Jumatatu 5 Oktoba 2026 - 09:00
Muqawama Uliilazimisha Marekani Kuondoka Iraq/ Usalama Haupatikani kwa Kujilinda Chini ya Mwavuli wa Marekani

Hawza/ Ustadh Ali Akbar Rashad, akizungumzia kuondoka Marekani nchini Iraq baada ya takribani miaka 22, amesema kuwa; kuondoka huko kulitokana na muqawama, wala si mazungumzo, maridhiano au kulegeza msimamo. Amezitaka pia nchi za eneo hilo kutambua kwamba usalama haupatikani kwa kujilinda chini ya mwavuli wa Marekani.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, ustadh Ali Akbar Rashad, msimamizi wa Jumuia ya Hawza ya Imam Ridha (as) na Mwenyekiti wa Baraza la Hawza ya Mkoa wa Tehran, mwanzoni mwa darsa yake ya juu ya Fiqhi ya Mahakama (Dars Kharij Fiqh al-Qadha), alizungumzia kuondoka Marekani nchini Iraq baada ya takribani miaka 22 ya uwepo na ukaliaji wa nchi hiyo. Pia alifafanua mafunzo ya kihistoria yanayotokana na vita vilivyolazimishwa, kukaliwa Iraq na kushindwa Marekani kutimiza malengo yake katika eneo hili. Alisisitiza kwamba kuondoka Marekani nchini Iraq kulitokana na muqawams, wala si mazungumzo, maridhiano au kulegeza msimamo.

Vita Vilivyolazimishwa: Moja ya Mafunzo ya Historia ya Karibuni

Ustadh Rashad, akieleza kwamba matukio yaliyotokea nchini Iraq katika miongo kadhaa iliyopita yanaweza kutoa mafunzo na mazingatio muhimu kwa historia, alisema: “Moja ya mafunzo hayo yanahusiana na kipindi cha miaka zaidi ya 40 iliyopita, wakati mtu mwenye kiburi, aliyejidanganya mwenyewe na mwenye tamaa ya madaraka alipovamia nchi huru ya Kiislamu iliyokuwa imefanya mapinduzi hivi karibuni na kuhuisha upya mfumo wake wa utawala, katika hali ambayo kwa nje ilionekana kuwa nchi hiyo haikuwa na maandalizi ya kutosha ya kujilinda.”

Aliongeza kwamba Saddam Hussein alikuwa na fikra potofu kwamba angeweza kufika Tehran ndani ya siku tatu na kuuangusha mfumo wa Kiislamu. Pia alikuwa na dhana ya udanganyifu kwamba angeikalia Khuzestan na kuipora Iran.

Mwenyekiti wa Baraza la Hawza ya Mkoa wa Tehran, huku akizungumzia uungaji mkono wa pande zote ambao madola makubwa duniani yaliutoa kwa utawala wa Saddam Hussein, alisema: “Madola yote makubwa yalikuwa nyuma yake; madola ya Magharibi, yaani Marekani na nchi za Ulaya, pamoja na dola ya Mashariki, yaani Umoja wa Kisovieti wa wakati huo. Misaada hiyo ilitolewa katika nyanja za diplomasia, taasisi za kimataifa na silaha. Saddam alipewa silaha za kisasa, silaha za maangamizi ya halaiki na silaha zisizo za kawaida, pamoja na misaada ya kimali na kifedha.”

Ulinzi Mtakatifu: Mfano wa Kusimama Imara kwa Kutegemea Wananchi

Ustaadh Rashad, akizungumzia ushindi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miaka nane ya Ulinzi Mtakatifu, alisema: “Tulipigana kwa ushujaa kwa miaka nane na, kwa mara ya kwanza katika historia yetu, hatukushindwa katika vita, bali tulishinda. Kwa takribani miaka 200, kila nguvu ya kigeni ilipoivamia Iran, sehemu ya ardhi ya nchi yetu ilikuwa ikitenganishwa nayo. Lakini safari hii, hata kipande kimoja cha ardhi ya Iran hakikutenganishwa na nchi hiyo.”

Alitaja mojawapo ya mafunzo muhimu zaidi ya Ulinzi Mtakatifu kuwa ni nafasi ya imani na uungaji mkono wa wananchi, akisema: “Nchi yenye serikali inayotokana na wananchi, iliyochipuka kutoka miongoni mwao na inayotegemea imani na uwezo wa ndani, inaweza, kwa msaada wa imani ya wananchi, azma ya kitaifa na uongozi wa Mwenyezi Mungu, kusimama imara dhidi ya uvamizi mkubwa. Hii inawezekana hata kama nchi hiyo haipati vifaa kutoka kwa mataifa yenye nguvu na haina kabisa silaha za kimkakati na za kiwango cha juu.”

Kuyategemea Madola ya Kigeni: Kosa la Kimkakati

Msimamizi wa Jumuia ya Hawza ya Imam Ridha (as), akizungumzia uvamizi wa Kuwait uliofanywa na Saddam Hussein, alisema: “Baada ya Saddam kukabiliwa na kushindwa na kudhoofika kutokana na vita dhidi ya Iran, aliweza kuikalia nchi jirani ndani ya siku moja au mbili tu. Viongozi wa nchi hiyo walikimbia na kuondoka nchini.”

Alitaja mojawapo ya mafunzo mengine muhimu ya matukio ya eneo hili kuwa ni hatari ya serikali na wananchi kutegemea madola ya kigeni kwa ajili ya kupata usalama, akisisitiza: “Funzo kubwa zaidi ni kwamba serikali na wananchi wanapaswa kuepuka kuufanya usalama wao kuwa tegemezi kwa nguvu ya kigeni ya Marekani.”

Ustaadh Rashad, akizungumzia sababu zilizoipeleka Marekani kuwa na uwepo wa kijeshi nchini Iraq, alisema: “Marekani iliingia tena katika eneo hili na Iraq kwa tamaa ya mafuta na nishati. Saddam hakuweza kusimama imara mbele ya Marekani kwa sababu wananchi hawakuwa nyuma yake, na hatimaye alikamatwa katika hali ile ya kufedheheshwa.”

Akisimulia kumbukumbu aliyosimuliwa na ndugu yake aliyekuwa shahidi kuhusu hali ya Saddam baada ya kukamatwa, aliongeza: “Ndugu yangu alinisimulia kwamba; Saddam alipotolewa katika shimo jeusi akiwa katika hali ya udhalili mkubwa, na askari alipoweka buti zake usoni mwake, nilimwonea huruma, sikutaka hata adui yangu adhalilishwe kwa namna hiyo.”

Marekani Iliingia Iraq kwa Kisingizio cha Usalama

Rashad akipinga madai ya Marekani kwamba uwepo wake katika eneo hili ulikuwa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi, alisema: “Si kweli kwamba nguvu fulani inapoingia katika eneo hili tunapaswa kudhani kwamba imekuja kwa sababu ya kutujali. Marekani ilikuja, na mara tu ilipoyapata mafuta, ilijikita hapo na kuendeleza uwepo wake.”

Akizungumzia madai ya Marekani kuhusu kuwepo kwa silaha za nyuklia na silaha za maangamizi ya halaiki nchini Iraq, alisema: “Marekani ilidai kwamba Saddam alikuwa na silaha za nyuklia na kwamba inaingia Iraq ili kuziharibu. Hali halisi ni kwamba jambo hilo halikuwepo kabisa; na hata kama silaha hizo zingekuwapo, hawakuweza kuzigundua wala kuziharibu.”

Msimamizi wa Jumuia ya Hawza ya Imam Ridha (as) aliongeza kwamba Marekani ilitumia kisingizio hicho ili kutawala rasilimali nyingi za nishati zilizopo katika eneo hili, na kwa kweli ndivyo ilivyofanya.

Muqawama wa Iraq: Sababu ya Kuondoka Marekani

Ustaadh Rashad, akieleza mkanganyiko uliopo kati ya madai ya Marekani ya kuwa dola yenye nguvu kubwa na hali halisi iliyopo katika medani, alisema: “Marekani, ikiwa katika kilele cha madai yake ya kuwa dola kuu duniani, inazitishia nchi kadhaa kwa kusema kwamba itaingia na kuziteka, lakini wakati huohuo inajiondoa katika eneo jingine ambalo hapo awali ilikuwa imelivamia na kulikalia.”

