafikiana kuhusu ramani ya njia ya kutatua mgogoro, lakini serikali ya Saudi Arabia haikutekeleza makubaliano hayo kikamilifu, hali iliyosababisha mambo kurejea katika mwelekeo wa kuongezeka mvutano. Alionya kuwa iwapo mzingiro dhidi ya Yemen utaendelea, upande wa Yemen nao utayachukulia hatua zake dhidi ya Saudi Arabia katika muktadha huo huo.

Abdulwahid Abu Ras alikanusha madai kwamba Yemen inailenga Makkah Tukufu au maeneo mengine matakatifu, akisema kuwa; wananchi wa Yemen wamekuwa wakisisitiza daima umuhimu wa kuheshimu Misikiti Miwili Mitukufu na Qur'ani Tukufu. Vilevile, alipendekeza kuwa nchi za Kiislamu ziwe na wajibu wa pamoja na zishirikiane katika usimamizi na ulinzi wa maeneo matakatifu.

Alielezea kuiunga mkono Palestina na Ghaza kuwa miongoni mwa vipaumbele vya Yemen, huku akisema kuwa nchi hiyo imechukua hatua dhidi ya Israel kwa lengo la kuwaunga mkono wananchi wa Palestina.

Mvutano na Marekani

Akizungumzia mvutano kati ya Yemen na Marekani, Abdulwahid Abu Ras alisema kuwa; operesheni za kijeshi za Marekani dhidi ya Yemen hazikuweza kufikia matokeo yaliyokusudiwa. Aliongeza kuwa baada ya hapo, Washington ilianzisha mawasiliano na Yemen kupitia Oman kwa lengo la kupunguza mvutano.

Wito kwa Pakistan na Uturuki Kutojiingiza Vitani

Abdulwahid Abu Ras alizitaka Pakistan na Uturuki kutojiunga na upande wowote wa kijeshi unaopambana na Yemen, na kujiepusha na hatua zinazoweza kuongeza mvutano katika eneo hilo. Akishukuru nafasi ya Pakistan, alisema kuwa wananchi wa Yemen wanawaheshimu na kuwapenda wananchi wa Pakistan. Kwa mujibu wake, iwapo Pakistan, badala ya kushiriki katika upande wowote wa kijeshi katika mzozo kati ya Saudi Arabia na Yemen, itashirikiana na Iran na Oman katika juhudi za kidiplomasia na upatanishi, Yemen itaipokea kwa furaha hatua hiyo.

Abu Ras aliitaja serikali iliyoko Sana'a kuwa inawakilisha sehemu kubwa ya wananchi wa Yemen, huku akiibua maswali kuhusu kiwango cha uwakilishi wa serikali iliyoko Riyadh, hata hivyo, suala la mamlaka ya kisiasa na uwakilishi nchini Yemen bado linazozaniwa, mivutano kati ya serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa na utawala wa Wahouthi ulioko Sana'a bado inaendelea.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Wahamiaji wa Yemen alionya kuwa, iwapo Saudi Arabia au nguvu nyingine yoyote ya kigeni itafanya operesheni ya kijeshi ya ardhini nchini Yemen, wananchi na vikosi vya kijeshi vya Yemen watapinga hatua hiyo kwa ajili ya kulinda uhuru, mamlaka na ukamilifu wa ardhi ya nchi yao.

Alisisitiza kuwa Yemen haitaki vita, bali inataka kujenga uhusiano na nchi zote kwa msingi wa kuheshimiana, kwa mujibu wake, suluhisho la mgogoro huo linapaswa kutafutwa kupitia kusitishwa mzingiro, kutekelezwa ramani ya njia iliyokubaliwa na kufanyika mazungumzo ya kisiasa kati ya pande mbalimbali za Yemen, badala ya kuchukua hatua za kijeshi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha