Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Ali Taysir, Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Haki za Binadamu nchini Yemen, siku ya Jumatatu alisisitiza kwamba uhalifu wa kuivunjia heshima miili ya mashahidi wa majeshi ya nchi na kuwavua nguo katika mkoa wa Taiz ni uhalifu kamili wa kivita na ukiukwaji mkubwa wa heshima ya mwanadamu.
Taysir amesema: Yale yaliyofanywa na mamluki hawa ni tabia iliyo kinyume na maadili ya dini ya Kiislamu na desturi za makabila ya Yemen. Kuvamia heshima ya waliokufa, kuwapiga picha na kuzisambaza picha hizo kunaonesha kwamba wahusika wamekosa hata viwango vya chini kabisa vya heshima na utu.
Ameeleza: Sheria ya Kimataifa ya Kibinadamu, kwa mujibu wa Kifungu cha (34) cha Mkataba wa Kwanza wa Geneva na Kifungu cha (130) cha Mkataba wa Tatu wa Geneva, inalazimisha kuiheshimu miili ya waliokufa, kuilinda na kukataza kuivunjia heshima miili hiyo.
Ameongeza: Vitendo hivi, kwa mujibu wa vifungu vya (8(b)) na (8(c)) vya Mkataba wa Roma wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, vinachukuliwa kuwa shambulio dhidi ya heshima ya mwanadamu na vitendo visivyo vya kibinadamu vinavyofikia kiwango cha uhalifu wa kivita, na hivyo vinawakilisha ukiukwaji wa sheria.
Amebainisha: Mafundisho ya Mtume Mtukufu (saww) pia yamekataza kuivunjia heshima miili ya maadui.
Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Haki za Binadamu pia ameitaja serikali ya Saudia kuwa mfadhili wa kifedha na msaidizi wa wanamgambo hao, na hivyo kuibebesha jukumu la uhalifu huu.
Mkuu huyo wa baraza ayataka makabila ya Taiz kulaani kitendo hiki na kujitenga na wahusika wake, na ameliomba Shirika la Umoja wa Mataifa pamoja na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kuwaweka wahalifu hao na makamanda wao katika orodha ya wahalifu wa kivita.
Ameeleza mwishoni: Baraza hili limehifadhi ushahidi wa uhalifu huu kwa njia ya sauti na picha, ili kuuwasilisha katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na kuwafuatilia wahalifu hao kupitia taratibu za kisheria.
Maoni yako