Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Mousawi, Imam wa Swala ya Ijumaa ya Baghdad na miongoni mwa walimu mashuhuri wa Hawza ya Najaf Tukufu, katika khutba yake ya kisiasa ya tarehe 2 Oktoba 2026 (10 Mehr 1405), huku akirejea msisitizo wa viongozi wa Iraq kuhusu kuondoka kikamilifu majeshi ya Marekani na majeshi ya kigeni nchini humo, alieleza matumaini kwamba kauli hizo ni za kweli. Hata hivyo, alisema uzoefu wa huko nyuma umesababisha wananchi wa Iraq kutokuwa na imani kamili na ahadi za Marekani.
Imam wa Swala ya Ijumaa ya Baghdad, huku akiuliza sababu halisi ya kuondoka majeshi ya Marekani nchini Iraq, alikataa kuhusisha kuondoka huko pekee na mazungumzo au ombi la Serikali ya Iraq, na kusema kwamba Marekani hadi dakika za mwisho ilitaka kuyahifadhi majeshi yake nchini Iraq, hususan katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Ayatullah Mousawi alisisitiza: “Ni Muqawama wa Kiislamu nchini Iraq uliyoilazimisha Marekani kuondoka, na kwa kulenga kambi na maeneo yalipokuwa yamewekwa majeshi ya Marekani, uliweka mazingira ya kuondoka kwao; lau Muqawama usingekuwepo, majeshi ya Marekani yasingeondoka Iraq.”
Aidha, alionya dhidi ya kuudhoofisha Muqawama au kupuuzia umuhimu wa silaha zake akisema kwamba; hatua kama hiyo ingeifanya Iraq kuwa katika mazingira ya kuathiriwa na Marekani na huenda ikatengeneza mazingira ya kurejea tena majeshi ya Marekani nchini humo.
Imam wa Swala ya Ijumaa ya Baghdad, katika muktadha huo, alikosoa jitihada za baadhi ya viongozi za kuhusisha kuondoka majeshi ya Marekani na utendaji wa serikali za Iraq, na kusisitiza kwamba ni wananchi wa Iraq ambao, kwa subira, kujitolea na Muqawama wao, walipata mafanikio hayo. Alitaja kuondoka majeshi ya Marekani kuwa ni kushindwa kwa mradi wa Marekani nchini Iraq na katika eneo hilo.
Ayatullah Mousawi aliendelea kwa kurejea mabadiliko ya Iraq na misimamo ya baadhi ya nchi za Kiarabu na za eneo hilo akisema; baadhi ya nchi hizo zilikuwa zikitegemea msaada wa Marekani. Hata hivyo, mabadiliko ya eneo yameonesha kwamba uwezo wa Marekani wa kutoa usalama na kuwalinda washirika wake una mipaka, na kwamba nchi hiyo haiwezi kuwalinda washirika wake wote.
Imam wa Swala ya Ijumaa ya Baghdad pia alisisitiza kuhusu maana ya utawala na mamlaka ya nchi, akisema kwamba; mamlaka ya nchi maana yake ni Serikali ya Iraq kuwa huru katika kufanya maamuzi yake na kutokubali kusalimu amri mbele ya matakwa ya nchi yoyote ya kigeni, iwe Marekani, Saudi Arabia, Uturuki, Jordan au Iran. Pia alisisitiza kwamba mamlaka ya nchi maana yake ni kuheshimu matakwa ya wananchi na kuitikia madai yao.
Ayatullah Mousawi, akikosoa udhaifu wa msimamo wa Iraq mbele ya baadhi ya nchi jirani, alirejea suala la Khor Abdullah na uhusiano kati ya Iraq na Kuwait akisema kwamba; serikali yenye nguvu ni ile inayolinda haki na heshima ya Iraq na isiyoruhusu matakwa ya kigeni kulazimishwa dhidi ya nchi hiyo.
Aidha, alikosoa utegemezi wa Iraq kwa baadhi ya nchi za eneo hilo badala ya kuimarisha uwezo wake wa ndani, na kusisitiza kwamba nguvu ya Iraq inapaswa kujengwa juu ya wananchi, Muqawama, uwezo wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama wa nchi hiyo.
Imam wa Swala ya Ijumaa ya Baghdad, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alisifu nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuunga mkono masuala ya eneo, hususan suala la Ghaza, na akakataa kwamba msaada huo unatolewa kwa lengo la maslahi ya Iran pekee.
Alisisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imegharamia gharama kubwa na kukabiliwa na mashinikizo mengi kutokana na kuunga mkono masuala ya Umma wa Kiislamu.
Ayatullah Sayyid Yasin al-Mousawi, mwishoni, alisisitiza umuhimu wa Iraq kuwa na maamuzi huru na kuwa na vipengele vya nguvu vinavyohitajika ili kulinda mamlaka na heshima ya nchi hiyo, akisema kwamba; mamlaka ya nchi si kauli mbiu tu, bali ni msimamo wa kisiasa na kiutendaji kwa ajili ya kuyalinda maslahi ya wananchi wa Iraq.
Maoni yako