Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kitengo cha habari za kimataifa, tukio hilo lilipokelewa kwa shauku kubwa na kundi la vijana, wanaharakati wa utamaduni, wasomi wa vyuo vikuu na watu wanaopenda maarifa ya Ahlul-Bayt (as) pamoja na harakati za Muqawama. Aidha, ujumbe wa ngazi ya juu ulioundwa na manaibu wakuu wa Hawza za kielimu nchini Iran ulihudhuria mkutano huo na kutoa hotuba. Ujumbe huo ulijumuisha Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Mufid Kuhsari, Naibu wa Masuala ya Kimataifa; Hujjatul-Islam wal-Muslimin Abbasi, Naibu wa Utafiti; Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rezaei, Naibu wa Mipango na Usimamizi wa Kimkakati; na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Alamzadeh, Naibu wa Malezi na Utakaso wa Nafsi.
Kusisitiza nafasi ya imani na uelewa wa kina wa vijana katika kukabiliana na changamoto
Mwanzoni mwa mkutano huo, Hujjatul-Islam Mohsen Nakhaei, mwakilishi wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (as) nchini Lebanon, aliwakaribisha wageni na washiriki, kisha akachambua nafasi muhimu ya imani na ufahamu katika kukabiliana na migogoro.
Akizungumzia msimamo thabiti wa kizazi cha vijana mbele ya mitihani mbalimbali, alisema: “Daima, tunapovuka matukio na matatizo mbalimbali, tumekuwa tukishuhudia kukua na kukomaa kwa imani, uimara wa msimamo na uelewa wa kina wa vijana katika njia ya kufikia utukufu na heshima ya Kiislamu. Jambo hili linaonesha kina cha athari za fikra za Ahlul-Bayt (as) katika itikadi na imani za kizazi kipya.”
Kuchunguza vipengele vya uimara na mustakabali wa harakati za Muqawama
Katika sehemu iliyofuata, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rezaei, Naibu wa Mipango na Usimamizi wa Kimkakati wa Hawza, alifafanua vipengele mbalimbali vya nafasi na mchango wa vijana katika mustakabali wa Muqawama.
Akifafanua misingi ya kidini ya ulinzi, alisisitiza umuhimu wa kushikamana na mifano ya kidini katika kuelekeza harakati za vijana. Pia, alirejea vipengele vikuu vya ustahimilivu na uimara kwa kuzingatia maarifa ya Kiislamu pamoja na mwenendo wa kielimu na kiutendaji wa madhehebu ya Ahlul-Bayt (as).
Kutoka katika “Muqawama wa Kijeshi wa Kujilinda” hadi “Muqawama wa Kijamii”
Baadaye, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Abbasi, Naibu wa Utafiti wa Hawza za Kielimu, alitoa hotuba na kusisitiza umuhimu wa kupanua dhana na muundo wa kielelezo cha Muqawama. Akizungumzia ulazima wa kuvuka mipaka ya mifumo inayojikita tu katika “ulinzi” na kuingia katika uwanja wa “Muqawama wa Kijamii”, alisema: “Vijana wanapaswa, kwa kutegemea mafundisho ya Ahlul-Bayt (as), kuimarisha na kueneza kielelezo cha maisha ya Muqawama katika nyanja zote za jamii, zikiwemo utamaduni, uchumi na mahusiano ya kijamii, ili Muqawama ugeuke kuwa mtindo wa maisha endelevu na wenye nguvu.”
Malezi ya kishujaa na jihadi; wajibu wa vijana katika kuweka mazingira ya kudhihiri Imam Mahdi (aj)
Katika sehemu nyingine ya programu, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Alamzadeh, Naibu wa Malezi na Utakaso wa Nafsi wa Hawza, alichunguza suala la malezi ya kishujaa na jihadi kwa mtazamo wa Qur’ani Tukufu na riwaya. Kwa kutegemea aya za Qur’ani Tukufu, alifafanua dhana sahihi ya “kungojea faraja” (Intidhār al-Faraj), na kusisitiza akisema: “Uelewa sahihi kuhusu kudhihiri Imam Mahdi (aj) unahitaji vijana wenye ufahamu na waliojiandaa binafsi kushiriki kikamilifu katika kuweka mazingira ya kudhihiri kwake. Malezi ya jihadi hayahusiani tu na kushiriki katika uwanja wa mapambano ya kivita, bali kujijenga kimaadili na kuwajibika kijamii ni miongoni mwa masharti muhimu kwa vijana wanaosubiri kudhihiri Imam Mahdi (aj) katika zama hizi.”
Vipengele vya Muqawama wa wananchi na mifumo yake ya kiitikadi
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Mufid Kuhsari, Naibu wa Masuala ya Kimataifa wa Hawza za Kielimu, alichambua harakati za wananchi kwa mtazamo wa kimuundo na kiitikadi. Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kuhsari alifafanua vipengele vikuu vinavyoimarisha uimara katika Muqawama wa wananchi, na kuchunguza misingi ya kiitikadi na kimawazo ya harakati hizo katika eneo hilo.
Maoni yako