Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Muhammad Hasan Abuturabi-Fard, katika khutba za Swala ya Ijumaa ya wiki hii, tarehe 10 Mehr 1405 (2 Oktoba 2026), zilizofanyika katika Chuo Kikuu cha Tehran, alipokuwa akielezea nafasi ya kumwabudu Mwenyezi Mungu na athari yake katika mahusiano ya kijamii, alisema: “Kwa kumtambua Mwenyezi Mungu Mtukufu na kujipamba na daraja la uja, mwanadamu hajidhulumu nafsi yake, bali huiheshimu na kuiweka katika daraja za juu za ukamilifu. Ni kupitia kurekebisha uhusiano na Mwenyezi Mungu Mtukufu ndipo uhusiano wa mtu na jamii pia unaporekebika.”
Akiashiria kwamba jamii inayosonga kwa msingi wa akili, elimu na maarifa, na ambayo imepambwa kwa fadhila za kimaadili, ni jamii inayohifadhi haki za wanadamu, aliongeza: “Qur’ani Tukufu imeeleza wazi kwamba kauli, mazungumzo ya siri na vikao vinavyofanyika mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu vinavyoheshimiwa ni vile ambavyo matokeo yake yanakuwa ni kukabiliana na kila kauli na mwenendo ambao haukubaliwi na akili wala Sharia, na ambao matokeo yake ni kuikuza jamii na kuipamba kwa mema. Katika mambo yote mema, kuna jambo moja ambalo limesisitizwa zaidi kuliko yote, nalo ni ‘islahi baina ya watu’ (kurekebisha uhusiano miongoni mwa watu).”
Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran alisisitiza: “Tunapaswa kuchukua hatua katika njia ya kurekebisha uhusiano wetu na wengine; kwa sababu hatua ya kwanza katika kuiimarisha jamii ya kidini ni kurekebisha uhusiano baina ya waumini. Ikiwa kundi hili litaimarika na mahusiano baina ya watu yakarekebishwa, njia ya kuirekebisha jamii ya wanadamu pia itakuwa rahisi. Maamrisho ya Uislamu, hata hukumu zile zinazowekwa katika kundi la ibada, kila moja ina nafasi muhimu katika kurekebisha mahusiano ya kijamii na mwingiliano wa wanadamu wao kwa wao.”
Mabadiliko katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ni ishara ya kudhoofika tawala ya Magharibi na kuamka mataifa mengine
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Abutorabi-Fard pia alizungumzia kufanyika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, uliowakutanisha viongozi wa nchi mbalimbali, na kusema: “Yaliyotokea katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ilikuwa tafsiri ya kudhoofika kisiasa kwa Magharibi, machweo ya nguvu ya Marekani na kuchipuka misingi safi ya kimantiki na kimaadili katika fikra za Mapinduzi ya Kiislamu.”
Imam wa Muda wa Swala ya Ijumaa Tehran aliendelea: “Dunia ya leo inakabiliwa na matukio na mabadiliko ya kimsingi, na leo sauti ya kutoridhika mataifa na serikali za dunia inasikika kwa nguvu zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Kuondoka wajumbe 77 wakati Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni alipokuwa akihutubia katika ukumbi wa Mkutano Mkuu ni ushahidi wa wazi wa ukweli huu.”
Alisema: “Uamsho huu mkubwa wa kisiasa wa watu duniani, harakati ya kasi ya Umma wa Kiislamu ya kurejea katika utambulisho wake safi wa kidini na kimaadili, kuongezeka nguvu ya Mhimili wa muqawama na ushindi unaovutia mbele ya Marekani, utawala wa Kizayuni na madola yanayounga mkono kambi ya Magharibi, yote yanaashiria mabadiliko katika mizani ya nguvu na mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi mwanzoni mwa milenia ya tatu. Kudhoofika Magharibi ni ishara ya mwisho wa mfumo wa upande mmoja katika dunia.”
Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran alisema: “Kwa kuangalia uvamizi mkubwa na wa kujigamba wa Marekani na Magharibi dhidi ya Afghanistan na Iraq kwa lengo la kubadilisha ramani ya Mashariki ya Kati kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni na Marekani, tunaweza kutambua umuhimu wa matukio haya.
Nchi ya Kiislamu ya Afghanistan ilikuwa chini ya uvamizi wa Marekani na washirika wake kuanzia mwaka 2001 hadi 2021, yaani kwa takribani miaka 20. Nchi yetu pendwa ya Iraq nayo mwaka 2003 ilikabiliwa na uvamizi wa vikosi vya kivita vya Marekani vilivyokuwa na magari ya kivita na mitambo ya kijeshi, kwa msaada wa kambi ya Magharibi.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Abutorabi-Fard alisisitiza: “Waziri wa Ulinzi wa wakati huo wa Marekani katika serikali ya George W. Bush, akiwa katika kambi ya anga ya Whitman, katika miaka ambayo ndege za B-2 zilikuwa zikitumwa katika anga ya Afghanistan, alidai kwa kujigamba kwamba ndege hizi za kivita huvuka bahari na mabara bila kuonekana, na huleta haki kutoka angani hadi ardhini. Vilevile, George Bush katika hafla ya mwaka 1383 Hijria Shamsia (2004) alidai kwamba anatumia vikosi vya kijeshi kwa ajili ya kueneza demokrasia, uhuru na kukomesha uasi.”
Kuondoka Marekani nchini Iraq ni mwanzo wa kuiweka Iraq katika nafasi ya uhuru na utukufu
Imam wa Muda wa Swala ya Ijumaa Tehran alizungumzia kuondoka Marekani nchini Iraq na kusema: “Mataifa ya Kiislamu yalishuhudia demokrasia ya Marekani ilileta zawadi gani kwa eneo hili, na jinsi damu safi ya mamia ya maelfu ya Waislamu, wakiwemo wanawake, wanaume na watoto, ilivyomwagika nchini Afghanistan na Iraq. Jinai za kutisha za Marekani na washirika wake wa Magharibi hazijafichika kwa mtu yeyote duniani. Sambamba na kuuwawa kishahidi maelfu ya Wairaqi, kwa mujibu wa ripoti ya Reuters, katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili ya operesheni za kijeshi nchini Iraq, takribani wanajeshi 4,500 wa Marekani pia waliuawa.”
Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran aliongeza: “Kuondoka Wamarekani nchini Iraq ni mwanzo wa kuwaweka watu na serikali ya Iraq katika nafasi ya uhuru na utukufu; kama ambavyo kuondoka Marekani nchini Afghanistan kutakuwa mwanzo wa heshima na nguvu kwa taifa letu pendwa na ndugu la Afghanistan.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Abutorabi-Fard alieleza: “Leo, msaada mkubwa zaidi wa kijeshi wa Marekani unaelekezwa kwa utawala wa Kizayuni, lakini muqawama wa taifa pendwa la Iran, Mhimili wa muqawama, pamoja na mataifa mashujaa ya Afghanistan, Iraq, Lebanon, Gaza, Palestina, Yemen na ulimwengu mzima wa Kiislamu, ndio mwanzo wa kukomesha uwepo huu wa aibu.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Abutorabi-Fard, akizungumzia vita vya Marekani dhidi ya Iran, aliendelea: “Gazeti la Wall Street Journal limeandika katika makala moja kwamba; vita dhidi ya Iran vilifichua ukweli usiopendeza kwa Marekani. Washington ilijifunza kwamba haiwezi kuendesha vita vifupi dhidi ya dola yenye nguvu ya kikanda bila kudhoofisha akiba na silaha zake muhimu. Hili ni somo ambalo ninyi taifa kubwa la Iran, ninyi wapiganaji mashujaa wa Faraja (Polisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran), na ninyi mashujaa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Jeshi la Iran, mmeifundisha Marekani na washirika wake.”
Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran alisema: “Mwanachama mwandamizi wa Taasisi ya Brookings anahitimisha kwamba tukio hili la tatu la Marekani la kujihusisha katika eneo hili (Vita vya Ramadhani, Vita vya Hormuz), huenda likawa tukio la mwisho la Marekani katika eneo hili. Kwa mujibu wa alichoandika, vita hivi vinaashiria mwisho wa juhudi za Marekani za kulitawala eneo hili. Huu ndio mtazamo wa wachambuzi wenye uelewa duniani kuhusu vita hivi visivyo na uwiano na ushindi wa taifa kubwa la Iran.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Abutorabi-Fard alisisitiza: “Tunapaswa kuulinda ushindi huu mkubwa. Kuulinda ushindi huu ni matokeo ya umoja, mshikamano wa kitaifa na subira ya pamoja ya taifa kubwa la Iran. Kulinda mafanikio haya kunategemea kuimarisha uhusiano baina ya makundi yote ya taifa pendwa la Iran, kuimarisha mshikamano wa mihimili mitatu ya dola na kuimarisha uhusiano usiokatika kati ya taifa na mfumo wa Kiislamu chini ya mhimili wa uongozi wa hekima wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Tunapaswa kuilinda hazina hii kubwa kwa kutumia busara, imani na subira, na Inshaallah tushuhudie ushindi mkubwa zaidi kwa Umma wa Kiislamu.”
Maoni yako