Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Alireza Panahiyan, katika hafla ya maombolezo ya usiku wa kumbukumbu ya kifo cha Karima wa Ahlul-Bayt (s.a.), iliyofanyika katika ukumbi wa Imam Khomeini (ra) ndani ya Haram Tukufu ya Hadhrat Fatima Ma’asuma (s.a.), huku akitoa salamu za rambirambi kufuatia kufariki dunia Ayatullah Al-dhzma Shubairi Zanjani (ra) na kwa mnasaba wa siku za maombolezo ya Bibi wa Karama, alizungumzia nafasi yake ya kielimu na kiroho, akasema: Miongoni mwa sababu za ukuu wa Bibi Ma’asuma (s.a.) ni nafasi yake ya kielimu; kiasi kwamba hata alipokuwa mtoto alikuwa akijibu masuala ya fiqhi, na Imam Musa Kadhim (a.s.) alithibitisha usahihi wa majibu yake.
Alieleza kwamba heshima ya pekee wanayopewa Bibi Fatima Ma’asuma (s.a.) na wanazuoni pamoja na watu wakubwa si jambo linalotokana na heshima ya watu wa kawaida pekee, bali akaongeza: Wanazuoni na wataalamu wakubwa wa elimu ya kiroho pia daima wamekuwa wakimuheshimu kwa namna ya pekee mwanamke huyu mtukufu, na Haram yake Tukufu imekuwa mojawapo ya vituo muhimu zaidi vya kielimu na kiroho katika ulimwengu wa Ushia.
Mwalimu huyu wa Hawza alisisitiza: Bibi Fatima Ma’asuma (s.a.) ni kielelezo dhahiri cha nafasi ya juu ya mwanamke katika Uislamu, na ukuu wake wa kielimu na kiroho unaonesha kwamba katika utamaduni wa Kiislamu, mwanamke anaweza kufikia daraja ambayo wanazuoni na mafakihi wakubwa huonesha unyenyekevu mbele ya hadhi yake.
Akizungumzia uhusiano uliopo baina ya heshima na hijabu, alibainisha: Wasichana na wanawake wa jamii ya Kiislamu wanapaswa kumtambua Hadhrat Ma’asuma (s.a.) kuwa ni mfano wa heshima na utukufu; kwa sababu mtu anapohisi kuwa ana heshima na hadhi, mienendo mingi sahihi pia huimarika ndani yake, na hijabu ni miongoni mwa matokeo ya heshima na utukufu huo.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Panahiyan, huku akisisitiza umuhimu wa elimu na faqihi katika Uislamu, alisema: Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’ani Tukufu: “لِیَتَفَقَّهُوا فِی الدِّینِ”, na aya hii inaonyesha kwamba miongoni mwa waumini lazima kuwe na kundi linalojitahidi kupata uelewa wa kina wa maarifa ya dini na kupata utaalamu katika uwanja huo.
Aliendelea kusema: Jamii inahitaji elimu na uelewa ili kutatua matatizo yake mbalimbali, na masuala mengi ya kiutamaduni, kiuchumi na kijamii hayawezi kutatuliwa bila kuwa na maarifa na mipango ya kisayansi. Hawza na vyuo vikuu pia vinapaswa kuongeza juhudi zaidi katika uzalishaji wa elimu na malezi ya wataalamu wenye ujuzi.
Mwalimu huyo wa Hawza na Chuo Kikuu, huku akizungumzia umuhimu wa kuwa karibu na Qur’ani katika maisha ya wanazuoni, alirejea kumbukumbu moja kuhusu Ayatullah Al-Udhma Shubairi Zanjani na kusema: Mara nyingi nimekuwa nikishuhudia kwamba katika muda mfupi aliokuwa nao kabla ya kusimamisha Swala katika eneo alilokuwepo, alikuwa akiitoa Qur’ani mfukoni mwake na kuanza kuisoma; tabia hii ilikuwa ikionesha namna alivyokuwa akitumia kwa umakini kila dakika ya maisha yake na jinsi alivyokuwa na mazoea ya kudumu ya kuwa karibu na Qur’ani.
Akisisitiza umuhimu wa kuimarisha taaluma za kielimu katika Hawza, alisema: Hawza inapaswa kuongeza juhudi katika kutambulisha uwezo wake wa kielimu kwa vijana, ili kizazi cha vijana kifahamu elimu na taaluma mbalimbali zinazofundishwa katika Hawza na kijue kwamba ndani ya Hawza kuna shughuli nyingi na pana za kielimu zinazofanyika.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Panahiyan, akizungumzia nafasi ya Bibi Fatima Ma’asuma (s.a.) katika kuundwa utambulisho wa kielimu wa mji wa Qum, alisema: Kuwepo mwanamke huyu mtukufu mjini Qum, sambamba na uwezo wa kielimu na kiroho wa mji huu, ilikuwa sababu ya kuibuka kituo kikubwa cha kielimu na kifaqihi, na leo Qum inatambulika kuwa miongoni mwa vituo muhimu zaidi vya elimu za Kiislamu.
Mwisho, akizungumzia siku za maombolezo ya Bibi Fatima Ma’asuma (s.a.), alisisitiza umuhimu wa kumfahamu zaidi Bibi huyo na mwenendo pamoja na shakhsia yake ya kielimu na kiroho, na akamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awajaalie waumini wanufaike na shafaa ya Karima wa Ahlul-Bayt (s.a.), na aharakishe kudhihiri Hadhrat Waliyyul-Asr (a.j.).
Maoni yako