Kwa mujibu wa idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Abed ni miongoni mwa takribani Wapalestina 160 ambao kwa sasa wanaishi nchini Mexico. Anauza vyakula vya Kipalestina katika masoko ya Mexico City na kuutambulisha utamaduni wake kwa wananchi wa Mexico.
Sauti kubwa bado humletea wasiwasi Muhammad Abed, ambaye ni mhandisi wa mifumo ya uendeshaji, mwenye asili ya Kipalestina na kutoka Ghaza. Ndege zinazopita angani mwa Mexico City pamoja na milio ya radi ya majira ya kiangazi humrejeshea kumbukumbu za mashambulizi ya mabomu ya Israel dhidi ya Ghaza mwaka 2025, ambapo shambulio la anga lilimuua binti yake mwenye umri wa miaka minne.
Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 36 alifika nchini Mexico katika majira ya kuchipua mwaka uliopita akiwa pamoja na watu 17 wa familia yake waliokuwa wakitafuta hifadhi. Siku hizi, siku za Jumanne asubuhi hazianzi kwa hofu ya mashambulizi ya mabomu, bali huanza kwa kazi. Kabla ya jua kuchomoza, huijaza baiskeli yake ya magurudumu matatu yenye injini kwa vyakula vya Kipalestina, kisha huenda kuviuza katika soko la wazi lililoko Condesa, mojawapo ya maeneo yenye shughuli nyingi na yenye mchanganyiko mkubwa wa kimataifa katika mji mkuu huo.
Hadithi ya uhamiaji wao ilianza baada ya mashambulizi ya mabomu yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wenye umwagaji damu na kuuwawa baadhi ya wanafamilia. Katika safari ya uhamiaji kutokana na mapigano yaliyosababishwa na utawala wa Israel, baadhi ya wanafamilia wengine pia waliuwawa kishahidi.
Kaka mdogo wa Abed, Fadi, pia anauza vyakula vya Kipalestina mjini Mexico City. Pia ana shughuli kubwa katika mitandao ya kijamii, ambako anajitahidi kuitambulisha Palestina. Akitumia jina la mtumiaji hijo.de.palestina (“Mwana wa Palestina”), huchapisha video za biashara yake ya vyakula inayozidi kukua, akizungumza kwa lafudhi nzito ya Kihispania.
Familia ya Abed bado inaendelea kuongezeka, anajitahidi kuwaleta dada zake wawili kutoka Ghaza. Aidha, mwezi Mei, mtoto wake mdogo, Yusuf, alizaliwa mjini Mexico City. Abed alisema: “Amezaliwa Mexico, lakini ana mizizi ya Ghaza moyoni mwake.”
Chanzo: Reuters
Maoni yako