Akijibu swali kuhusu nguvu iliyoshindwa na Marekani kiasi cha kushindwa kuendeleza uwepo wake nchini Iraq, alisema: “Marekani haikushindwa na serikali ya Iraq, wala hata na jeshi la sasa la Iraq, bali ilipata fedheha hii mbele ya muqawama wa Al-Hashd al-Shaabi.”

Mwenyekiti wa Baraza la Hawza ya Mkoa wa Tehran alisisitiza kwamba; Wamarekani walishindwa mbele ya jukwaa la muqawama la Iraq na wakalazimika kuondoka katika eneo hilo.

Akizungumzia makundi mbalimbali ya muqawama nchini Iraq na uhusiano wao na harakati za muqawama katika eneo hili na duniani kwa ujumla, alisema: “Nguvu ya muqawama wa Iraq inaundwa na makundi kadhaa ambayo kwa ujumla wake yanaweza kuitwa jukwaa moja. Jukwaa hili linajumuisha harakati za muqawama katika eneo hili na hata katika kiwango cha dunia, na leo hii zimeungana na kuwa na mshikamano.”

Usalama Haupatikani Chini ya Mwavuli wa Marekani

Ustaadh Rashad, akizungumzia ujumbe unaopaswa kupatikana kutokana na matukio haya kwa nchi za eneo hili, alisema: “Nchi hizi ambazo kwa mwonekano zinajiita nchi huru zinapaswa kujua kwamba usalama haupatikani chini ya mwavuli wa Marekani.”

Aliongeza: “Marekani ilikaa Iraq kwa miaka 22, lakini matokeo ya uwepo wake yalikuwa uporaji wa mafuta na kuacha idadi kubwa ya watu wakiwa wameuawa. Huo ndio usalama ambao Marekani inadai kuiletea nchi za eneo hili.” Rashad alieleza matumaini yake kwamba nchi za eneo hili zitautambua ukweli huo na kujifunza kutokana na tukio hilo.

Marekani Haikuondoka Iraq kwa Mazungumzo na Maridhiano

Msimamizi wa Jumuia ya Hawza ya Imam Ridha (as), akisisitiza kwamba ushindi haupatikani kwa kutegemea silaha pekee wala mazungumzo pekee, alisema: “Kuondoka Marekani nchini Iraq hakukupatikana kupitia mazungumzo, wala hakukutokana na kulegeza msimamo, kujisalimisha au kufanya maridhiano. Badala yake, ni muqawama ulioilazimisha Marekani kuondoka.”

Aliongeza: “Makundi kadhaa ya watu wa dini, waumini na wapiganaji wa jihadi, ambao hawakuwa na silaha kubwa za kimkakati wala silaha za kiwango cha juu, yalisimama mbele ya dola kuu inayojiona kuwa ndiyo yenye nguvu zaidi duniani. Ni kundi hili la waumini na watu wa dini ambalo, kupitia muqawama wake, liliilazimisha Marekani kuondoka katika nchi yao.”

Mazungumzo Hayapaswi Kufanywa Mkakati Mkuu

Ustadh Rashad, huku akisisitiza umuhimu wa baadhi ya viongozi wa nchi kujifunza kutokana na uzoefu wa Iraq, alisema kwamba sehemu hii ya matukio ya Iraq inapaswa kuwa funzo kwa baadhi ya viongozi wa nchi yao ili wasitegemee sana mazungumzo na kuendelea kuyapigia debe.

Aliendelea kusema: “Hatudai kwamba mazungumzo yamekatazwa kabisa, lakini hatupaswi kuyawekea matumaini yetu yote. Kwa hakika, mazungumzo hayo si ya pande mbili zilizo sawa; upande mmoja unataka kulazimisha matakwa yake kwa upande mwingine.”

Mwenyekiti wa Baraza la Hawza ya Mkoa wa Tehran alisisitiza: “Unapoketi kwenye meza ya mazungumzo na kudhani kwamba upande wa pili unakutambua kama mshiriki huru na aliye sawa naye, ilhali kwa msingi haukutambui hata kama upande unaopaswa kuzungumza nao, huwezi kuweka matumaini yako katika matokeo ya mazungumzo hayo.”

Marekani Haijawahi Kuheshimu Ahadi Zake

Mwalimu Rashad, akizungumzia historia ya Marekani ya kuvunja ahadi na mikataba, aliuliza: “Ni mara ngapi wanapaswa kuvunja ahadi na mikataba yao? Je, wamewahi hata mara moja kutimiza ahadi zao?”

Aliongeza kwamba tangu kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kupitia mkataba uliohusiana na tukio la kutekwa ubalozi wa Marekani uliotajwa kama pango la ujasusi na Makubaliano ya Algiers, hadi uzoefu wa hivi karibuni walioupata mwaka huu, wamekuwa wakikabiliwa na uvunjaji wa ahadi.

Akisisitiza kwamba, tatizo kuu halihusu tu vifungu vilivyoandikwa katika mikataba, alisema: “Inawezekana kwenye karatasi ikaonekana kwamba kuna vifungu vinne vinavyomnufaisha upande wa pili na vifungu 10 vinavyotunufaisha sisi. Lakini tatizo ni kwamba upande wa pili hauikubali karatasi hiyo kwa maana ileile tunayodhani sisi.”

Ustaadh Rashad, akikosoa matumizi ya mara kwa mara ya neno ‘makubaliano ya maelewano’ katika kauli za baadhi ya viongozi, alisema: “Wakati upande wa pili haukubali wajibu wowote, basi hakuna tena maelewano. Viongozi hawapaswi kuendelea kuzungumzia makubaliano ya maelewano na mambo ambayo kimsingi hayakujumuishwa katika maelewano hayo.”

Teknolojia ya Nyuklia: Ina Maana Kubwa Zaidi ya Silaha

Msimamizi wa Jumuia ya Hawza ya Imam Ridha (as), katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akizungumzia baadhi ya mitazamo inayotaka kuachwa kwa teknolojia ya nyuklia kwa lengo la kuzuia vita, alisema: “Mara kwa mara tunasikia baadhi ya watu wakisema kwamba ikiwa suala la nyuklia linahusu silaha na limekuwa kisingizio cha vita, na sisi hatutaki kupigana, basi tuachane nalo na kuliondoa kabisa.”

Akisisitiza umuhimu wa kutambua thamani ya teknolojia ya nyuklia, alisema: “Teknolojia ya nyuklia si silaha tu. Silaha yetu changamani ni imani yetu. Inawezekana mtu akasema kwamba hatuhitaji silaha za nyuklia, lakini teknolojia ya nyuklia ni suala tofauti.”

Melim Rashad aliongeza: “Leo hii, teknolojia ya nyuklia inamaanisha kilimo, viwanda, dawa, tiba na teknolojia. Kwa sasa, teknolojia ya nyuklia ni ishara, dhihirisho, kilele na hatua ya juu zaidi ya maendeleo ya kila nchi na ustaarabu duniani.”

Aliendelea kusema kwamba, leo hii kuwa na teknolojia ya nyuklia ni miongoni mwa vigezo vinavyotumika kupima maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia ya nchi, huku maadui wakipinga maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kuondoka Marekani Iraq: Mwanzo wa Kuondoka Katika Eneo Hili

Mwisho wa hotuba yake, ustaadh Rashad alieleza furaha yake kutokana na kuondoka Marekani nchini Iraq, akisema: “Tunafurahi sana kwamba Marekani, ikiwa katika kilele cha kiburi chake, kujidanganya na madai yake makubwa, leo hii inaondoka katika eneo hili.”

Alitaja tukio hilo kuwa mwanzo wa kuondoka kwa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, akisema: “Tunatumaini kwamba mwenendo huu utaendelea katika maeneo mengine ya dunia ambayo bado yanakaliwa kwa mabavu.”

Msimamizi wa Jumuia ya Hawza ya Imam Ridha (as) aliongeza: “Mungu akipenda, katika siku zijazo tutashuhudia Marekani ikilazimika kuondoka katika eneo hili lote, kwa sababu haina tena usalama katika eneo hili.”

Alibainisha kwamba nguvu iliyoingia katika eneo hili kwa kisingizio cha kuhakikisha usalama sasa yenyewe inakabiliwa na ukosefu wa usalama na inalazimika kujitahidi kujilinda.

Mwisho, ustaadh Rashad alieleza matumaini yake kwamba; kuondoka Marekani nchini Iraq kutakuwa mwisho wa ukaliawaji wa nchi hiyo na mwanzo wa uhuru na kujitawala kwa eneo hili.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha